Jan 29, 2023 08:18 UTC
  • Mauaji ya kikatili ya raia mwingine mweusi; ukatili usio na mwisho wa polisi wa Marekani

Siku ya Ijumaa na baada ya kuchapishwa picha za kutisha za kupigwa kinyama Tyre Nichols, Mmarekani mweusi mwenye umri wa miaka 29 na polisi huko Memphis, katika jimbo la Tennessee, wimbi jipya la maandamano limeanza nchini humo na hasa katika miji ya Memphis, Boston, Chicago, Detroit, New York City, Portland, Oregon na Washington dhidi ya ukatili unaofanywa na polisi dhidi ya watu weusi.

Tyre Nichols, ambaye alisimamishwa na polisi Januari 7 na kukabiliwa na ukandamizaji pamoja na hatua za mabavu za polisi kwa madai ya kuendesha gari kwa njia isiyofaa na hatari, aliaga dunia Januari 10 siku tatu baada ya kufikishwa hospitalini, kutokana na majeraha makali aliyopata kutokana na kipigo cha mmbwa alichopata kutoka kwa polisi hao. Video ya kukamatwa Nichols inaonyesha kwamba maafisa wa polisi walimshambulia na kumpulizia pilipili kwa muda wa dakika tatu, wakatumia bunduki ya kumfisha ganzi na kumpiga makonde makali kijana huyo masikini mweusi mwenye umri wa miaka 29. Katika video hiyo, Nichols anasikika akiita na kuomba msaada wa mama yake wakati akipigwa na polisi. Maafisa watano waliohusika na kifo cha Nichols, ambao wote ni weusi pia, walitimuliwa kutoka Idara ya Polisi ya Memphis wiki iliyopita na kushtakiwa kwa mauaji ya daraja la pili na uhalifu mwingine.

Mojawapo ya madhihirisho muhimu zaidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Marekani ambao umekuwa ukiendelea kwa mamia ya miaka katika nchi hiyo inayodai kutetea haki za binadamu na uhuru, ni ubaguzi wa rangi na miamala ya kibaguzi dhidi ya watu weusi, kwa namna ambayo ubaguzi dhidi yao katika sekta za elimu, kazi na masuala ya kijamii limekuwa ni jambo la kawaida.

Rais weusi Marekani waandamana kulaani ukatili wa polisi dhidi yao

Kwa mujibu wa Barack Obama, rais wa zamani wa Marekani, ubaguzi wa rangi upo katika msimbo jeni au kwa ibara nyingine DNA ya Wamarekani. Moja ya madhihirisho ya tatizo hilo ambalo limekuwa likiongezeka katika miaka ya hivi karibuni, ni unyanyasaji na ubaguzi usio na kikomo wa polisi wa Marekani dhidi ya watu weusi. Takwimu zinaonyesha kuwa wahanga wakuu wa ukatili wa polisi wa Marekani ni watu weusi na chimbuko la ukatili huo ni ubaguzi wa rangi uliokita mizizi katika jamii ya Marekani. Suala la ukatili wa kutisha wa polisi ya Marekani dhidi ya watu weusi, hasa baada ya mauaji ya kikatili na yasiyo ya haki ya George Floyd, Mmarekani mweusi, Mei 25, 2020, yaliyotekelezwa na afisa wa polisi mzungu kwa jina Derek Chauvin, katika mji wa Minneapolis, Minnesota, na ambayo yaliibua maandamano makubwa nchini Marekani, limekuwa likizingatiwa sana katika ngazi za kimataifa.

Kwa mujibu wa takwimu, watu weusi wana uwezekano wa kuuawa na polisi mara tatu zaidi kuliko watu weupe. Kwa hakika, sehemu kubwa ya jeuri ya wabaguzi wa rangi katika jamii ya Marekani ni dhidi ya watu wachache wa rangi na kidini, ikiwa ni pamoja na watu weusi, ambapo polisi weupe wabaguzi wa rangi wana nafasi kubwa katika uhalifu huo. Suala hilo ni moja ya sababu kuu za maandamano na ghasia zinazotokea mara kwa mara katika miji tofauti ya Marekani. Licha ya ahadi nyingi zinazotolewa kwa ajili ya kurekebisha tabia za polisi ya Marekani, lakini hakuna hatua zozote za maana zinazochukuliwa katika uwanja huo na ndio maana maafisa wa polisi wamekuwa wakiendeleza tabia za mabavu na mauaji dhidi ya raia weusi wa nchi hiyo.

Kesi ya karibuni zaidi katika uwanja huo ni mauaji ya Tyre Nichols, ambapo video iliyosambazwa kuhusu tukio hilo inaonyesha kipigo cha mmbwa alichopata kijana huyo mweusi na hatimaye kupelekea kupoteza maisha. Kitendo hicho cha polisi kilikuwa cha kinyama na cha kutisha kiasi kwamba kimepelekea hata maafisa wakuu wa Marekani kukilaani. Mkurugenzi wa FBI Christopher Ray amesema: "Kilichotokea ni kitendo cha kusikitisha. Nimeshtushwa na kutiwa hofu na video hii. Siwezi kupata neno zuri la kuelezea mshtuko nilioupata."

Wabunge wa Congress ya Marekani pia wametoa radiamali zao kuhusu tukio hilo. Bernie Sanders, seneta wa kujitegemea kutoka jimbo la Vermont, ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba: "Wahusika wa mauaji haya ya kikatili wanapaswa kuadhibiwa, lakini pamoja na hayo kuadhibiwa kwao hakutamfufua Tyer. Tunapasa kufanya kila tunaloweza kwa ajili ya kukomesha ukatili wa polisi dhidi ya watu wa rangi nchini Marekani.

Polisi wakimpiga kinyama Tyre Nichols

Ripoti nyingi za mashirika ya kutetea haki za binadamu pia zinaonyesha kuwa ubaguzi wa rangi wa kimfumo, ambao ni moja ya viashiria vya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Marekani, na matumizi ya mara kwa mara ya unyanyasaji wa polisi dhidi ya jamii za wachache unaendelea kama kawaida nchini humo.

Rais Joe Biden wa Marekani, alisema baada ya mauaji ya Tyre Nichols kuwa ataishinikiza Congress ya nchi hiyo ipitishe sheria ya marekebisho ya polisi ya Marekani, ambayo inajulikana kama "Haki kwa George Floyd katika Utekelezwaji Sheria na polisi". Idara ya polisi ya Marekani kwa kawaida hufumbia macho uhalifu unaofanywa na maafisa wa polisi wanaotumia mabavu au kuua watu weusi kinyume cha sheria. Mfumo wa mahakama wa Marekani pia umekuwa ukipuuza na kutowachukulia hatua kali polisi wanaohusika na mauaji, na hili limechochea kuendelea ukatili wa polisi dhidi ya watu weusi.

Tags