Namna Ulaya Ilivyojiweka Mbali na Uhuru Wake wa Kimkakati
https://parstoday.ir/sw/news/world-i141146-namna_ulaya_ilivyojiweka_mbali_na_uhuru_wake_wa_kimkakati
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kwamba, Ulaya lazima ichague kama itakuwa mhusika huru au itaendelea kufuata kibubusa siasa na sera za watu wengine. Kauli hii ya Esmaeil Baghaei, inafafanua msimamo wa hivi karibuni wa Umoja wa Ulaya katika kuunga mkono mashinikizo ya kiuchumi ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2026-09-02T10:19:34+00:00 )
Sep 02, 2026 10:09 UTC
  • Namna Ulaya Ilivyojiweka Mbali na Uhuru Wake wa Kimkakati

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kwamba, Ulaya lazima ichague kama itakuwa mhusika huru au itaendelea kufuata kibubusa siasa na sera za watu wengine. Kauli hii ya Esmaeil Baghaei, inafafanua msimamo wa hivi karibuni wa Umoja wa Ulaya katika kuunga mkono mashinikizo ya kiuchumi ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Suala hili linatokana na utata na mgangonao wa wazi kwa upande wa Ulaya kuhusu masuala yanayohusiana na Tehran. Umoja wa Ulaya unaunga mkono vikwazo ambavyo havina msingi wowote wa kisheria na utekelezaji wake unapingana moja kwa moja na kanuni na misimamo rasmi ya Ulaya. Baghaei amesema: "Kwa kuzingatia kanuni zake wenyewe, Umoja wa Ulaya hautambui utekelezaji wa sheria za nchi nyingine nje ya mipaka ya nchi wanachama, na unaona kuwa kutekelezwa sheria kama hizo ni kinyume na sheria za kimataifa." Hivyo, anaibua swali muhimu la kisheria na kisiasa: "Ikiwa hali ni hiyo, ni kwa msingi gani Umoja wa Ulaya sasa unaunga mkono vikwazo haramu na vya ukandamizaji mkubwa dhidi ya Iran?"

Jibu la swali hili linapaswa kutafutwa katika mabadiliko ya msimamo wa Ulaya katika miaka ya karibuni. Mnamo mwaka 1996, wakati vikwazo vya Marekani vilipotishia mamlaka na maslahi ya Umoja wa Ulaya, umoja huo ulipitisha sheria ya kuzuia hatua hiyo ya upande mmoja ya Marekani ya kutaka kulazimisha sheria zake za ndani dhidi ya mataifa mengine. Huko nyuma, Ulaya ilifafanua uhuru na kujitawala kwake si kwa maneno matupu tu, bali kupitia upinzani wa kivitendo dhidi ya Washington. Hata hivyo, leo, wakati mantiki hiyo hiyo ya vikwazo inapotumika dhidi ya Iran, Ulaya si tu inafumbia macho kanuni na sheria hiyo iliyoitunga yenyewe, bali hata inashirikiana na upande unaotekeleza vikwazo hivyo visivyo vya kisheria dhidi ya taifa jingine huru.

