Jun 01, 2023 06:31 UTC
  • Sergei Lavrov
    Sergei Lavrov

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov, amekosoa shutuma zilizotolewa na balozi wa Marekani nchini Afrika Kusini kuhusu madai ya kutuma silaha Russia kutoka Pretoria na kusema: Balozi wa Marekani anapaswa kuzingatia kazi yake la si vinginevyo.

Akizungumzia madai yaliyotolewa na balozi Reuben E. Brigety II kuhusu usafirishaji wa silaha eti zilizopelekwa na meli ya mizigo ya Lady R hadi Russia, Sergei Lavrov amesema: Tofauti na nchi za Magharibi zinazoiunga mkono Ukraine, Russia haijawahi kukiuka kanuni za kimataifa katika suala la kusambaza silaha.

Ameashiria hatua ya nchi za Magharibi ya kuipatia Ukraine risasi za uranium iliyokhafifishwa na kusema: Nchi za Magharibi, zinadai kuwa haziegemei upande wowote katika matukio ya Ukraine, huku zikiendelea kutuma kiasi kikubwa cha silaha za masafa marefu na zisizo salama kwa serikali ya Kiev. Amesisitiza kuwa silaha hizo si salama na zinawazodhuru hata watumiaji wake.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Russia ameongeza kuwa, "Magharibi inaendelea kutoa misaada ya silaha kwa Ukraine wakati mamlaka ya nchi hiyo imetishia kuwaua Warusi wote, hivyo ni bora kwa mabalozi wa Marekani kuzingatia zaidi sura ya Washington katika maoni ya umma ya dunia."

Wiki kadhaa zilizopita balozi wa Marekani nchini Afrika Kusini, Ruben Brighetti, alidai kuwa, nchi hiyo iliipelekea Russia silaha mwezi Disemba mwaka jana kupitia meli ya Russia iliyotia nanga katika kituo cha jeshi la wanamaji cha Simmons Town mjini Cape Town.

 Madai hayo yalikadhibiishwa vikali na serikali ya Pretoria. 

Maafisa wa Russiai na baadhi ya wataalamu na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi wamevitaja vita vya Ukraine kuwa ni vita vya niaba kati ya Magharibi na Russia.