China yatoa onyo kwa Japan, yakosoa mazoezi ya pamoja ya kijeshi inayofanya kila mara na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i141474-china_yatoa_onyo_kwa_japan_yakosoa_mazoezi_ya_pamoja_ya_kijeshi_inayofanya_kila_mara_na_marekani
China imekosoa hatua ya Japan ya kutangulia kupanga silaha za kimkakati za ushambuliaji na vilevile kwa mazoezi ya kijeshi inayoendelea kufanya kila mara kwa kushirikiana na Marekani na Australia, ikisema, vitendo hivyo vinaongeza hatari ya makabiliano katika eneo hilo.
(last modified 2026-09-15T10:41:35+00:00 )
Sep 15, 2026 10:36 UTC
  • China yatoa onyo kwa Japan, yakosoa mazoezi ya pamoja ya kijeshi inayofanya kila mara na Marekani

China imekosoa hatua ya Japan ya kutangulia kupanga silaha za kimkakati za ushambuliaji na vilevile kwa mazoezi ya kijeshi inayoendelea kufanya kila mara kwa kushirikiana na Marekani na Australia, ikisema, vitendo hivyo vinaongeza hatari ya makabiliano katika eneo hilo.

Jiang Bin, msemaji wa Wizara ya Ulinzi wa Kitaifa ya China, ametoa kauli hiyo ukiwa ni mjibizo kwa ripoti kadhaa kwamba vikosi vya nchi kavu vya Japan vinafanya mazoezi ya pamoja na majeshi ya Marekani na Australia katika maeneo ya Hokkaido na Kagoshima nchini Japan.

Kwa mujibu wa gazeti la China Daily, msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya China amesema: "Tunapinga vikali mazoezi haya ya pamoja."

Manuva ya pamoja yaitwayo "Ngao ya Mashariki 26" (Eastern Shield 26) yalianza Septemba 8 na yataendelea hadi Septemba 24.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi wa Kitaifa ya China amebainisha kuwa, lengo la mazoezi hayo ya kijeshi ni kuendeleza upangaji wa silaha za kimkakati za mashambulizi kwa kutumia anuani ya "Ngao", ambayo ni tishio kubwa kwa amani na utulivu wa kanda hiyo.

Amesema, Japan imekiuka mara kadhaa kanuni za msingi za sera yake ya kutetea amani na ya kujihami tu kwa kutengeneza silaha za mashambulizi za masafa marefu na kuharakisha mchakato wa "kuzijatiti tena kijeshi" kupitia mazoezi ya kijeshi ya nje ya mipaka yake.

"Kitendo chochote kinachoichochea tamaa ya kuwa na nguvu kubwa za kijeshi ya Japan kitalitumbukiza eneo kwenye dimbwi hatari, na mwishowe kuidhuru Japan yenyewe," ameeleza afisa huyo wa China.

Jiang Bin ametoa wito kwa Marekani, Australia na Japan "kuheshimu wasiwasi wa kiusalama zilionao nchi zingine, kurekebisha mwenendo wao usio sahihi, na kutoa mchango chanya kwa amani na utulivu wa kikanda kupitia uchukuaji hatua za kivitendo"…/