Jan 30, 2023 02:46 UTC
  • Waziri: Migomo itatatiza usafiri wa umma kote nchini Ufaransa

Waziri wa Uchukuzi wa Ufaransa amesema migomo ya wafanyakazi wa sekta hiyo kuanzia kesho Jumanne inatazamiwa kulemaza usafiri wa umma katika pembe zote za nchi hiyo ya Ulaya.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Clement Beaune alisema hayo jana Jumapili akizungumza katika televisheni ya LCI na kueleza kuwa, "Hali itakuwa mbaya mno katika uchukuzi wa umma. Tunatazamia kulemaa kwa shughuli za usafiri wa umma kwa kiasi kikubwa kesho, (Jumanne) itakuwa siku ngumu mno."

Licha ya waziri huyo kudai kuwa serikali ya Rais Emmanuel Macron ipo tayari kwa ajili ya mazungumzo na miungano ya wafanyakazi, lakini wakuu wa jumuiya hizo za kutetea maslahi ya wafanyakazi wa umma wamekuwa wakisisitiza kuwa, viongozi wa Ufaransa wamekuwa wakipuuza matakwa na maslahi ya wafanyakazi kila kunapofanyika mazungumzo.

Wahudumu wa sekta ya uchukuzi na sekta nyinginezo nchini Ufaransa wamekuwa wakifanya migomo na maandamano kwa muda mrefu sasa, kulalamikia sera za Macron na hususan mageuzi tata ya pensheni yanayotazamiwa kuanza kutekelezwa mwaka huu wa 2023.

Nchi hiyo ya Ulaya imekuwa ikishuhudia maandamano ya mara kwa mara, ya kulalamikia sheria hiyo wanaoitaja kuwa ya kibepari. Wafanyakazi nchini Ufaransa wanalalamikia ongezeko la umri wa kustaafu kutoka umri wa miaka 62 ya sasa hadi miaka 65 katika sheria hiyo tatanishi.

Maandamano dhidi ya serikali Ufaransa

Mbali na kulalamikia mageuzi hayo ya sheria ya kustaafu, wananchi wa Ufaransa wanalalamikia pia mfumko wa bei za bidhaa, mgogoro wa nishati, na ughali wa maisha uliotokana na mtikisiko wa uchumi wa nchi hiyo.

Ongezeko kubwa la mfumuko wa bei na gharama ya maisha nchini Ufaransa kutokana na kuiwekea Russia vikwazo, na kutokuwapo mlingano baina ya gharama za matumizi na mapato ya sehemu kubwa ya Wafaransa, kumesababisha wimbi hilo la migomo katika nchi hiyo ya Ulaya.

Tags