Watetezi wa Palestina washinda katika uteuzi wa wagombea wa Democratic wa uchaguzi wa US
Matokeo ya uchaguzi wa mashinani wa Marekani wa kuteua wagombea wa Seneti na Baraza la Wawakilishi katika uchaguzi wa Novemba yanaonyesha ushawishi unaoongezeka wa mrengo wa chama cha Democratic unaotaka mabadiliko, ambao umeliweka suala la Palestina kwenye kitovu cha wito wake wa kisiasa.
Waungaji mkono wa harakati hiyo wanasema, zaidi ya wagombea 250 wa mrengo huo wa mabadiliko hivi sasa wanashikilia nafasi za kuchaguliwa kote nchini Marekani.
Aidha, wanasema wagombea 35 Wademocrat wa mrengo wa wapenda mabadiliko wamewashinda wagombea wa chama hicho wanaoungwa mkono na mrengo mkuu wa chama katika kuwania uteuzi wa kuwania ubunge, wakielezea matokeo hayo kama mabadiliko makubwa ndani ya chama cha Democratic.
Marekani kwa sasa inafanya chaguzi za mashinani kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa Novemba 2026, ambapo wapiga kura wa chama cha Democratic na Republican wanawachagua wagombea wa vyama vyao kwa ajili ya uchaguzi huo wa Bunge.
Miongoni mwa matokeo muhimu zaidi ya michuano ya awali ya wiki hii yalikuwa ni ushindi wa siku ya Jumanne aliopata Abdulrahman El-Sayed wa kunyakua nafasi ya uteuzi wa mgombea wa chama cha Democratic kwa ajili ya Seneti ya Marekani katika jimbo la Michigan, pamoja na ushindi wa wagombea kadhaa wanaounga mkono Palestina, wakiwemo Rashida Tlaib, Donovan McKinney, na William Lawrence.
Kufuatia ushindi aliopata El-Sayed Lobi ya kizayuni yenye ushawishi mkubwa ndani ya Marekani ya AIPAC, ambayo ilitumia karibu dola milioni 32 kumtangaza na kumpigia kampeni Haley Stevens, mgombea anayeuunga mkono utawala wa kizayuni wa Israel na kumshambulia El-Sayed, hivi sasa inapanga kutumia makumi ya mamilioni ya dola kumuunga mkono Mike Rogers mgombea wa Seneti kwa tiketi ya Republican baada ya kushindwa njama yake ya kumwangusha El-Sayed katika uchaguzi wa mchujo wa chama cha Democratic.
Jaribio la pili la AIPAC la kumshinda El-Sayed linaonekana kama hatua ya kutapatapa na kukata tamaa wakati upinzani dhidi ya utawala wa kizayuni wa Israel ukiwa unazidi kuongezeka miongoni mwa wapiga kura wa Marekani…/