Muda wa Kuondolewa Vituo vya Kijeshi vya Marekani Barani Ulaya Umeshaanza Rasmi?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i138128-muda_wa_kuondolewa_vituo_vya_kijeshi_vya_marekani_barani_ulaya_umeshaanza_rasmi
Wizara ya vita ya Marekani Pentagon imetangaza rasmi kuwa, itawaondoa wanajeshi 5,000 wa nchi hiyo walioko Ujerumani; uamuzi ambao utatekelezwa ndani ya muda wa miezi sita hadi kumi na mbili ijayo.
(last modified 2026-05-03T09:56:47+00:00 )
May 03, 2026 09:48 UTC
  • Muda wa Kuondolewa Vituo vya Kijeshi vya Marekani Barani Ulaya Umeshaanza Rasmi?

Wizara ya vita ya Marekani Pentagon imetangaza rasmi kuwa, itawaondoa wanajeshi 5,000 wa nchi hiyo walioko Ujerumani; uamuzi ambao utatekelezwa ndani ya muda wa miezi sita hadi kumi na mbili ijayo.

Maafisa wa Marekani wamesema, uamuzi huo ni mjibizo wa kuongezeka hitilafu kati ya Washington na washirika wake wa Ulaya hususan kuhusiana na vita vya Iran. Kuondolewa wanajeshi wa Marekani nchini Ujerumani si mabadiliko ya kitaktiki tu. Hatua hiyo inaashiria kufifia kidogo kidogo muungano ambao kwa muda wa miaka 70 ulikuwa ndio uti wa mgongo wa usalama wa nchi za Magharibi. Baada ya Japan, Ujerumani ndiyo nchi ya pili yenye kambi kubwa zaidi ya kijeshi ya Marekani nje ya nchi. Kuna wanajeshi 36,400 wa Marekani waliopiga kambi ndani ya ardhi ya nchi hiyo.
Makao makuu ya Kamandi ya Marekani ya Ulaya na Afrika yako katika mji wa Stuttgart. Kituo cha jeshi la anga cha Ramstein ndicho kinachoratibu operesheni za Marekani katika Asia Magharibi. Hospitali kubwa zaidi ya kijeshi ya Marekani nje ya ardhi yake iko Ujerumani pia katika mji wa Landstuhl. Taasisi hizo ni mtaji wa uwekezaji wa miongo kadhaa. Kuanzisha mbadala wa vituo hivyo katika nchi za Poland au Italia kutagharimu mabilioni ya dola na kuchukua muda wa miaka kadhaa hadi kukamilika. 
Moja ya sababu kuu za kuchukuliwa uamuzi huo ni malumbano na majibizano ya maneno yaliyojiri kati ya Donald Trump na Kansela wa Ujerumani Friedrich Mertz.
Mertz alikosoa mkakati wa Marekani kuhusiana na Iran akisema, Washington "imedhalilishwa" na Tehran. Trump naye akajibu mapigo kwa kumuelezea Mertz kuwa ni mtu "asiye na uwezo wowote", na kisha akatoa amri ya kuondolewa askari wa Marekani walioko Ujerumani. Msemaji wa Pentagon amesisitiza kuwa, hatua hiyo "ni utekelezaji kamili wa amri za amiri jeshi mkuu wa vikosi vya ulinzi" vya Marekani. 

Wanadiplomasia wa Ulaya wanaielezea hali iliyopo kuwa ni "ya kutia wasiwasi na isiyotabirika." Kiasi kwamba, hata viongozi waliojaribu kujikomba na kujipendekeza kwa Trump nao pia hawajasalimika. Waziri Mkuu wa Italia Giorgi Meloni na Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte nao pia wametusiwa na Trump. Mwanadiplomasia mmoja wa Ulaya ameiambia Reuters: "Kila mtu anajua kwamba kujipendekeza hakusaidii kitu. Njia bora ni kuendelea kuwa ngangari kimsimamo na kuupa fursa muda upite.” 
Lakini mbali na upande wa kijeshi, uamuzi uliotangazwa na Pentagon una athari za kisiasa pia. Wataalamu wa Ulaya wanaamini kuwa, hatua hiyo ina matokeo hasi matatu ya msingi ya kijiopolitiki. Kwanza, ni kudhoofisha uwezo wa kuzuia hujuma dhidi ya Russia, hususan upande wa Ulaya Mashariki na katika nchi za Baltiki. Pili, ni kuteteresha imani iliyopo kwa Kifungu cha 5 cha NATO cha (msingi wa kujihami kwa pamoja). Na tatu, ni kuharakisha mchakato wa Ulaya kujitegemea kiulinzi. Mwanadiplomasia mmoja wa Magharibi amesisitiza kwa kusema: "Ulaya haiwezi tena kutegemea muundo wa baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Inapasa iwe eneo, si la nguvu laini tu, lakini pia lenye uwezo wa nguvu za kijeshi”.
Ujerumani nayo kwa upande wake haijajipweteka. Berlin imeidhinisha mpango wa kuongeza matumizi ya kiulinzi hadi kiwango cha asilimia 3.7 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2030. Uzalishaji wa ndani wa mitambo ya Patriot na makombora ya Stinger nao pia umeanza.  Imepangwa kuwa, viwanda vya kwanza vya uundaji silaha za kisiasa vitajengwa katika ardhi ya Ujerumani. Baadhi ya wakosoaji wa sera za Trump barani Ulaya wanaamini kuwa, Ikulu ya White House inaweza ikadhani kwamba kwa uamuzi huo wa kuwaondoa askari wa Marekani inaiadhibu Ujerumani iliyoasi. Lakini ukweli halisi ni kitu kingine kabisa.
Washington inautoa mhanga uwekezaji iliougharamia kwa miongo kadhaa kwa sababu ya uono finyu na hasira za muda mfupi tu. Kuondoka Ujerumani ni mwisho wa moja ya enzi. Na si kwa Ulaya, bali kwa Marekani yenyewe. Lakini suali linaloendelea kuulizwa ni: Vipi unatarajia kwamba utaweza kubaki kuwa dola kuu lenye nguvu bila kufikia kitovu cha Ulaya? Ukweli ni kuwa, uamuzi wa kupunguza askari wa Marekani nchini Ujerumani ni ishara ya kufifia na kuyoyoma zama za Marekani yenye sauti ya juu kabisa duniani; na katika upeo mpana zaidi, ni kumalizika kwa enzi ya Magharibi. Ulaya kwa ujumla haina mshikamano unaohitajika wa kutoa mchango wa pamoja katika mabadiliko yanayojiri duniani. Kupanuka ufa wa mpasuko uliopo kati ya Marekani na Ulaya kunaiandalia fursa kadhaa mihimili mingine ya madola yenye nguvu ulimwenguni.../