Ripoti: Trump alibadilisha ndege kwa siri nchini Uturuki kutokana na 'tishio la Iran'
-
Trump alibadili ndege akihofia tishio la Iran
Vyanzo vya habari vya nchini Marekani vimeripoti kuwa Rais Donald Trump wa nchi hiyo mwezi uliopita alibadilisha kwa siri ndege ya Air Force One na kutumia ndege ndogo ya kijeshi ya Marekani baada ya kuondoka kwenye mkutano wa kilele wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) mjini Ankara, Uturuki, katika operesheni iliyoripotiwa kuchochewa na "tishio la Iran,".
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa jana Jumatatu na gazeti la The Washington Post, awali Trump alipanda ndege ya Air Force One ya modeli ya zamani mjini Ankara, Uturuki mbele ya kamera za televisheni, huku waandishi wa habari na baadhi ya wafanyakazi wa Ikulu ya White Houuse wakiamini kuwa angesafiri kwa ndege hiyo hadi kwenye kituo cha Royal Air Force Mildenhall nchini Uingereza.
Gazeti la The Washington Post limebainisha haya kwa mujibu wa afisa wa Marekani anayefahamu operesheni hiyo, na mtu mwingine mwenye taarifa kuhusu safari za Trump.
Hata hivyo, dakika chache baada ya kupanda ndege ya Air Force One, Trump na wasaidizi wake kadhaa walihamishiwa kwenye ndege ndogo zaidi aina ya Air Force C-32A wakitumia gari la kubebea chakula na mahitaji mengine ya ndege," imeongeza taarifa ya The Washington Post.
Waandishi wa habari, ambao waliamini kuwa wanasafiri pamoja na Trump waliagizwa kushusha vifuniko vya madirisha yao kabla ya ndege kupaa. Kisha Trump akasafiri hadi Mildenhall kwa kutumia ndege aina ya C-32A.
Operesheni hiyo ilifanyika wakati vikosi vya majeshi ya Marekani vilipokuwa vikifanya mashambulizi makubwa ya kichokozi dhidi ya Iran.