Ripoti: Marekani inazishinikiza nchi za Afrika kujiondoa ICC au kukabiliwa na madhara
-
Serikali ya Marekani
Utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani unazishinikiza nchi za Afrika kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na kutishia kuzichukulia hatua, huku Washington ikiongeza kasi ya kampeni yake dhidi ya mahakama hiyo.
Ripoti iliyochapishwa na gazeti la Le Monde Jumanne wiki hii imefichua kuwa Marekani inatumia mbinu mbili kuzishinikiza nchi za Afrika kuondoka ICC, ikiwa ni pamoja na kupitia "taarifa potofu" na kueleza kuwa serikali lengwa zinaweza kukabiliwa na mashtaka.
Ripoti hiyo imevinukuu vyanzo mbalimbali na kusema kuwa, njia ya pili inahusisha kuzitishia nchi za Kiafrika kwamba mikataba ya usalama iliyosaini na Marekani pamoja na aina nyingine za ushirikiano itafutwa iwapo zitakataa kujiondoa katika Mahakama ya ICC.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Uganda ilipokea barua kutoka Marekani tarehe 24 Julai mwaka huu iliyotoa sharti la mwisho kwa Kampala ili kujiondoa katika mahakama ya ICC au kukabiliwa na "hatua hasi" hata hivyo Uganda hadi sasa haijatoa jibu kwa sharti hilo la Marekani.
Ripoti ya Le Monde pia imeeleza kuwa Washington iliwasiliana na Benin kama sehemu ya kampeni ya kuishiniza nchi hiyo, hata hivyo mamlaka husika ya nchi hiyo iliwasilisha azimio la kupinga sharti la Washington la kuitaka nchi hiyo ijiondoe ICC.
Jaji wa ICC kutoka Benin, Reine Alapini-Gansou alikuwa miongoni mwa majaji watatu waliofungua kesi mjini New York mwezi Juni kupinga vikwazo vya Marekani dhidi ya maafisa wa mahakama hiyo.
Gazeti la Le Monde limeripoti kuwa kampeni ya Marekani dhidi ya ICC imeshika kasi tangu mahakama hiyo ilipotoa hati za kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na aliyekuwa Waziri wa Vita wa utawala huo, Yoav Gallant, mnamo Novemba 21, 2024 kwa tuhuma za kutenda jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu wakati wa vita vya mauaji ya kimbari vilivyofanywa na Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.