Uungaji Mkono wa Ulaya kwa Jinai za Israel Umekuwa na Matokeo Gani?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i138168-uungaji_mkono_wa_ulaya_kwa_jinai_za_israel_umekuwa_na_matokeo_gani
Francesca Albanese, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya haki za binadamu katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu ametoa indhari kali akisema, nchi za Ulaya zinazizoesha jamii zao sera za kikatili za Israel, yakiwa ni matokeo ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kijeshi na kibiashara na utawala huo wa kizayuni licha ya kuwa unakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kimbari katika mahakama za kimataifa.
(last modified 2026-05-04T12:50:52+00:00 )
May 04, 2026 12:37 UTC
  • Uungaji Mkono wa Ulaya kwa Jinai za Israel Umekuwa na Matokeo Gani?

Francesca Albanese, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya haki za binadamu katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu ametoa indhari kali akisema, nchi za Ulaya zinazizoesha jamii zao sera za kikatili za Israel, yakiwa ni matokeo ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kijeshi na kibiashara na utawala huo wa kizayuni licha ya kuwa unakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kimbari katika mahakama za kimataifa.

Francesca Albanese, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya haki za binadamu katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu ametoa indhari kali akisema, nchi za Ulaya zinazizoesha jamii zao sera za kikatili za Israel, yakiwa ni matokeo ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kijeshi na kibiashara na utawala huo wa kizayuni licha ya kuwa unakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kimbari katika mahakama za kimataifa; na wakati huohuo, nchi hizo za Ulaya zinawakandamiza waharakati wanaotetea na kuunga mkono Palestina barani humo. 
Albanese anaitakidi kuwa, mwenendo huo umedhoofisha sana hadhi ya kimataifa ya Ulaya. Ripota huyo Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na hali ya haki za binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ametoa indhari hiyo wakati alipohutubia maandamano ya kuunga mkono Muqawama wa Palestina katika mji mkuu wa Ugiriki, Athens; ambapo sambamba na kuashiria hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ amesisitiza kwamba, hakuna nchi yoyote mwanachama wa Umoja wa Mataifa yenye haki ya kuisaidia Israel hadi pale ukaliaji wa mabavu wa Palestina utakapokomeshwa kikamilifu na bila masharti yoyote na utawala huo.
Lakini licha ya sisitizo hilo, sio tu Ulaya haijakata misaada yake kwa Israel, lakini pia imeendelea kuupatia utawala huo wa kizayuni silaha, kununua kutoka kwake teknolojia ya ujasusi sambamba na kushadidisha ukandamizaji na hatua za kiusalama ndani ya jamii zake. 
Francesca Albanese amesema, matokeo ya sera hiyo yamekuwa ni kushuhudiwa wimbi kubwa la kamatakamata dhidi ya waandamanaji wapinzani, kukiukwa uhuru wa kutoa maoni na kugeuzwa wanaharakati wanaoiunga mkono Palestina kuwa raia wa daraja la pili kwenye kitovu cha bara hilo la Ulaya. 
Yanis Varoufakis, waziri wa zamani wa fedha wa Ugiriki, yeye alisema katika mkutano huo kwamba Ugiriki imeizoesha zaidi jamii yake sera za Israel kuliko nchi nyingine yoyote ya Ulaya. Varoufakis ameashiria jinsi Athens ilivyoshirikiana na Tel Aviv kuuzuia na kuukamata msafara wa meli wa kimataifa wa Sumud katika maji ya kimataifa, kitendo ambacho Albanese amekielezea kuwa "si sahihi" na ni ukiukaji wa sheria za safari za baharini. 
Uungaji mkono wa hali na mali wa serikali za Ulaya kwa utawala mtenda jinai wa Kizayuni unaoua na kumwaga damu za watoto wa Kipalestina kila uchao umeigharimu sana Ulaya.
Kwa miaka mingi, Umoja wa Ulaya umejionyesha kama mbeba bendera ya utetezi wa haki za binadamu, utawala wa sheria na utaratibu unaozingatia kanuni za kimataifa. Lakini muamala na utendaji wa kiundumakuwili wa umoja huo katika migogoro ya Ukraine na Ghaza na jinai zilizofanywa na Wazayuni za kuua watoto, wanawake na raia wa kawaida wa Iran vimeyadhihaki na kuyatoa maanani madai hayo ya Ulaya. 
Tovuti ya habari ya Middle East Eye imeeleza katika uchambuzi ulioandikwa na Carlo Cornelius, mwanadiplomasia wa zamani wa Italia kwamba, katika upande mmoja, baada ya kupita masaa 48 tu ya kuanza vita vya Ukraine, Umoja wa Ulaya uliweka vikwazo vikali zaidi katika historia yake dhidi ya Russia; lakini katika upande mwingine, umoja huo umekataa hata kusitisha tu mkataba wa ushirikiano wake na Israel kutokana na mauaji ya kimbari uliyofanya utawala huo wa kizayuni huko Ghaza.

