Pezeshkian: Marekani ilikiuka MoU ya Islamabad, ikahamia kwenye madai ya kuchupa mipaka ndani ya wiki mbili
https://parstoday.ir/sw/news/world-i141130-pezeshkian_marekani_ilikiuka_mou_ya_islamabad_ikahamia_kwenye_madai_ya_kuchupa_mipaka_ndani_ya_wiki_mbili
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kwamba usalama endelevu haupatikani kupitia makabiliano, bali kupitia njia ya kuaminiana, kuheshimu mamlaka ya kujitawala ya nchi nyingine, kutoingilia mambo yao ya ndani, na ushirikiano kati ya serikali, na ametoa wito wa kuimarishwa ushirikiano wa kiusalama na kiuchumi katika Shirika la Ushirikiano la Shanghai.
(last modified 2026-09-01T14:57:24+00:00 )
Sep 01, 2026 14:56 UTC
  • Rais Masoud Pezeshkian akihutubia mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai (SCO)
    Rais Masoud Pezeshkian akihutubia mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai (SCO)

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kwamba usalama endelevu haupatikani kupitia makabiliano, bali kupitia njia ya kuaminiana, kuheshimu mamlaka ya kujitawala ya nchi nyingine, kutoingilia mambo yao ya ndani, na ushirikiano kati ya serikali, na ametoa wito wa kuimarishwa ushirikiano wa kiusalama na kiuchumi katika Shirika la Ushirikiano la Shanghai.

Akihutubia mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai (SCO), mapema leo Jumanne, Rais Masoud Pezeshkian amezungumzia changamoto muhimu zaidi za kiusalama na kiuchumi katika eneo hilo na kusisitiza haja ya kuimarisha ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama ili kuimarisha amani na kupanga mustakabali wa pamoja.
Akizungumzia vitisho kama vile ugaidi, Rais Pezeshkian ametaja misimamo mikali ya kikatili, biashara haramu ya dawa za kulevya, uhalifu uliopangwa wa kimataifa na uhalifu wa mtandaoni, kuongeza ushindani wa kijiopoliti, sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja, na matumizi ya nguvu za kijeshi kuwa ni mambo mengine yanayozitia wasiwasi nchi za eneo hilo na uchumi unaoibuka.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amezungumzia matukio ya hivi karibuni katika eneo la Asia Magharibi na mashambulizi ya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, akielezea vitendo hivyo kiwa ni uchokozi dhidi ya kanuni za msingi za Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa. Huku akielezea mwenendo wa vita na matukio yaliyofuata, amesisitiza msimamo wa Iran wa kuheshimu Mkataba wa Maelewano wa Islamabad.Dokta Pezeshkian amebainisha kuwa Marekani "iliheshimu majukumu yake kwenye hati yenye sahihi ya rais wake kwa chini ya wiki mbili kabla ya kuanza kutoa madai ya kupindukia na kukiuka majukumu yake, jambo ambalo linaendelea hadi leo."
"Ukiukaji wa majukumu wa Marekani ulikabiliwa na jibu linalofaa kutoka Iran," Pezeshkian amesema.Ameongeza kwa kusema: Tofauti na Marekani, nchi yangu ina rekodi nzuri ya kuheshimu majukumu na makubaliano yake ya kimataifa na imekuwa ikitenda kwa mujibu wa kanuni na sheria za kimataifa.”
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Rais Pezeshkian ameutaja usalama na maendeleo kuwa dhana mbili zinazohusiana na zisizotenganishwa na kusisitiza udharura wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai kuimarisha mshikamano, ufanisi, na muunganiko wa shirika hilo.