Licha ya ushahidi wa UN, serikali ya UK yakataa kutambua mauaji ya kimbari ya Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i140242-licha_ya_ushahidi_wa_un_serikali_ya_uk_yakataa_kutambua_mauaji_ya_kimbari_ya_ghaza
Serikali mpya ya Uingereza imekataa wito uliotolewa wabunge 80 na wenzao wa kuyatambua mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Israel katika Ukanda wa Ghaza, kuuwekea utawala huo wa kizayuni vikwazo kamili vya silaha na kuanzisha vikwazo kamili dhidi ya utawala huo ghasibu.
(last modified 2026-07-29T02:25:26+00:00 )
Jul 29, 2026 02:23 UTC
  • Ungereza yakataa kutambua mauaji ya kimbari Ghaza
    Ungereza yakataa kutambua mauaji ya kimbari Ghaza

Serikali mpya ya Uingereza imekataa wito uliotolewa wabunge 80 na wenzao wa kuyatambua mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Israel katika Ukanda wa Ghaza, kuuwekea utawala huo wa kizayuni vikwazo kamili vya silaha na kuanzisha vikwazo kamili dhidi ya utawala huo ghasibu.

Uamuzi huo umezidisha ukosoaji dhidi ya Waziri Mkuu mpya Andy Burnham na Waziri wake wa Mambo ya Nje Ed Miliband, ambao kauli zao za mwanzo walizotoa walipoingia madarakani ziliibua matarajio ya kuachana na sera za Waziri Mkuu wa zamani Keir Starmer, lakini hadi sasa hazijaleta mabadiliko ya maana.

Barua iliyoandikwa na vyama mbalimbali iliyoongozwa na Mbunge wa chama cha Leba Kim Johnson, wajumbe wa Bunge la Wananchi na Baraza la Malodi imemhimiza Burnham ayatambua matokeo ya uchunguzi wa Tume Huru ya Kimataifa ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa, ambayo ilifikia hitimisho kwamba Israel ilifanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Ghaza.

Wabunge hao wameitaka serikali ya London "ibadilishe kimsingi msimamo wake" kwa kuunga mkono haki za Wapalestina na kuchukua hatua za kuzuia ukiukwaji zaidi wa sheria za kimataifa unaofanywa na utawala wa kizayuni wa Israel.

Vilevile wamewahimiza mawaziri kutekeleza uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuhusu uvamizi haramu na ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na Israel, kuuwekea utawala huo vikwazo kamili, kuanzisha vikwazo kamili vya silaha na kupiga marufuku biashara ya bidhaa na huduma zinazohusiana na vitongoji haramu vya Israeli katika Eneo la Wapalestina Linalokaliwa kwa Mabavu.

Hata hivyo, Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo imekataa kuidhinisha matakwa yoyote kati ya hayo.

Mnamo Septemba 2025, Tume Huru ya Uchunguzi ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa ilifikia hitimisho katika uchunguzi wake kwamba Israel ilifanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Ghaza. Iligundua kuwa mamlaka za Israel zilihusika na vitendo vya aina vinne kati ya tano vya mauaji ya kimbari vilivyotambuliwa katika Mkataba wa Mauaji ya Kimbari wa 1948…/