Ripoti: Nchi 125 zawajibika kisheria kumkamata Netanyahu huku hati ya ICC ikimnyemelea Waziri Mkuu huyo wa Israel
-
Mtendai jinai za kivita, Netanyahu, anasakwa na ICC
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anakabiliwa na vizuizi vikali kimataifa vya kusafiri huku nchi 125 duniani zikiwajibika kisheria kwa kuwa wanachama katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kumtia mbaroni mtenda jinai huyo iwapo awasili katika nchi hizo.
Netanyahu "hawezi kuzitembelea katika nchi 125 leo hii yakiwemo madola makuu ya Magharibi ambazo ni miongoni mwa washirika wa karibu zaidi na wa kibiashara wa Israel," imeeleza ripoti iliyoandikwa na gazeti la Times of Israel linalochapishwa kwa lugha ya Kiebrania.
Gazeti hilo la Israel limeeleza kuwa nchi hizo ni pamoja na Ufaransa, Uingereza, Ujerumani na Kanada.
Vizuizi hivi tajwa vinavyomkabili Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel vimetokana na hati ya kukamatwa iliyotolewa na mahakama ya ICC Novemba 2024 dhidi ya Netanyahu kuhusiana na jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu zilizofanywa wakati wa kampeni ya mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Gaza, ambayo imesababisha vifo vya Wapalestina wasiopungua 73,000 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 17,000 tangu ilipoanza Oktoba 2023.
Mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague Uholanzi inamtia hatiani Netanyahu kwa uhalifu wa kivita wa kutumia njaa kama mbinu ya kivita, pamoja na jinai dhidi ya binadamu unaojumuisha mauaji, mateso na vitendo vingine vya kikatili dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza.
Athari za kivitendo tayari zimeonekana katika safari za nje za Netanyahu, huku ndege yake ikitumia njia mbadala ili kuepuka anga za nchi wanachama wa mahakama ya ICC.
Ripoti ya gazeti la Times of Israel imeongeza kuwa Netanyahu ameepuka kushiriki katika matukio katika nchi ambazo kibali hicho kinaweza kutekelezwa, ikiwa ni pamoja na Jukwaa la Uchumi Duniani huko Davos, Uswisi, kwa sababu Uswisi ni nchi mwanachama wa ICC.