Kaja Kallas, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, ameilaani Russia mara 11 katika vikao vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kutaka ianzishwe mahakama maalumu ya kushughulikia kesi za uhalifu wa ubakaji huko Ukraine, lakini hajawahi hata mara moja kulitaja jina la Israel au Marekani ambazo ni wavunjaji wakuu wa sheria za kimataifa. Kwa mtazamo wa wachunguzi wa mambo, kimya hicho chenye maana maalumu, hakitokani na kutokuwa na uelewa, bali ni “uhepaji wa kimfumo wa uchukuaji hatua ili kuwapa kinga wahalifu ya kutoweza kuadhibiwa”. Ujumbe wa mwenendo huo kwa walimwengu uko wazi kabisa, nao ni kwamba: baadhi ya ukiukaji wa sheria za kimataifa "hausamaheki," lakini baadhi yao huwa ni " wa kusikitisha" tu.
Vipimo hivi vya kiundumakuwili na kinafiki vimeigharimu sana Ulaya; kwanza ni kwamba, itibari na thamani ya kimaadili ya Umoja wa Ulaya, EU katika Ulimwengu wa Kiislamu na Kusini mwa Dunia imeshuka hadi kiwango cha sifuri. Chunguzi za maoni zilizofanywa kimataifa zinaonyesha kuwa umaarufu wa Ulaya katika nchi za Kiarabu na Asia umeshuka hadi kiwango cha chini zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia yake. 
Lakini pili, ushawishi wa kidiplomasia wa Umoja wa Ulaya katika eneo la Asia Magharibi umetoweka kikamilifu. Nchi za eneo hilo haziioni tena Brussels kama mpatanishi asiyependelea upande wowote, bali zinaichukulia kuwa ni mshirika wa kisiasa na kijeshi wa utawala bandia na wa kijinai wa Israel. 
Tatu ni kuwa, kudhoofika nafasi hiyo kumetoa fursa kwa madola makubwa mapya yanayoibukia kama vile China na Russia ya kujaza ombwe na nafasi tupu ya ushawishi iliyoachwa wazi na Ulaya.
Katika hotuba yake ya mjini Athens, Francesca Albanese ameashiria nukta nyingine ya kutafakarisha akisema: sambamba na kuzizoesha jamii za Ulaya sera za Israel, sasa hivi kuna namna fulani ya kuzizoesha pia hali ya Wapalestina. Kwa maana kwamba, kuna makundi mbalimbali ya raia wa Ulaya - hususan wanaharakati wanaoiunga mkono Palestina, jamii ya Waislamu walio wachache na watu wanaopaza sauti za upinzani - ambao wanakumbwa na hali ya unyongeshwaji ya kunyimwa haki zao, kuwekwa kizuizini kiholela na kukandamizwa kimfumo, sawa na wanavyotendewa Wapalestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Nchini Ujerumani, maandamano ya kuunga mkono Ghaza yamepigwa marufuku au yanakandamizwa vikali na polisi. Huko Ufaransa, wanachuo na wanaakademia wanafukuzwa katika vyuo vikuu au kufunguliwa mashtaka kwa kosa la kuonyesha mshikamano na Palestina. Nchini Uingereza pia, wanaharakati wa kisiasa wanatiwa nguvuni kwa madai eti ya "kushiriki katika ugaidi." 
Francesca Albanese, ameeleza masikitiko makubwa kwa hatua ya maafisa wa Ugiriki kushirikiana na Israel katika kuuzuia msafara wa misaada ya kibinadamu wa Sumud na akasema, muelekeo huo batili unafikisha ujumbe hatari kwa walimwengu wa kwamba: Ulaya, iliyo mtetezi wa haki za binadamu, sasa imegeuka kuwa mshirika wa mhalifu. 
Makala ya tovuti ya Middle East Eye inamalizia kwa kueleza kwamba, maadamu Brussels inalitumia suala la haki za binadamu kama wenzo tu, ndoto ya kiitwacho "Ulaya yenye nguvu za kijiopolitiki" itabaki kuwa kitu cha pembeni ya mabadiliko ya kimataifa, na kambi hiyo ya Ulaya itaendelea kuandika ukurasa mwingine wa kitabu chake cha kujifutia hadhi na itibari yake.../