Vyombo vya habari Ulaya vyafichua mpango wa kifisadi wa Rais wa FIFA na wandani wa Trump
Jarida la The Times limefichua kiasi kikubwa cha fedha ambazo rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), Gianni Infantino, angeweka mfukoni iwapo mpango wa kuuza Kombe la Dunia ungetekelezwa.
Rais wa FIFA, Gianni Infantino, awali alidai kwamba hafaidiki na mpango wa kuuza haki za kibiashara za Kombe la Dunia, lakini kwa mujibu wa ufichuzi wa jarida la Times la Uingereza, kama mpango huo ungetekelezwa, rais wa FIFA angepokea mshahara wa zaidi ya euro milioni 30 kila mwaka, na pia angepewa bonasi za kifedha.
Kufichuliwa takwimu hizi za donge kubwa la rais wa FIFA katika mpango wa kuuza Kombe la Dunia kwa kampuni inayohusishwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, kumetajwa na vyombo vya habari vya Ulaya kuwa ni matumizi mabaya ya madaraka kwa ajili ya kujipatia faida binafsi.
Rais wa FIFA alikuwa amepanga kuuza haki za kibiashara za Kombe la Dunia kwa kampuni ya kaka wa mkwe wa Trump kwa dola bilioni 20, lakini alikumbana na malalamiko na upinzani mkali kutoka mashirikisho ya soka ya UEFA, AFC na CONCACAF, na kulazimika kutupilia mbali mpango huo.
Pendekezo la Infantino la mpango huo wa kifisadi wa kujinufaisha kifedha na kisiasa limesababisha 70% ya wanachama wa FIFA kupingana naye vikali, na kuibua mapinduzi makubwa ndani ya shirikisho hilo la mpira wa miguu duniani (FIFA), wengi wakitaka alazimishwe kujiuzulu au atimuliwe.
Gazeti la Times linafichua kwamba Gianni Infantino angepokea zaidi ya euro milioni 30 kama mshahara pamoja na bonasi kama angetekeleza mpango wa FIFA Forward Enterprise, kiwango ambacho ni kikubwa zaidi kuliko mshahara wake wa kawaida kama rais wa FIFA.
Mshahara wa sasa wa rais wa FIFA unakadiriwa kuwa karibu euro milioni 3 kwa mwaka; kwa hivyo, mapato ambayo Infantino alitarajiwa kupata kutokana na mpango wa mauzo ya Kombe la Dunia yalikuwa mara 10 ya mapato yake ya sasa.