Waziri wa Fedha Uingereza atoa tahadhari kuhusu athari za kiuchumi za vita dhidi ya Iran
Waziri wa Fedha wa Uingereza, John Healey, ametoa tahadhari kali kwamba vita vinavyoendelea vya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran vinaongeza shinikizo kwenye uchumi wa Uingereza na fedha za serikali, jambo linalotishia kuyumbisha Bajeti ya mwezi Oktoba.
Healey ameliambia gazeti la Financial Times kuwa, “Kinachotokea Mashariki ya Kati kinaathiri mfumuko wa bei, ukuaji wa uchumi, na gharama za kukopa,” akikiri kuwa vita hivyo vinazidisha hali tete ya kiuchumi iliyopo.
Tahadhari hiyo imetolewa wakati kukopa kwa serikali kulipanda kwa kasi mapema wiki hii, hali inayoashiria wazi kuwa masoko ya kifedha yanazidi kuwa na wasiwasi kuhusu matokeo ya mfumuko wa bei kutokana na mzozo unaozidi kukua huko Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).
Healey amekiri kuwa mgogoro huo unavuka mipaka ya viashiria vya kifedha vya muda mfupi, akielezea tishio pana la kijiopolitika kama “sehemu ya ulimwengu hatari zaidi na usio na uhakika, na ni moja ya changamoto tunazopaswa kukabiliana nazo katika nchi hii.”
Vita vya kigaidi vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vimesababisha gharama za nishati kupanda kote barani Ulaya, huku Uingereza ikibeba sehemu kubwa ya mzigo huo.
Licha ya Mkataba wa Maelewano wa Islamabad uliotiwa saini baina ya Iran na Marekani tarehe 17 Juni, ambao ulikusudiwa kumaliza uhasama katika nyanja zote, Marekani imeendelea na mzingiro wake wa majini katika Ghuba ya Uajemi katika wiki za hivi karibuni na kushambulia maeneo kadhaa kusini mwa Iran. Wakati huo huo, Iran imejibu kwa kufunga Lango Bahari la Hormuz ambayo ni njia muhimu ya baharini dhidi ya maadui wavamizi.