Ikiwa Ulaya itadai kuwa msimamo huo unaihusu Marekani tu, basi fikra nzima ya "uhuru wa kimkakati" inakuwa haina maana ya kweli na inabaki kuwa ya kimaonyesho tu. Kwa sababu hiyo, Baghaei anasisitiza kuwa, "Ulaya haiwezi tena kuzungumzia suala la 'uhuru wa kimkakati' huku ikiruhusu kutumika kama mtekelezaji tu wa maagizo ya Washington." Pia anafafanua kigezo cha uhuru huo kwa kusema: "Uhuru wa kimkakati haupatikani kwa matamshi makubwa na ya kuvutia tu, bali unapatikana kwa kuonyesha nia na uwezo wa kufanya maamuzi huru na ya kuwajibika, hata pale maamuzi hayo yanapokinzana na msimamo wa nguvu kubwa zaidi duniani." Uungaji mkono wa Ulaya kwa mashinikizo ya kiuchumi ya Marekani dhidi ya Iran umekuwa kipimo halisi cha madai haya, na matokeo yake yanaonyesha kuwa tatizo kuu la Ulaya si kutokuwa na uwezo, bali ni kutokuwa na utashi wa kufanya maamuzi huru. Umoja wa Ulaya una rasilimali muhimu za kiuchumi, kisiasa na kisheria za kuchukua msimamo huru, lakini kwa bahati mbaya umeamua kuungana na Washington katika kutekeleza sera hiyo isiyo ya haki ya Marekani dhidi ya Iran, hata pale hatua hiyo inapokinzana wazi na kanuni za kisheria na maslahi ya kimkakati ya Ulaya yenyewe. Hapa ndipo utata wa msimamo wa Ulaya unapodhihiri wazi. Umoja huohuo unaounga mkono mashinikizo ya kiuchumi dhidi ya Iran, hauna hata haya unaposimama na kudai hadharani kuwa ni mtetezi wa kupunguza mivutano na kudumisha utulivu katika Mashariki ya Kati. Sera hizi mbili kinzani haziwezi kuoanishwa kabisa. Huwezi kuunga mkono matumizi ya mashinikizo ya kiuchumi kama wenzo dhidi ya upande wa pili na wakati huo huo kudai kuwa unatafuta njia za kudhibiti mzozo. Kuhusiana na hili, Baghaei amesema: "Umoja wa Ulaya hauwezi kuunga mkono ugaidi wa kiuchumi wa Washington dhidi ya Iran huku ukidai kujitahidi kupunguza mvutano na kuleta utulivu katika eneo. Misimamo hii miwili haiendani kabisa."

Matokeo ya msimamo huu usio wa kimantiki yamerejea na kuidhuru Ulaya yenyewe. Migogoro ya kikanda, ukosefu wa usalama baharini na mashinikizo kwenye masoko ya nishati vimeathiri pia uchumi wa Ulaya. Ulaya inabeba gharama za kiuchumi na kiusalama zinazotokana na ukosefu wa utulivu, lakini inaendelea kuunga mkono sera ambayo, badala ya kupunguza mashinikizo, inachochea vita. Hapa ndipo msimamo wa kisiasa wa kuungana na Washington unapogeuka kuwa kosa la kimkakati. Hivyo, uungaji mkono wa Ulaya kwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran si msimamo wa kisiasa usio na gharama. Baghaei anasisitiza kwamba: "Uungaji mkono wa Umoja wa Ulaya kwa vita vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya Iran ni ukiukaji mkubwa na wa wazi wa sheria za kimataifa." Kuunga mkono sera ya namna hiyo hakumuondolei mhusika dhima ya matokeo yake; mataifa ya Ulaya hayawezi kushiriki kisiasa katika mchakato huu huku yakijitenga na matokeo na taathira zake hasi.

Undumakuwili unaoonyeshwa na Umoja wa Ulaya kuhusiana na suala zima la utekelezaji kinyume cha sheria, kanuni za ndani ya Marekani dhidi ya mataifa mengine, umedhoofisha pakubwa madai ya Ulaya ya kuwa na uhuru wa kimkakati katika kupunguza mvutano na wakati huo huo kuunga mkono mashinikizo ya kidhalimu ya kiuchumi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kama Baghaei alivyoonya: "Ulaya lazima ichague kati ya kuwa mdau huru, au kuzoea sana kuwa mhudumu na mtekelezaji wa siasa za upande wa pili, kama inavyoonekana katika kesi hii ya hujuma ya kiuchumi ya Marekani dhidi ya Iran, ambapo Ulaya imeamua kutii na kutekeleza kikamilifu matakwa ya Marekani dhidi ya Tehran kinyume na maazimio na sheria za Ulaya yenyewe.