Jun 01, 2023 11:30 UTC
  • Islamic Centre of England
    Islamic Centre of England

Makumi ya mashirika na jumuiya za Kiislamu nchini Uingereza zimepinga vikali uingiliaji wa serikali ya nchi hiyo katika masuala ya Waislamu.

Wawakilishi wa makumi ya mashirika na jumuiya za Kiislamu nchini Uingereza, zimemwandikia barua Orlando Fraser, mkuu wa Kamisheni ya Misaada ya Uingereza, (Charity Commission) yakipinga vikali kuwekwa kwa mkurugenzi asiye Muislamu kusimamia masuala ya Kituo cha Kiislamu, yakitaka kufutwa uamuzi huo.

Imeelezwa katika barua hiyo kwamba, uamuzi huo umechukuliwa kwa malengo ya kisiasa na unaendana na maslahi ya watu wenye chuki dhidi ya Uislamu ambao wamelenga kituo hicho cha kijamii na mahali pa ibada.

Jumuiya za Kiislamu zilizotayarisha barua hiyo zimeeleza wasiwasi wao kuhusu uingiliaji kati wa Kamisheni ya Misaada ya Uingereza katika masuala ya ndani ya vituo vya kidini na kusisitiza kwamba, taasisi hiyo haina mamlaka ya kutoa maoni kuhusu ubora wa programu za mashirika ya kidini.

Imeelezwa katika barua hiyo kwamba: Kuteuliwa meneja asiyekuwa Mwislamu kwa ajili ya Kituo cha Kiislamu cha Uingereza, ambaye hafahamu mahitaji ya kiroho na kidini ya Waislamu, ni ishara kwamba kamisheni hiyo haina uelewa wa kutosha kuhusu matakwa na mahitaji ya jamii ya Kiislamu.

Islamic Centre of England

Kituo cha Kiislamu cha Uingereza ni miongoni mwa vituo vikuu vya jamii ya Waislamu wa mataifa mbalimbali kwa ajili ya kutekeleza majukumu na ibada za kidini mjini London; na katika miezi ya hivi karibuni kimekuwa kikilengwa kwa mashambulizi ya makundi mbalimbali yanayopinga Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na makundi yanayopiga vita Uislamu.