Afisa wa zamani wa CIA: Trump amebomoa muungano wa nchi za Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i55053-afisa_wa_zamani_wa_cia_trump_amebomoa_muungano_wa_nchi_za_magharibi
Afisa wa zamani wa shirika la ujasusi la Marekani CIA amesema kuwa rais wa nchi hiyo amebomoa muungano wa nchi za Magharibi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 28, 2019 23:50 UTC
  • Afisa wa zamani wa CIA: Trump amebomoa muungano wa nchi za Magharibi

Afisa wa zamani wa shirika la ujasusi la Marekani CIA amesema kuwa rais wa nchi hiyo amebomoa muungano wa nchi za Magharibi.

John McLaughlin aliyewahi kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa shirika la ujasusi la CIA la Marekani amesema kuwa, mingongano iliyopo katika utendaji na mienendo ya serikali ya Donald Trump inahatarisha miungano iliyopo baina ya nchi za Magharibi.

McLaughlin ameongeza kuwa, waitifaki wa Marekani katika nchi za Magharibi wamechanganyikiwa na hawajui waamini maneno na matamshi ya nani nchini Marekani. 

Katika kipindi cha utawala wake wa zaidi ya miaka miwili sasa nchini Marekani, Rais Donald Trump amekuwa akizishambulia kwa maneno nchi waitifaki wa serikali ya Washington na kuchukua maamuzi ya kihasama dhidi ya nchi hizo. 

Katika hatua yake ya hivi karibuni katika uwanja huo Trump amezitaja sera za kibiashara za Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kuwa ni za "kipumbavu". 

Macron na Trump

Mbali na kuwadhalilisha viongozi wa nchi waitifaki wa Marekani, Donald Trump pia amesababisha changamoto kubwa katika misingi ya uhusiano wa Marekani na nchi waitifaki. 

Wakati wa kampeni zake za uchaguzi wa rais hapo mwaka 2016 pia Donald Trump alisema kuwa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) limepitwa na wakati na halipo tena.