Bei ya dizeli Marekani yavunja rekodi huku vita dhidi ya Iran vikiwadhuru Wamarekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i141222-bei_ya_dizeli_marekani_yavunja_rekodi_huku_vita_dhidi_ya_iran_vikiwadhuru_wamarekani
Wastani wa bei ya dizeli umefikia rekodi ya juu nchini Marekani, kufuatia vitendo vya uchokozi vya Marekani dhidi ya Iran na kufungwa kwa Lango Bahari la Hormuz, ambalo kabla ya vita lilikuwa likipitisha  takriban asilimia 20 ya mafuta yanayouzwa duniani.
(last modified 2026-09-05T12:00:00+00:00 )
Sep 05, 2026 11:50 UTC
  • Bei ya dizeli Marekani yavunja rekodi huku vita dhidi ya Iran vikiwadhuru Wamarekani

Wastani wa bei ya dizeli umefikia rekodi ya juu nchini Marekani, kufuatia vitendo vya uchokozi vya Marekani dhidi ya Iran na kufungwa kwa Lango Bahari la Hormuz, ambalo kabla ya vita lilikuwa likipitisha  takriban asilimia 20 ya mafuta yanayouzwa duniani.

Siku ya Ijumaa, bei ya dizeli ilipanda hadi kufikia dola 5.85 kwa galoni kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa vita vya kichokozi vya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran mnamo Februari 28.

Kupanda kwa bei ya dizeli, ambayo hutumika sana katika malori ya mizigo, kilimo, na shughuli za viwandani, kunamaanisha kuongezeka kwa gharama za usafiri na uzalishaji ambazo baadaye zinapandisha bei za vyakula, na kuleta athari kubwa kiuchumi na kuongeza gharama za maisha kwa ujumla.

Baadhi ya wafanyabiashara tayari wamezibebesha gharama hizo wananchi kupitia ada za ziada kwenye maagizo ya mtandaoni na vifurushi vinavyotumwa kwa posta.

Bei za bidhaa nyingine kama vile mavazi, vipodozi, na fanicha, ambazo pia husafirishwa kwa malori ya dizeli, treni, na boti, nazo zinatarajiwa kupanda.

Hali hii inaleta changamoto nyingine kwa chama tawala cha Republican kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa Novemba, huku umaarufu wa Rais Donald Trump ukizidi kuporomoka.

Kulingana na kura ya maoni ya hivi karibuni ya AP-NORC, watu 2 kati ya 3 wazima nchini Marekani wanapinga jinsi Trump anavyoshughulikia masuala ya uchumi.

Bei ya petroli ya kawaida pia imekuwa ikipanda, ingawa si kwa kasi kama bei ya dizeli. Wastani wa bei uko katika dola 4.15 kwa galoni, ikilinganishwa na dola 3.20 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Aidha katika soko la kimataifa mafuta ghafi ya petrili ya  Brent yameuzwa kwa zaidi ya dola 95 kwa pipa siku ya Ijumaa, ikilinganishwa na takriban dola 70 kabla ya kuanza kwa vita.

Iran imekuwa ikizuia usafiri kupitia Lango Bahari la Hormuz kutokana na vita vya uchokozi vya Marekani na utawala wa Kizayuni.

Iran imeruhusu meli zinazohudumia nchi zisizoegemea upande wowote, kama vile China, kupita, huku ikizuia meli zinazohusiana na wachokozi na wafuasi wao.