Trump apanga kuipatia Israel 'shehena kubwa zaidi ya mabomu katika historia ya Marekani'
https://parstoday.ir/sw/news/world-i141494-trump_apanga_kuipatia_israel_'shehena_kubwa_zaidi_ya_mabomu_katika_historia_ya_marekani'
Ripoti moja inasema, serikali ya Trump inaandaa mpango wa kuupatia utawala wa kizayuni wa Israel shehena ya mabomu 40,000 yenye uzito wa pauni 2,000 kila moja, ambayo thamani yake ni dola bilioni 2.8.
(last modified 2026-09-16T03:35:28+00:00 )
Sep 16, 2026 03:34 UTC
  • Trump apanga kuipatia Israel 'shehena kubwa zaidi ya mabomu katika historia ya Marekani'

Ripoti moja inasema, serikali ya Trump inaandaa mpango wa kuupatia utawala wa kizayuni wa Israel shehena ya mabomu 40,000 yenye uzito wa pauni 2,000 kila moja, ambayo thamani yake ni dola bilioni 2.8.

Gazeti la The Washington Post limeripoti katika toleo lake la jana Jumanne, likimnukuu afisa mmoja wa Marekani, kwamba mpango huo unajumuisha mabomu 20,000 ya aina ya MK-84, 20,000 ya aina ya BLU-117, na vichwa vya mabomu 20,000 vya aina ya I-2000 vyenye uwezo mkubwa wa upenyaji.

Japokuwa mpango huo unaelezewa kuwa utafanyika kwa sura ya mauzo,  lakini utafadhiliwa kupitia mpango wa Marekani wa Ufadhili wa Kijeshi kwa Nchi za Nje (Foreign Military Financing), ambapo Washington hutoa fedha ambazo utawala huo hutumia kununua silaha za Marekani.

Taarifa kuhusu utumaji huo uliopendekezwa, wa kiwango cha kutisha cha mabomu katika historia ya Marekani, imewasilishwa kwa njia isiyo rasmi kwa kamati za Bunge la Marekani, huku utawala wa Trump ukiwashinikiza maafisa wa Bunge wauidhinishe.

Akizungumzia ripoti hiyo, mchambuzi mashuhuri wa mrengo wa kihafidhina nchini Marekani Tucker Carlson amekosoa vikali utumaji huo uliopangwa wa shehena ya mabomu, akitilia mkazo zaidi wingi wake ambao haujawahi kushuhudiwa.

"Huu unaonekana kuwa uhamishaji mkubwa zaidi wa silaha za kawaida za miripuko kutoka Marekani katika historia ya sasa," ameeleza Carlson katika andiko aliloweka kwenye mtandao wa X.

Carlson amelinganisha kiwango hicho cha tani 40,000 za mabomu zilizopendekezwa kupatiwa utawala wa kizayuni na operesheni kubwa za mashambulizi ya anga za Marekani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, akikumbusha kuwa shambulio la Machi 1945 la Jeshi la Anga la Nane (Eighth Air Force) dhidi ya Berlin lilihusisha takribani tani 3,000 za mabomu, nayo Operesheni Meetinghouse dhidi ya Tokyo ikahusisha karibu tani 1,600.

Amesema, kiwango hicho kikubwa kabisa cha utumaji wa mabomu kilichopendekezwa hakina mfano wowote wa kihistoria na akahoji uhalali wa kijeshi uliotumika kutetea upelekaji wa silaha kama hizo katika eneo la Asia Magharibi.

"Haihalalishiki kwa namna yoyote," ameandika Carlson, akisema kuwa ukubwa wa uhamishaji huo wa mabomu utamfanya mtu adhani kwamba utawala wa Israel unaendesha "Vita Vikuu vya Pili vya Dunia"…/