Mwanadiplomasia wa kizayuni: Baadhi ya Wademocrat wanaipendelea Iran kuliko serikali ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i140604-mwanadiplomasia_wa_kizayuni_baadhi_ya_wademocrat_wanaipendelea_iran_kuliko_serikali_ya_marekani
Mwanadiplomasia mmoja mwandamizi wa utawala wa kizayuni wa Israel amesema, ametiwa wasiwasi mkubwa na alichokiita "mabadiliko ya mwelekeo" katika sera ya Marekani, akisisitiza kwamba Tel Aviv inajiandaa kwa zama za kupunguza utegemezi kwa Washington na kujitegemea zaidi, ikiwa ni pamoja na "kuanzisha muungano na nchi zingine."
(last modified 2026-08-12T03:38:32+00:00 )
Aug 12, 2026 03:36 UTC
  • Ofir Akunis
    Ofir Akunis

Mwanadiplomasia mmoja mwandamizi wa utawala wa kizayuni wa Israel amesema, ametiwa wasiwasi mkubwa na alichokiita "mabadiliko ya mwelekeo" katika sera ya Marekani, akisisitiza kwamba Tel Aviv inajiandaa kwa zama za kupunguza utegemezi kwa Washington na kujitegemea zaidi, ikiwa ni pamoja na "kuanzisha muungano na nchi zingine."

Ofir Akunis, balozi mdogo wa Israel huko New York, amesema katika mahojiano na tovuti ya habari ya Newsweek kwamba kinachomtia wasiwasi zaidi ni "mabadiliko ya mwelekeo katika sera ya Marekani," ambayo anaamini kuna siku yanaweza kusababisha kuvunjika kwa muungano wao wa kihistoria.

Akunis amezungumzia ushindi wa hivi karibuni wa uchaguzi waliopata wagombea wapenda mabadiliko wa Chama cha Democrat ambao ni maarufu kwa kuukosoa utawala wa Kizayuni na uingiliaji wa Marekani nje ya nchi, na kudai kwamba "ukweli ni kuwa, baadhi ya watu hapa, bila shaka wanaipendelea Iran kuliko serikali ya Marekani".

Mwanadiplomasia huyo kizayuni amedai kwa kusema: "unaweza kumchukia rais wako, unaweza usimpende, unaweza usimjali, au unaweza ukataka kubadilisha serikali; yote haya ni sehemu ya mchezo wa kidemokrasia. Lakini kuwapendelea maadui zako kuliko wapinzani wako wa kisiasa, hili ni jambo jipya."

Huku akisema: “natumai Marekani itabaki kuwa nasi daima,” Akunis amebainisha kwamba, kwa namna anavyouona mwenendo wa sasa unavyokwenda, “watahitaji kujiandaa kujitegemea zaidi kuliko walivyozoea.”

Aidha, amesema kuimarisha hisia ya kuwa huru na kujitegemea hakumaanishi ubinafsi, na akaongeza kuwa: “mbali na muungano wetu na Marekani, tutaendelea kujenga miungano na nchi zingine.”

Kwa mujibu wa Newsweek, balozi huyo mdogo wa Israel nchini Marekani amaeashiria kuimarisha uhusiano na nchi kama India, Ugiriki, na Cyprus ikiwa ni sehemu ya “miungano yenye ncha sita” ambayo waziri mkuu wa utawala huo wa kizayuni Benjamin Netanyahu alishawahi kuizungumzia hapo kabla…/