Oct 09, 2023 07:33 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Oktoba 9

Karibu tuangazie baadhi ya matukio ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbalimbali za dunia.

Iran yachota medali 54 Michezo ya Asia

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemaliza katika nafasi ya saba kwenye Michezo ya Asia iliyofanyika huko Hangzhou nchini China, baada ya kukusanya jumla ya medali 54 kwenye mashindano hayo. Wanamichezo 289 wa Iran wameng'ara kwenye mashindano hayo ya kibara katika michezo na kategoria mbalimbali na kutwaa medali 13 za dhahabu, fedha 21 na shaba 20. Baadhi ya wanariadha wa Iran waliotwaa medali za dhahabu kwenye mashindano hayo ya bara Asia ni Afshin Salimi na Yousef Sabri (Wushu), Sadegh Azarang (Kurash), Hossein Rasouli (Urushaji wa kisahani), Mohammad-Hadi Saravi (Mieleka mtindo wa Greco-Roman safu ya kilo 97) na Reza Alipour (Ukweaji). Wairani wamezoa pia medali kochokocho kwenye michezo ya mieleka, taekwondo na voliboli, miongoni mwa michezo mingine.

Michezo ya Asia

Kadhalika wanamichezo kadhaa wa Jamhuri ya Kiislamu wamevunja rekodi kwenye michezo mbalimbali kwenye mashindano hayo ya kibara. Mwenye China imeibuka kidedea kwenye mashindano hayo ya kibara kwa kukusanya jumla ya medali 383 zikiwemo 201 za dhahabu, huku nafasi ya pili na tatu zikitwaliwa na Japan na Korea Kusini. Wanamichezao zaidi ya 12,000 kutoka nchi 45 wanachama wa Baraza la Olimpiki la Asia wameshiriki mashindano hayo yaliyoanza Septemba 23 na kufunga pazia lake Jumapili hii ya Oktoba 8.

Muaythai; Iran yatwaa medali kibao Uturuki

Wapambanaji wa mchezo wa Muaythai wa Iran wametia kibindoni medali tano za kung'aa kwenye mashindano ya kimataifa ya vijana wenye chini ya miaka 23 kwenye mchezo huo mjini Antalya, Uturuki. Miongoni mwa vijana wa Iran waliong'ara kwenye mashindano hayo ya Kombe la Dunia ya IFMA ni mtoto wa kike, Setareh Morshedi aliyetwaa medali ya fedha baada ya kuzidiwa ujuzi na hasimu wake kutoka Russia katika fainali ya vijana wenye chini ya miaka 17 katogoria wa wanamichezo wenye chini ya kilo 60. Zahra Kianpour (-67kg) na Kiarash Ahamdi Chegini (-86kg) wametwaa medali ya fedha na shaba kwa usanjari huo, katika katogoria ya wanamichezo wenye chini ya miaka 21. Wairani wengine waliopa Jamhuri ya Kiislamu medali kwenye mchezo huo unaofahamika pia kama masumbwi ya Thai ni Mohammad-Ali Mazaheri (-38kg) katika safu ya wanamichezo wenye chinia ya miaka 11 na Maedeh Sadeghzadeh (-36kg) katika katogoria ya wenye chini ya miaka 13. Mashindano hayo ya ubingwa wa dunia ya Muaythai kwa vijana ulifanyika baina ya Septemba 29 na Oktoba 7 katikak mji bandari wa Antalya, pwani ya kusinimagharibi mwa Uturuki.   

Soka Wanawake Afrika

Timu ya taifa ya soka ya wanawake wasiozidi umri wa miaka 20 ya Kenya Rising Starlets, siku ya Jumapili ilishuka dimbani kuvaana na Angola uwanjani Nyayo jiji Nairobi, katika mchuano wa raundi ya kwanza ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la Wanawake mwakani. Akina dada hao wa Kenya waliipa Angola kichapo cha mbwa kungia msitini, kwa kuichabanga mabao 6-1. Valerie Nekesa alifungwa mabao 3 ya hatrick, huku Charity Midewa akifanikiwa kucheka na nyavu mara mbili. Bao la sita la Kenya lilifungwa na Faith Naliaka. Kocha wa Rising Starlets ya Kenya, Beldine Odemba anasema, ndio kwanza mkoko umealika maua. Siku ya Jumamosi, Cameroon iliisagasaga Botswana mabao 2-0 katika mchuano mwingine uliopigwa mjini Doula. Mshindi wa jumla wa mechi zote mbili atakutana na mshindi kati ya Cameroon na Botswana katika raundi ya tatu na ya nne baadaye mwaka huu 2023. Mshindi atafuzu moja kwa moja kwa Kombe la Dunia nchini Colombia kuanzia kati ya Septemba 5-22 mwaka ujao 2024.

Katika droo ya Ligi ya Mabingwa Afrika zilizofanyika Afrika Kusini siku ya Ijumaa, Kundi A inajumuisha Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Pyramids FC ya Misri, TP Mazembe ya DRC, na FC Nouadhibou ya Mauritania. Kundi B ikizileta pamoja timu za Wydad Csablanca ya Morocco, Simba SC ya Tanzania, ASEC Mimosa ya Kodivaa na Jwaneng Galaxy ya Botswana. Klabu ya Yanga ya Tanzania imepangwa kwenye Kundi D na Al Ahly SC ya Misri, CR Belouizdad na Medeama ya Ghana, huku Kundi C ikizijumuisha Petro Atletico ya Angola, CR Belouzdad ya Algeria, Al Hilal ya Sudan na Esperence ya Tunisia. Na kwa harakanikudokeze pia Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo Kundi A inajumuisha USM Alger, Future FC, Supersport United na Al Hilal, huku Kundi B ikizileta pamoja Zamalek, Sagrada Esperanca, S.O.A.R na Abu Salim. Kundi C ina timu za Rivers United, Club Africain, Dreams FC na APC Lobito wakati ambapo Kundi D inazijumuisha RS Berkane, Diables Noirs, Stade Malien na Sekhukhune United.

