ILO: Mafunzo ya ufundi yatumike kukabiliana na ongezeko la ukosefu wa ajira kwa vijana
https://parstoday.ir/sw/news/world-i140644-ilo_mafunzo_ya_ufundi_yatumike_kukabiliana_na_ongezeko_la_ukosefu_wa_ajira_kwa_vijana
Ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana duniani umeongezeka, huku ukuaji dhaifu wa uchumi na upungufu wa nafasi mpya za kazi ukiwaweka vijana katika mazingira magumu ya kuingia katika soko la ajira.
(last modified 2026-08-13T14:27:22+00:00 )
Aug 13, 2026 10:34 UTC
  • Kiwanda cha pikipiki
    Kiwanda cha pikipiki

Ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana duniani umeongezeka, huku ukuaji dhaifu wa uchumi na upungufu wa nafasi mpya za kazi ukiwaweka vijana katika mazingira magumu ya kuingia katika soko la ajira.

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi Duniani (ILO), iliyopatiwa jina Mwelekeo wa Ajira kwa vijana 2026: Kujerejea kwenye Mustakabali,  kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana kilifikia asilimia 12.4 mwaka 2025, sawa na vijana milioni 67 wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 24.

Ripoti hiyo ambayo imetolewa Geneva Uswisi pia inaonesha kuwa asilimia 20 ya vijana, ambao ni zaidi ya milioni 257, hawakuwa katika ajira, elimu au mafunzo mwaka 2025.

Katika nchi zinazoendelea, changamoto kubwa ni kupata ajira za kutosha na zenye staha kwa idadi inayoongezeka ya vijana. Takriban vijana tisa kati ya 10 wenye umri wa miaka 15 hadi 29 katika nchi zenye kipato cha chini na cha chini-kati wanafanya kazi katika sekta isiyo rasmi.

ILO inaonya kuwa hali hiyo inawaweka vijana katika hatari ya kipato kisicho na uhakika na ukosefu wa ulinzi wa kijamii.

Ripoti pia inaonesha kuwa maendeleo ya kiteknolojia, ikiwemo akili mnemba, yanabadilisha aina ya ajira zinazopatikana kwa vijana. 

Takriban asilimia 6.1 ya ajira zinazofanywa na vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 29 ziko katika sekta zilizo katika hatari kubwa ya kuathiriwa na mabadiliko yanayohusiana na akili bandia.

ILO inataka kuongezwa kwa uwekezaji katika elimu bora, mafunzo ya ufundi, kuendelea kujifunza katika kipindi chote cha maisha na ulinzi wa kijamii ili kuwawezesha vijana kukabiliana na mabadiliko ya soko la ajira.

ILO inasisitiza kuwa nchi zinapaswa kuunda ajira zaidi zenye usalama, heshima na fursa za maendeleo kwa vijana.

Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Gilbert F. Houngbo, amesema “kizazi kisichoweza kupata ajira zenye staha hakiwezi kujenga mustakabali wake kwa kujiamini.”

 Ameongeza kuwa kuwawezesha vijana kupata ajira bora ni uwekezaji muhimu kwa uchumi na mshikamano wa kijamii.