Katika kumbukumbu ya mwaka wa 81 tangu US ilipoishambulia Hiroshima, UN yataka silaha za nyuklia ziangamizwe
https://parstoday.ir/sw/news/world-i140482-katika_kumbukumbu_ya_mwaka_wa_81_tangu_us_ilipoishambulia_hiroshima_un_yataka_silaha_za_nyuklia_ziangamizwe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameonya kuwa dunia inakabiliwa na ongezeko la hatari ya matumizi ya silaha za nyuklia kutokana na kushamiri migawanyiko ya kisiasa, kutokuaminiana na mashindano ya kijeshi.
(last modified 2026-09-15T11:41:35+00:00 )
Aug 07, 2026 12:25 UTC
  • Katika kumbukumbu ya mwaka wa 81 tangu US ilipoishambulia Hiroshima, UN yataka silaha za nyuklia ziangamizwe

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameonya kuwa dunia inakabiliwa na ongezeko la hatari ya matumizi ya silaha za nyuklia kutokana na kushamiri migawanyiko ya kisiasa, kutokuaminiana na mashindano ya kijeshi.

Guterres ameeleza hayo katika ujumbe aliotoa kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mwaka wa 81 tangu Marekani ilipoishambulia kwa mabomu ya atomiki miji ya Japan ya Hiroshima na Nagasaki na kuangamiza roho za maelfu ya watu.

“Wakati umefika kwa mataifa kuchagua njia ya mazungumzo, ushirikiano na upokonyaji wa silaha badala ya kutegemea nguvu za kijeshi ili kutatua mizozo,” ameeleza Katibu Mkuu wa UN katika ujumbe wake huo.

Guterres amesema, miaka 81 iliyopita, Hiroshima iligeuzwa kuwa kifusi, maelfu ya watu wakapoteza maisha na dunia ikashuhudia kwa mara ya kwanza madhara mabaya ya vita vya nyuklia.

Amesema, wakati leo tunawakumbuka waliopoteza maisha na kuwaenzi manusura wa shambulizi hilo, wanaojulikana kama hibakusha, ambao idadi yao inaendelea kupungua, ujumbe wao wa amani unaendelea kuwa muhimu kwa dunia.

"Kumbukizi hii si siku ya kumbukumbu pekee, bali pia ni wakati wa kujiuliza kama tumejifunza kwa dhati kilichotokana na maafa ya Hiroshima, na kama ubinadamu utachagua mustakabali wa amani au utaendelea kuishi chini ya kivuli cha maangamizi ya nyuklia," ameeleza Guterres.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, somo la Hiroshima halihusu madhara tu ya silaha za nyuklia, bali pia umuhimu wa kujenga dunia ambayo matumizi au hata tishio la kutumia silaha hizo litakuwa jambo lisilokubalika.

Amesema: "amani hujengwa kwa kuaminiana, mazungumzo ya kudumu, diplomasia, ushirikiano wa kimataifa na kuheshimu sheria za kimataifa."

Aidha, amezitaka nchi zote, hususan zile zenye silaha za nyuklia, kuchukua hatua za kupunguza hatari, kurejesha imani na kuharakisha juhudi za kuondoa kabisa silaha hizo…/