Waziri wa Jeshi la Marekani ajiuzulu huku Hegseth akiendeleza fagio la chuma katikati ya vita
-
Daniel Driscoll
Jeshi la Marekani linakabiliwa na mgogoro mkubwa wa uongozi hasa baada ya Waziri wa Jeshi, Dan Driscoll, kuwasilisha barua ya kujiuzulu, huku Waziri wa Vita wa nchi hiyo, Pete Hegseth akiendelea na harakati za ndani za kuwafutilia mbali wapinzani wake.
Kunga'tuka huko kwa kiongozi wa ngazi za juu katika jeshi la USA kunakuja wakati Marekani inapoingia mwezi wa saba wa vita vyake vyenye gharama kubwa dhidi ya Iran, na kuliacha jeshi bila uongozi wa kudumu wa kiraia au kijeshi katika kipindi hiki muhimu.
Ikulu ya White House ilithibitisha kujiuzulu kwa Driscoll siku ya Jumatatu.Ingawa utawala wa Donald Trump umejaribu kuonyesha taswira ya nguvu, lakini nyuma ya pazia, kujiuzulu Waziri wa Jeshi wa Marekani ni kilele cha miezi kadhaa ya mvutano mkali kati ya Driscoll na Hegseth.Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la habari la Reuters likinukuu vyanzo vinavyofahamu jambo hilo, Driscoll alizidi kukatishwa tamaa na ukwamishaji wa Hegseth wa juhudi za mabadiliko na utayarifu wa jeshi, haswa tabia ya Waziri huyo wa Vita wa Marekani ya kuwafukuza kazi majenerali waliohusika na kutekeleza mikakati ya kulisasisha jeshi.
Ombwe la uongozi ndani ya jeshi la Marekani ni kubwa hasa kutokana na mashambulizi ya kijeshi yanayoendelea kufanywa na nchi hiyo huko Asia Magharibi.
Sambamba na makumi ya maelfu ya wanajeshi wa Marekani waliotumwa katika vita vya miezi saba dhidi ya Iran ambavyo havijakuwa na ushindi wowote na kupungua kwa kiasi kikubwa akiba ya silaha za Marekani, jeshi sasa linafanya kazi bila waziri wa kudumu wa kiraia au kiongozi mkuu wa kijeshi.Mwezi Aprili mwaka huu Hegseth alimfukuza kazi ghafla Mkuu wa Majeshi ya Marekani, Jenerali Randy George na ameshindwa kumteua mrithi wa kudumu.
Inasemekana Driscoll aliitambua hatua hiyo kuwa ni sawa na kukata kichwa cha jeshi wakati vita kali ikiendelea, hali iliyozidi kuwa mbaya wakati Hegseth alipompiga kalamu nyekundu mkuu wa majeshi ya Marekani barani Ulaya na kuzuia kupandishwa vyeo maafisa wengine wakuu.
Ripoti zinasema, Hegseth alikuwa akimuona Driscoll kama tishio na kwa muda mrefu na alikuwa akitafuta njia ya kuondolewa kwake jeshini.
Wachunguzi wa masuala ya kijeshi na wakosoaji wa ndani wanasema kwamba Pentagon inamomonyoka kutokea ndani kutokana na watu wenye itikadi za kisiasa.