Jan 28, 2023 08:03 UTC
  • Mtaalamu wa UK: Magharibi imerudi kwenye zama za giza za uchomaji vitabu

Mtaalamu mmoja wa masuala ya kisiasa wa Uingereza amesema kuhusiana na kitendo cha hivi karibuni cha Wamagharibi cha kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu kwamba, jamii ya Magharibi imerejea katika zama za giza za uchomaji vitabu.

Makundi kadhaa yenye misimamo ya kufurutu mpaka nchini Sweden hivi karibuni yalifanya kitendo cha kifidhuli cha kuichoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu mbele ya ubalozi wa Uturuki mjini Stockholm. Kiongozi wa kikundi cha watu wenye misimamo ya kufurutu ada kinachojulikana kwa jina la Pegida nchini Uholanzi, naye pia aliiga na kufuata kitendo hicho baada ya kuchana kurasa za msahafu na kukichoma moto kitabu hicho kitakatifu cha mbinguni.
Kwa mujibu wa IRIB, Rodney Shakespeare, mchambuzi wa masuala ya kisiasa mjini London, amesema: "kwa kuchukua hatua kadhaa kama kuonyesha Waislamu ni maadui, kuichoma moto Qur'ani na kumvunjia heshima Mtume wa Waislamu, baadhi ya watu Magharibi wanathibitisha kuwa nchi za Magharibi zimerejea kwenye zama za giza za uchomaji moto vitabu na ufuatiliaji wa imani za watu.
 
Mtaalamu huyo wa masuala ya kisiasa amesema, Magharibi imesibiwa na hali ya kuemewa na akaongeza kuwa: "katika baadhi ya matukio, mataifa ya Magharibi hayajui nini chanzo cha matatizo na machafuko yao ya ndani, na kwa sababu hiyo inatolewa fursa kwa watu wenye misimamo ya kufurutu mpaka ili wazibabaishe fikra na akili za watu juu ya ukweli halisi wa mambo; na kwa maoni yangu, sababu kuu ya mashambulizi dhidi ya Waislamu, chuki dhidi ya Uislamu na kuichoma moto Qur'ani inatokana na kuemewa huko".
Wakati huohuo, Masoud Shajareh, Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Kibinadamu ya Kiislamu ya Uingereza, naye pia amekosoa mielekeo ya Wamagharibi katika kutafsiri maana ya uhuru wa kutoa maoni na akasema: Wanaodai kutetea uhuru wa kujieleza katika jamii za Magharibi ikiwemo Uingereza waliitaja hatua ya Waislamu ya kukichoma moto kitabu cha Aya za Shetani cha Salman Rushdie kuwa ni kupiga vita uhuru wa fikra na maoni, lakini watu hao hao sasa wanasema, kuichoma moto Qur'ani ni uhuru wa kujieleza.../