Biashara ya utumwa: UN inasema nchi zina wajibu wa kisheria wa kuzingatia fidia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i141148-biashara_ya_utumwa_un_inasema_nchi_zina_wajibu_wa_kisheria_wa_kuzingatia_fidia
Kwa miongo kadhaa sasa Afrika imekuwa ikidai haki na fidia. Sasa Umoja wa Mataifa unaitikia wito huo wa Waafrika.
(last modified 2026-09-02T12:49:51+00:00 )
Sep 02, 2026 12:46 UTC
  • UN yataka wathirika wa utumwa kulipwa fidia
    UN yataka wathirika wa utumwa kulipwa fidia

Kwa miongo kadhaa sasa Afrika imekuwa ikidai haki na fidia. Sasa Umoja wa Mataifa unaitikia wito huo wa Waafrika.

Kamati ya Umoja wa Mataifa inasema nchi zilizohusika moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika biashara ya utumwa ya kuvuka Bahari ya Atlantiki zinalazimika kisheria kulipa fidia. Sio kwa pesa tu bali pia kwa kuchukua hatua kivitendo.

Katika ripoti iliyochapishwa Jumatatu wiki hii, Kamati ya Kutokomeza Ubaguzi wa Rangi ilieleza kuwa "hatua kuu za kuwalipa fidia watu wenye asili ya Afrika zinapaswa kutekelezwa kwa kuwakilisha vipengee vyote vya kufikia suluhu.

Hii inafuatia tukio muhimu la mwezi wa Machi, ambapo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio lililoongozwa na Ghana likilaani biashara ya utumwa ya Bahari ya Atlantiki na kuutaja kuwa "uhalifu mbaya zaidi dhidi ya binadamu."

Matokeo ya kura yalikuwa ya ushindi mkubwa: Kura 123 ziliunga mkono azimio hilo lililoongozwa na Ghana.

Hata hivyo, Marekani, Argentina na Israel zilipinga azimio hilo, huku nchi 52, zikiwemo Uingereza na nchi zote 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya zikijiepusha kupiga kura.

Hati hiyo inaeleza kuwa biashara ya utumwa “ilivuruga mahusiano ya kiuchumi duniani” na “kusambaza utajiri uliopatikana kwa njia isiyo ya haki ambapo athari zake bado zipo hadi sasa.

Mnamo mwezi wa Juni, viongozi kutoka Afrika na Karibea walikutana nchini Ghana. Ujumbe wao ulikuwa wazi: Ombeni radhi, rudisheni kilichonyakuliwa na lipeni kinachodaiwa. 

Walitaka kurejeshwa turathi za kale za kitamaduni zilizoporwa.

Kati ya karne ya 15 na 19, Waafrika wasiopungua milioni 12.5 walisafirishwa wakiwa wamefungwa pingu hasa kutoka vituo vya pwani ya Atlantiki nchini Ghana, Nigeria na Senegal na kuuzwa katika bara Amerika.