Je, BRICS Itazuia Vipi Siasa na Hatua za Upande Mmoja za Marekani?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i141422-je_brics_itazuia_vipi_siasa_na_hatua_za_upande_mmoja_za_marekani
Mkutano wa 18 wa kilele wa BRICS mjini New Delhi unafanyika wakati ambapo kundi hilo si tena kama muungano wa kiuchumi wa mataifa yanayoinukia pekee; bali, limebadilika kuwa jukwaa muhimu la mashindano kuhusu sura ya baadaye ya mfumo wa dunia.
(last modified 2026-09-13T10:25:58+00:00 )
Sep 13, 2026 10:22 UTC
  • Je, BRICS Itazuia Vipi Siasa na Hatua za Upande Mmoja za Marekani?

Mkutano wa 18 wa kilele wa BRICS mjini New Delhi unafanyika wakati ambapo kundi hilo si tena kama muungano wa kiuchumi wa mataifa yanayoinukia pekee; bali, limebadilika kuwa jukwaa muhimu la mashindano kuhusu sura ya baadaye ya mfumo wa dunia.

Mkutano huo unaofanyika tarehe 12 na 13 Septemba kwa ajili ya kuadhimisha miaka ishirini tangu kuanzishwa kwa kundi hilo, umewakutanisha wanachama wake kumi na mmoja ambao kwa pamoja wanawakilisha takriban asilimia 49.5 ya watu duniani, asilimia 40 ya uchumi wa dunia na asilimia 26 ya biashara ya kimataifa. Hotuba iliyotolewa na Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kuhusiana na mkutano huu ilijikita hasa katika suala hilo. BRICS ina uwezo wa kubadilika kutoka kuwa jukwaa la kiuchumi tu na kuwa chombo madhubuti cha kupinga siasa na hatua za upande mmoja katika masuala ya kimataifa. Kwa kusisitiza ulazima wa kuanzishwa Benki ya Maendeleo ya BRICS na kupunguza utegemezi kwa dola, Rais wa Iran amewasilisha suala hilo kwa namna ambayo inathibitisha kuwa linavuka mipaka ya mahusiano ya kibiashara pekee. Kwa mtazamo wa Tehran, kiini cha suala hili ni kubadilishwa kanuni za mfumo wa uchumi wa kimataifa na kuzuia uwezekano wa kutumika zana za kifedha na sarafu kama silaha ya kutoa mashinikizo dhidi ya mataifa huru.

Dalili za dhahiri za mabadiliko haya zilianza kujitokeza wakati wa maandalizi ya mkutano huo wa kilele ambapo mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu wa nchi wanachama wa BRICS walitoa wito wa kufanyika marekebisho katika miundo ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, pamoja na kuongezwa nguvu ya kupiga kura kwa mataifa yanayoinukia kiuchumi na yale yanayoendelea. Pia wameonya dhidi ya ushuru wa upande mmoja na hatua za biashara na kifedha zinazoweka mzigo zaidi kwa uchumi wa nchi zinazoendelea, huku wakisisitiza uzingatiaji wa mifumo ya malipo ya mipakani na matumizi yanayoongezeka ya sarafu za kitaifa. Matukio haya ni muhimu sana, kwani yanaonyesha kwamba msimamo wa BRICS umebadilika kutoka malalamiko ya kisiasa tu na kuwa takwa muhimu la kurekebisha usanifu wa kifedha wa kimataifa.

Kwa mtazamo huu, Rais Pezeshkian anaiona BRICS kama chombo cha kukabiliana na "udikteta na siasa za upande mmoja." Mtazamo huu una umuhimu maalum kwa Iran kwani katika miaka ya hivi karibuni, imekabiliwa na matokeo hasi ya siasa za mfumo wa fedha wa kimataifa, vikwazo vya upande mmoja, na matumizi mabaya ya dola kuliko mwanachama mwingine yeyote wa BRICS. Hivyo, kupunguza utegemezi wa dola si lengo la kiuchumi tu kwa Iran, bali ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uhuru wa kisiasa na kiuchumi.

Hata hivyo, umuhimu wa mkutano wa kilele wa New Delhi utapimwa kwa uwezo wa BRICS wa kubadilisha kauli mbiu hizi kuwa mifumo madhubuti inayotekelezeka kivitendo. Kuanzisha mitandao huru ya malipo, kufanya miamala ya kibiashara kwa kutumia sarafu za kitaifa, kuimarisha benki ya maendeleo ya BRICS, na kuongeza ushiriki wa nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi katika taasisi za kifedha za kimataifa ni mchakato unaopaswa kutekelezwa hatua kwa hatua. Hata uchambuzi wa wataalamu unaonyesha kuwa BRICS haikusudii kufutilia mbali kabisa dola katika muda mfupi, bali inalenga kupunguza taratibu utegemezi wake kwa safari hiyo.

Katika muktadha huu, uwepo wa Pezeshkian katika mkutano wa kilele una umuhimu wa kipekee kijiopolitiki. Mgogoro unaohusisha Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, pamoja na hali ya wasiwasi katika Lango-Bahari la Hormuz, vimeliweka kundi la BRICS katika mtihani mkubwa. Mvutano kati ya Iran na Marekani umeathiri moja kwa moja usalama wa nishati na biashara ya kimataifa, huku migawanyiko miongoni mwa wanachama wa BRICS kuhusiana na mzozo huu pia ikijitokeza wazi. Hivyo, suala hili linavuka mipaka ya kutoa tamko la kisiasa tu ambapo sasa swali muhimu linaloulizwa ni iwapo BRICS inaweza kuchukua hatua kama mshiriki madhubuti na huru katika kukabiliana na mzozo unaoathiri mfumo wa uchumi na usalama duniani, au itaendelea kuwa jukwaa tu la mazungumzo matupu yasiyotekelezwa kivitendo.

Hotuba zilizotolewa na Pezeshkian katika mkutano wa kilele wa New Delhi kwa hakika zinatoa changamoto ya kimkakati kwa BRICS. Ikiwa kundi hili kwa kweli linawakilisha sehemu kubwa ya dunia, ni lazima lidai kuwa na sauti katika kuunda kanuni za uchumi wa kimataifa na siasa za dunia. BRICS sasa imevuka hatua ya kudhihirisha tu uwezo wake na kuingia katika awamu ya utekelezaji wa kivitendo. New Delhi inaweza kuwa mahala ambapo upinzani dhidi ya hatua za upande mmoja unageuka kuwa mabadiliko ya kitaasisi, uhuru wa kifedha na ushirikiano wa kivitendo, njia ambayo Iran inaiona kuwa athirifu zaidi katika kupunguza satwa na udhibiti wa dola na wakati huo huo kuimarisha ushirikiano wa pande nyingi.