Jan 28, 2023 12:20 UTC
  • Ziara ya kiduru ya Lavrov katika nchi za Afrika; jitihada za Russia za kuzidisha satwa yake barani Afrika

Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Jumatatu tarehe 23 mwezi huu alianza safari ya kiduru kwa kuzitembelea nchi kadhaa za Kiafrika na hadi sasa amefanya safari huko Afrika Kusini, Eswatini, Angola na Eritrea.

Hii ni safari ya pili kufanywa na Lavrov barani Afrika katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia mwezi Julai mwaka jana pia alizitembelea nchi kadhaa za Kiafrika. Akiwa ziarani huko Eswatini, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameeleza kuwa, nchi yake haiingilia siasa za ndani za nyingine nyingine. Vilevile ametilia mkazo ushirikiano kati ya nchi mbili katika ziara yeke nchini Afrika Kusini.

Mazungumzo kuhusu Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Baraza la Kiuchumi la Russia na Afrika uliopangwa kufanyika kuanzia tarehe 26 hadi 29 mwezi Julai mwaka huu huko Saint Petersburg ni kati ya ajenda kuu zilizojadiliwa katika mazungumzo ya  Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia na viongozi wa Afrika Kusini.

Sergei Lavrov akiwa ziarani Pretoria, Afrika Kusini  

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameashiria  uingiliaji wa nchi za Magharibi katika suala la kufanyika maneva ya pamoja ya kijeshi kati ya Russia, Afrika Kusini na China na kueleza kuwa: Russia haitaki "chokochoko” zozote kuhusu mazoezi ya pamoja. Wakati huo huo serikali ya Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini imeeleza hamu na nia yake ya kuwa mpatanishi katika vita vinavyoendelea kati ya Russia na Ukraine. Suala hili lina mantiki kwa kuzingatia uanachama wa Russia na Afrika Kusini katika kundi la BRICS na uhusiano wa karibu kati ya nchi mbili hizo. Naledi Pandor Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amesisitiza kuwa nchi yake haitaburuzwa katika kuunga mkono upande wowote na amezikosoa nchi za Magharibi kwa kuishutumu Russia huku zikipuuza hatua nyingine za uvamizi na kichokozi kama mashambulizi yanayofanywa kila uchao na uvamizi wa utawala wa Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.   

Baadhi ya nchi za Kiafrika zimedhihirisha msimamo wa kutoegemea upande wowote kuhusu vita vinavyoendelea huko Ukraine. Nchi za Kiafrika zilijizuia kupiga kura kuunga mkono azimio la kwanza lililowasilishwa katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Machi mwaka jana lililolaani oparesheni ya Russia dhidi ya Ukraine. Aidha Eritrea, Syria, Korea ya Kaskazini, China na Belarus ni nchi tano ambazo zilipiga kura ya hapana kupinga azimio hilo. Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amekosoa melengo ya jitihada za Wamagharibi za kujaribu kuzidisha satwa na ushawishi wao barani Afrika.  

Sergei Lavrov ameeleza kuwa: Marekani na nchi za Ulaya ambazo zinataka nchi za Kiafrika zisitishe ushirikiano wao na Russia, kwa hakika zinapigania kurejesha utegemezi na zama za ukoloni wa nchi za  barani Afrika kwa madola ya Magharibi. 

Suala muhimu linaonekana katika ziara hii ya kiduru ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia katika nchi za Kiarika ni juhudi zinazofanywa na Moscow ili kujitoa katika hali ya kutengwa kisiasa kwa kuzidisha ushirikiano wa kisiasa na kidiplomasia na nchi za bara hilo; na pia kuzishawishi nchi hizo kuunga mkono misimamo yake, kutafuta fursa mpya  za kiuchumi na kibiashara na kuibua masoko mapya barani Afrika. 

Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia 

Nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zimeiwekea vikwazo vikali zaidi Russia katika nyanya zote zinazowezekana; na hatua hiyo imeisababishia Moscow vizuizi na mibinyo na aina mbalimbali. Ni jambo la kawaida katika mazingira kama haya Russia kutafuta washirika wapya katika nyuga za kisiasa, kibiashara na kiuchumi; ambapo Moscow imeamua kuelekeza juhudi zake katika kuimarisha uhusiano na nchi ambazo hazikuunga mkono sera za Magharibi za kuiwekea vikwazo Russia bali zinataka kulinda na hata kupanua uhusiano wao na Moscow katika sekta na nyanja mbalimbali. Kwa mujibu wa weledi wa mambo na kwa kuzingatia mchakato wa sera za nje za Russia, hatua ya Moscow ya kutoa zingatio maalumu na kutilia maanani pakubwa nchi za Kiafrika inaashiria kuanza kwa juhudi za dhati za Moscow za kuboresha uhusiano wa pande zote na nchi za bara hilo na kuwa na satwa na ushawishi mkubwa barani humo.

Inaonekana kuwa, sasa Moscow imejikita na kuelekeza juhudi zake katika kupanua uhusiano wa kisiasa na nchi za Kiafrika. Viongozi wa Moscow wamesisitiza mara kadhaa kuhusu umuhimu wa kuwa na uhusiano na nchi za Kiafrika. Kuhusiana na suala hilo, Rais Vladimir Putin wa Russia ameeleza kuwa, ushirikiano wa nchi yake na nchi za Kiafrika ni wa kistratejia na wa muda mrefu na kwamba moja ya vipaumbele vya sera za nje za Russia ni kustawisha uhusiano na nchi za Kiafrika na taasisi za kikanda za bara hilo. 

Theodore Murphy, Mkuu wa Kitengo cha Afrika katika Baraza la Uhusiano wa Nje la Ulaya ameeleza kuwa: Russia imepata fursa ya kurejesha ushawishi wake Afrika kwa kutoa misaada ya kiusalama ya masharti nafuu kwa nchi za bara hilo kulinganisha na nchi za Magharibi. 

Tags