Muislamu aliyeshinda kuwania Useneta Michigan atumiwa jumbe za chuki 3,000 kwa siku
Uchunguzi mpya uliofanywa na Kituo cha Utafiti wa Chuki Zilizoratibiwa (CSOH) cha nchini Marekani unaonyesha kuwa jumbe za maandishi zilizomlenga Abdulraham El-Sayed, za hisia za chuki dhidi yake kwa sababu ya Uislamu wake zilifikia wastani wa 3,099 kwa siku katika muda wa wiki moja baada ya ushindi wake, ikilinganishwa na wastani wa watu 155 kila siku katika miezi miwili kabla yake; hilo likiwa ni ongezeko la asilimia 1,895.
Ndani ya saa chache baada ya El-Sayed kuibuka mshindi katika uchaguzi wa mashinani wa kuteua mgombea wa kiti cha Useneti cha jimbo la Michigan kwa tiketi ya chama cha Democratic, idadi ya jumbe zilizotokana na chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) dhidi yake ziliongezeka kwa kiwango cha kutisha.
Mnamo Agosti 5, siku ambayo mpinzani wake alikubali rasmi kushindwa, idadi ya jumbe za chuki dhidi ya Waislamu zilizomhusu El-Sayed ilifikia kilele cha karibu 7,000 kwa siku moja.
Na katika muda wa wiki moja zilitumwa mitandaoni jumbe za chuki dhidi ya Uislamu kumhusu mgombea huyo wa Baraza la Seneti la Marekani, ambazo ni nyingi zaidi kuliko zilizotumwa miezi saba iliyopita kwa pamoja.
El-Sayed, afisa wa zamani wa afya ya umma wa Michigan anayegombea kiti cha Seneti cha Marekani kilichoachwa wazi na Gary Peters, ni Muislamu; na hilo limekuwa chanzo kikuu cha unyanyasaji unaofanywa dhidi yake.
Uchambuzi wa CSOH, ambao umetokana na jumbe na maandiko yanayotumwa kwenye mitandao ya X, Facebook, Instagram, YouTube, Reddit na Bluesky, umegundua kuwa sehemu kubwa ya tuhuma anazoelekezewa El-Sayed ni za kumhusisha na harakati za Hamas ya Palestina, Hizbullah ya Lebanon na Ikhwanul Muslimin ya Misri huku maandiko mengine mengi pia yakimtambulisha yeye kama 'mwanajihadi'.
Wengine wamemtuhumu bila msingi kwamba anapanga kulazimisha utekelezaji wa Sharia za Kiislamu, huku sehemu nyingine kubwa ya jumbe zikienda mbali zaidi kwa kusema suluhisho pekee ni kwa wahamiaji Waislamu walioko Magharibi kuhama huko na kurudi walikotoka.
CSOH imesema inatarajia kwamba, kampeni za ubaguzi dhidi ya Waislamu nchini Marekani zitazidi kuongezeka sambamba na kupamba moto kampeni za uchaguzi wa katikati ya muhula wa 2026 nchini humo…/