Jun 01, 2023 06:17 UTC
  • China yakabidhi nyumba 225 zilizoandaliwa kwa ajili ya waathiriwa wa tetemeko la ardhi huko Syria

Serikali ya China imekabidhi kwa serikali ya Syria nyumba 225 zenye kuhamishika zilizojengwa hapo kabla kwa ajili ya raia wa nchi hiyo walioathiriwa na tetemeko la ardhi ili kuwawezesha raia hao kurejea katika maisha yao ya kawaida.

Hati ya makabidhiano ya nyumba hizo ilisainiwa huko Damascus na Hussein Makhlouf Waziri wa Serikali za Mitaa na Mazingira wa Syria na Balozi wa China huko Syria, Shi Hongwei. Nyumba hizo 225 tayari zimewasili katika bandari huko katika mji wa Latakia kaskazini magharibi mwa Syria na zinatazamiwa kuanza kugawiwa kwa raia walioathirika na tetemeko la ardhi katika mikoa ya kaskazini huko Latakia na Aleppo.  

Baada ya kusaini hati hiyo ya makabidhiano, Balozi wa China nchini Syria, Shi Hongwei alieleza wasiwasi mkubwa wa nchi hiyo kuhusu athari za tetemeko la ardhi nchini Syria, na kusisitiza juu ya azma ya China kutoa misaada mbalimbali kwa Syria kwa kuzingatia mahitaji maalum ya nchi hiyo. Amesema, China itaendelea kutoa misaada ya kibinadamu kwa wananchi wa Syria. Balozi Shi amesema hivi na hapa ninamnukuu: "Tutatoa misaada yote inayowezekana kwa wananchi wa Syria walioathiriwa na zilzala na kushirikiana zaidi katika uwanja huo.  

Naye Hussein Makhlouf Waziri wa Serikali za Mitaa na Mazingira wa Syria amesifu uungaji mkono na misaada athirifu ya serikali ya China kwa nchi yake. Tetemeko kubwa la ardhi lililokuwa na ukubwa wa 7.8 kwa kipimo cha rishta lilitokea kusini mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria mapema mwezi Fabruari mwaka huu. Itakumbukwa kuwa nchi mbalimbali ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zilitoa misaada mbalimbali kwa waathiriwa wa zilzala huko Syria na Uturuki. 

Tetemeko la ardhi lililoikumba Syria mapema mwezi Februari mwaka huu