Waombolezaji Iran, duniani wajitokeza kwa wingi kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein AS
Mamilioni ya Waislamu katika nchi mbali mbali duniani wamejotokeza kwa mamilioni katika Siku ya Ashura kukumbuka siku alipouawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein AS.
Nchini Iran, tokea jana tarehe 9 Mfunguo Nne Muharram mamilioni ya waumini walijiunga na wenzao kote duniani katika vikao, majlisi na maombolezo ya kukumbuka misiba na masaibu yaliyomsibu Imam Hussein bin Ali AS ndugu na maswahaba zake waaminifu katika jangwa la Karbala nchini Iraq mwaka 61 Hijria. Siku ya kuuawa Shahidi Imam Hussein AS na wafuasi wake watiifu wapatao 72 hujulikana kama Siku ya Ashura.
Kilele cha maombolezo hayo duniani ni katika mji wa Karbala, Iraq iliko Haram Takatifu ya Imam Hussein AS ambapo wapenzi wa Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW na wapenda haki kutoka maeneo yote ya dunia wamejumuika kukumbuka tukio la Ashura. Maombolezo mengi makubwa yanafanyika pia katika nchi kama vile Lebanon, Syria, Pakistan, India, Uturuki, na miji mingie mikubwa duniani katika mabara ya Asia, Afrika, Ulaya na Amerika.
Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote na kwa kila mpenda haki na ukombozi duniani kwa mnasaba wa kukumbuka msiba huu mkubwa uliomfika Bwana Mtume Muhammad SAW na Uislamu kiujumla.