Dondoo za Hapa na Pale

Rais William Ruto ameliongoza taifa la Kenya kumpongeza mshikilizi mpya wa rekodi ya mbio za masafa marefu duniani Kelvin Kiptum. Dkt Ruto amemtaja mwanariadha chipukizi Kitum kama shujaa, baada ya kuiletea Kenya fahari kwa kuvunja rekodi ya Chicago Marathan, Jumapili Oktoba 8. Kiptum ameandikisha rekodi mpya ya dunia kwenye mbio hizo za Chicago Marathon 2023, nchini Marekani, iliyokuwa imeshikiliwa na Mkenya mwenza Eliud Kipchoge. Amemaliza mbio hizo kwa kutumia saa 2 na sekunde 35, na kuvunja rekodi ya saa 2 na dakika 1. Kipchoge alikuwa mmiliki wa rekodi hii tangu alipotimka na kuibuka mshindi kwenye mbio za Berlin, Ujerumani Septemba 25, 2022. Bingwa wa London Marathon, Sifan Hassan raia wa Uholanzi aliibuka kidedea kwenye safu ya wanawake mjini Chicago, baada ya kumaliza mbiuo hizo za kilomita 42 kwa kutumia saa 2, dakika 13 na sekunde 44. Mkenya Ruth Chepng'etich aliibuka wa pili huku nafasi ya tatu ikitwaliwa na raia wa Ethiopia Megertu Alemu.

Mbali na hayo, dunia ilibakia kinywa wazi Jumanne usiku baada ya timu maarufu za Manchester United na Arsenal ziliposhindwa kuwika mbele ya limbukeni katika mechi za makundi za kuwania ubingwa Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA). Matokeo ya kushangaza zaidi yalishuhudiwa Old Trafford, wakati ambapo wenyeji Man U walichapwa mabao 3-2 na Galatasaray kutokana na mabao ya Wilfried Zaha, Mohammed Kerem Akturkoglu na Mauro Icardi, wakati Rasmus Hojlund akiwafungia wenyeji Mashetani Wekundu, mabao yote mawili.

Manchester watakutana na FC Copenhagen katika mechi ijayo mnamo Novemba 29, siku ambayo Galatsaray itaalika Bayern Munich jijini Istanbul nchini Uturuki. Kwingineko, licha ya kutangulia kuona lango kupitia kwa bao la Gabriel Jesus, kocha Mikel Arteta alishuhudia vijana wake wa Arsenal wakichapwa 2-1 ugenini na Lens ya Ufaransa. Jesus alifunga bao lake mapema dakika ya 14, lakini matumaini yake yakazimwa na mabao ya Adrien Thomasson na Elye Wahi waliofunga dakika za 25 na 69 mtawaliwa.

Gunners katika ubora wao

Gunners siku ya Jumapili walijiliwaza na kuondoa maruweruwe ya kunyoroshwa kwenye UEFA, kwa kuitandika Man City bao moja bila jibu katika Ligi Kuu ya Uingereza. Bayern wanaongoza Kundi A katika UEFA kwa pointi sita, wakifuatiwa na Galatasaray. Lens walio na pointi nne ndio vinara wa Kundi B mbele ya Arsenal kwa tofauti ya pointi moja. Katika matokeo ya mechi nyingine zilizochezwa Jumanne, Copenhagen ilitandikwa mabao 2-1 na Bayern Munich, Inter Milan iliizaba Benfica 1-0, Union Berlin ilichapwa mabao 3-2 na Braga, RB Slazburg ilinyoroshwa magoli 2-0 na Real Sociedad huku na Real Madrid ikiisasambua Napoli mabao 3-2 Napoli.

Na kwa kutamatisha, sasa ni wazi kuwa, fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2030 zitachezwa katika mabara matatu tofauti. Hii ni baada ya Morocco, Uhispania na Ureno kushinda mbio za kuwania kuwa wenyeji wa mashindano hayo makubwa zaidi ya mpira wa miguu. Kadhalika Uruguay, Argentina na Paraguay zimeidhinishwa kuwa wenyeji wa mechi tatu za kwanza za mashindano hayo yatakayozileta pamoja timu 48. Gianni Infantino, Rais wa Shirikisho la Soka Duniani FIFA sanjari na kuthibitisha habari hizo siku ya Jumatano amesema, Baraza la FIFA ambalo linawakilisha ulimwengu mzima wa kandanda, kwa kauli moja limeafiki mechi hizo zipigwe katika nchi hizo zilizoko katika mabara ya Afrika, Ulaya na Amerika ya Latini mwaka 2030, wakati ambapo dunia ya soka itakuwa inasherehekea karne moja tangu Kombe la Dunia lichezwe kwa mara ya kwanza mwaka 1930 nchini Uruguay.

.........................TAMATI.................