Hukumu ya kihistoria nchini Uingereza: Kupinga Uzayuni si chuki dhidi ya Wayahudi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i140432-hukumu_ya_kihistoria_nchini_uingereza_kupinga_uzayuni_si_chuki_dhidi_ya_wayahudi
Katika uamuzi wa kihistoria uliotolewa jana Agosti 4, 2026, Mahakama Kuu ya Rufaa ya Ajira ya Uingereza ilikataa rufaa iliyowasilishwa na Chuo Kikuu cha Bristol dhidi ya msomi David Miller, ikithibitisha mfano wa kisheria unaotambua imani za kupinga Uzayuni kuwa ni itikadi ya kifalsafa inayolindwa chini ya Kifungu cha 10 cha Sheria ya Usawa ya Uingereza ya 2010.
(last modified 2026-08-05T12:10:38+00:00 )
Aug 05, 2026 12:03 UTC
  • Mahakama Uingereza: Kupinga Uzayuni si chuki dhidi ya Wayahudi
    Mahakama Uingereza: Kupinga Uzayuni si chuki dhidi ya Wayahudi

Katika uamuzi wa kihistoria uliotolewa jana Agosti 4, 2026, Mahakama Kuu ya Rufaa ya Ajira ya Uingereza ilikataa rufaa iliyowasilishwa na Chuo Kikuu cha Bristol dhidi ya msomi David Miller, ikithibitisha mfano wa kisheria unaotambua imani za kupinga Uzayuni kuwa ni itikadi ya kifalsafa inayolindwa chini ya Kifungu cha 10 cha Sheria ya Usawa ya Uingereza ya 2010.

Uamuzi huo, uliotolewa chini ya uenyekiti wa jaji Lord Fairley, unawakilisha mabadiliko makubwa ya kisheria; kwani unaweka mipaka ya uhuru wa kujieleza na ukosoaji wa kitaaluma wa Uzayuni ndani ya taasisi, na unakataza kutambua misimamo inayopinga uzayuni au kutangaza mshikamano na Palestina kuwa ni sababu ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu au kufukuzwa kazi.

Uamuzi huo unaweka sheria za kiutaratibu zinazowazuia waajiri na taasisi mbalimbali nchini Uingereza kuwafukuza kazi au kuwaadhibu watu binafsi kiutawala kwa sababu tu ya kuwa na misimamo ya kupinga Uzayuni.

Mahakama hiyo imesisitiza katika hoja yake kwamba uchambuzi wa kifikra unaoelezea Uzayuni kuwa ni itikadi ya kibaguzi au ya kikoloni una kiwango cha kutosha cha mshikamano na uwazi unaoupa kinga ya kisheria kama imani ya kifalsafa katika jamii ya kidemokrasia.

Katika taarifa yake baada ya kutolewa hukumu hiyo, Dkt. David Miller, Profesa wa Sosholojia ya Siasa, amesema kwamba uamuzi huo unaweka mpaka kati ya ukosoaji wa kitaaluma na shutuma za kiutawala.

Ameongeza kuwa, "Chuo Kikuu cha Bristol kilikabiliwa na msururu wa malalamiko ambayo yalilenga utafiti wangu wa kisayansi na uchambuzi wa kijamii wa Uzayuni, na uamuzi wa mahakama umethibitisha kwamba mpango wa kupinga Uzayuni unawakilisha msimamo wa kifikra na kisiasa unaolindwa na sheria, na hauingiliani na dhana ya chuki dhidi ya Uyahudi."

Katika muktadha huo huo, Masoud Shadjara, mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu ya Kiislamu, amesema kwamba "uamuzi huu utawapa wataalamu na wafanyakazi wa taasisii mbalimbali imani kubwa zaidi kwamba imani zao dhidi ya Uzayuni zinalindwa kisheria."