Wanajeshi wa Marekani wauana ndani ya manuari ya kivita ya USS Abraham Lincoln
https://parstoday.ir/sw/news/world-i140606-wanajeshi_wa_marekani_wauana_ndani_ya_manuari_ya_kivita_ya_uss_abraham_lincoln
Wanajeshi saba wa Jeshi la Wanamaji la Marekani wameripotiwa kuuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mapigano makali ndani ya meli ya USS Abraham Lincoln, huku machafuko yanayoongezeka miongoni mwa wafanyakazi wa meli hiyo yakiweka wazi mashinikizo makubwa ndani ya jeshi la Marekani kutokana na majukumu ya muda mrefu ya kivita.
(last modified 2026-08-17T09:53:57+00:00 )
Aug 12, 2026 03:38 UTC
  • Wanajeshi wa Marekani wauana ndani ya manuari ya kivita ya USS Abraham Lincoln

Wanajeshi saba wa Jeshi la Wanamaji la Marekani wameripotiwa kuuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mapigano makali ndani ya meli ya USS Abraham Lincoln, huku machafuko yanayoongezeka miongoni mwa wafanyakazi wa meli hiyo yakiweka wazi mashinikizo makubwa ndani ya jeshi la Marekani kutokana na majukumu ya muda mrefu ya kivita.

Shirika la habari la Tasnim, likinukuu chanzo cha kijeshi chenye taarifa kamili limeripoti kuwa, tukio hilo lilitokea baada ya mshauri wa Kamandi Kuu ya Majeshi ya Marekani (CENTCOM), Brad Cooper kupanda meli hiyo ili kushughulikia malalamiko yanayoongezeka kutoka kwa maafisa wa kijeshi kufuatia upinzani wa familia zao kuhusu kuendelea majukumu ya wanajeshi walioko kwenye meli hiyo kwa muda mrefu.

Inasemekana mshauri huyo alikumbana na matusi na kurushiwa chupa za maji alipokuwa akihutubia mkutano wa wanajeshi walioko ndani ya manuari USS Abraham Lincoln.

Malumbano hayo baadaye yaligeuka na kuwa mapigano kati ya wanajeshi wa Marekani yaliyohusisha visu na silaha zingine kali, na kusababisha vifo vya maafisa saba na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Shirika la habari la Tasnim limeripoti kuwa hali ya mambo ndani ya meli hiyo ya kubeba ndege bado ni ya wasiwasi na mvutano.

Manuari ya kijeshi ya Abraham Lincoln imekuwa katika majukumu ya kijeshi kwa siku 263 na kwa sasa inafanya kazi katika Bahari ya Hindi, ambapo dhamira yake kuu ni kutekeleza mzingiro haramu wa majini dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

USS Abraham Lincoln

Machafuko hayo yameripotiwa huku kukiwa na wasiwasi unaoongezeka kuhusu hali ya maisha na mazingira ya kazi ya mabaharia na wanajeshi wa majini wapatao 5,000 wa Marekani walioko ndani ya meli hiyo.

Inaripotiwa kwamba wanajeshi walioko ndani ya meli hiyo wanalalamikia uhaba wa chakula, huku milo yao ikipunguzwa hadi nusu kikombe cha wali na vipande viwili vya nyama. Vitengo vya kufulia nguo vya manuari hiyo pia vimeharibika kwa wiki mbili, na ukungu katika maeneo ya kuogea umesababisha maambukizi ya fangasi miongoni mwa wanajeshi hao.

Familia za wanajeshi walioko ndani ya manuari ya Abraham Lincoln zimeelezea wasiwasi wao kuhusu uchovu, afya ya akili na athari mbaya za mwendo mrefu wa operesheni za muda mrefu za kijeshii kwenye uwezo wa wanajeshi hao wa kutekeleza majukumu yao kwa amani.

Vifo vilivyoripotiwa ndani ya meli ya Abraham Lincoln vinafuatia tukio lingine kubwa lililohusisha meli ya USS Gerald R. Ford. Mnamo Machi 12, 2026, moto ulizuka katika makazi ya wanajeshi wapatao 600 na kujeruhi 200 miongoni mwao.

Meli ya Gerald R. Ford baadaye iliwapeleka wanajeshi waliojeruhiwa kwenye kituo cha jeshi la majini la Marekani kwenye kisiwa cha Krete nchini Ugiriki kabla ya kulazimishwa kurudi Marekani.