Katibu Mkuu wa UN: Imani ya wananchi kwa serikali inadorora, uhusiano baina yao unazidi kudhoofika
https://parstoday.ir/sw/news/world-i141476-katibu_mkuu_wa_un_imani_ya_wananchi_kwa_serikali_inadorora_uhusiano_baina_yao_unazidi_kudhoofika
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema demokrasia inakabiliwa na wakati mgumu huku migogoro ikiongezeka, imani ya wananchi kwa taasisi za serikali ikidorora na uhusiano kati ya raia na serikali zao ukizidi kudhoofika.
(last modified 2026-10-15T07:22:56+00:00 )
Sep 15, 2026 10:42 UTC
  • Katibu Mkuu wa UN: Imani ya wananchi kwa serikali inadorora, uhusiano baina yao unazidi kudhoofika

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema demokrasia inakabiliwa na wakati mgumu huku migogoro ikiongezeka, imani ya wananchi kwa taasisi za serikali ikidorora na uhusiano kati ya raia na serikali zao ukizidi kudhoofika.

Guterres ameyasema hayo katika ujumbe wake kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Demokrasia inayoadhimishwa leo Septemba 15.

Katibu Mkuu wa UN ameeleza kwamba, kinachowekwa hatarini si uchaguzi pekee, bali msingi mpana wa jamii pia, ambao unahakikisha haki za binadamu zinalindwa, utawala wa sheria unaheshimiwa na wananchi wanashiriki kikamilifu katika maisha ya kisiasa na kiraia.

Kwa mujibu wa Guterres, dunia inashuhudia mgawanyiko mkubwa unaozidi kuongezeka, huku migogoro ikizuka katika maeneo mbalimbali na imani kati ya wananchi na serikali ikipungua.

Amesisitiza kuwa, demokrasia haiwezi kujengwa kwa sanduku la kura pekee. Inahitaji mazungumzo ya mara kwa mara, ushirikiano na utayari wa kusikiliza mitazamo tofauti, ikiwemo sauti kutoka mashirika ya kiraia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza pia kwamba, demokrasia haipaswi kuchukuliwa kuwa jambo la kudumu bila juhudi za kuilinda.

Katika sehemu nyingine ya ujumbe wake, Guterres amesisitizia umuhimu wa michakato shirikishi ya kufanya maamuzi, inayowaleta pamoja watu kutoka sehemu mbalimbali za jamii ili kutoa mawazo yao na kushiriki katika masuala yanayowahusu.

Siku ya Kimataifa ya Demokrasia iliidhinishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 8 Novemba mwaka 2007 kupitia azimio namba 62/7 kwa lengo la kukuza na kuzingatia misingi ya demokrasia, pamoja na kuzihimiza serikali kuimarisha mipango ya kitaifa ya kuendeleza na kuimarisha demokrasia.

Siku ya tarehe 15 Septemba ilichaguliwa kwa pendekezo la Umoja wa Mabunge Duniani, (IPU) ikiendana na kumbukumbu ya mwaka 1997 ya Tamko la Ulimwengu kuhusu Demokrasia lililotolewa na umoja huo…/