BBC: Uingereza ni mwathirika mkubwa zaidi wa kiuchumi wa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran
-
Vita vya US na Israel dhidi ya Iran vilivyoathiri pakubwa uchumi wa Uingereza
Ripoti ya BBC inasema Uingereza inakabiliwa na pigo kubwa zaidi kwa ukuaji wa uchumi miononi mwa nchi za kundi la 20 (G20), kutokana na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran na kufungwa Mlango Bahari wa Hormuz.
Katika ripoti yake inayotegemea takwimu mpya za Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD), Shirika la Utangazaji la Serikali ya Uingereza, BBC limechambua athari mbaya za vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran kwa uchumi wa Uingereza, na kuielezea nchi hiyo kama mwathirika mkubwa zaidi wa kiuchumi miongoni mwa madola makubwa duniani.
Ripoti hiyo inasema, kushuka kwa kasi kiwango cha ukuaji wa uchumi, kurejea janga la mfumuko wa bei, mkwamo wa viwango vya riba, na migogoro ya kisiasa ya ndani ni miongoni mwa matokeo ya vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran. Ripoti ya BBC inasisitiza kuwa, kinyume na dhana za awali, Uingereza ni mwathiriwa zaidi kuliko chumi nyingine kutokana na athari za muda mrefu za vita dhidi ya Iran , na ikiwa misukosuko katika soko la nishati haitapungua hadi majira ya kiangazi, Uingereza itakabiliwa na mgogoro mkubwa na mpana zaidi katika sekta ya maisha ya watu.
Katika muktadha huo, Shirika la taarifa za Nishati na Hali ya Hewa la Uingereza limeonya katika ripoti kwamba bei za vyakula nchini humo zinaweza kupanda kwa hadi asilimai 50 kufikia mwezi Novemba ikilinganishwa na viwango vilivyokuwepo mwanzoni mwa mgogoro wa gharama za maisha miaka mitano iliyopita.