Mfululizo wa vipindi vya 'Ukatili wa Mabudha dhidi ya Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar' na Sauti
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya kwanza ya makala yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar.
Ndugu wasikilizaji jamii ya watu wa kabila la Rohingya ni moja ya jamii za wachache duniani ambazo zimedhulumiwa sana. Hii ni kwa kuwa, karibu kila siku hujiri dhulma na ukandamizaji mkubwa dhidi ya watu wa jamii hiyo katika hali ambayo ukandamizaji huo huwa hauakisiwi wala kuripotiwa.

Je, jamii hiyo ya wachache inaishi wapi duniani na inapitisha vipi maisha yake? Hayo na mengine ndio mtakayoyasikiliza katika mfululizo wa vipindi hivi, Karibuni
****************************
Mwezi Januari mwaka 2017 vyombo mbalimbali vya habari vilisambaza picha ya kutisha ya mwili wa mtoto mmoja mwenye umri wa miezi 16 wa kabila la Rohingya ambao ulikutwa kando ya mto Naf ulio mpakani mwa Myanmar na Bangladesh. Kuenea kwa picha hiyo kulikoziumiza nyoyo za walimwengu kulikumbushia tukio chungu la mwaka jana la kuokotwa mwili wa Alan Kurdi, mtoto mchanga raia wa Syria ambaye alifariki dunia katika harakati za familia yake kukimbia vita. Mwili wa Alan Kurdi uliokotwa katika pwani ya Uturuki ambapo viongozi na watu wote duniani waliguswa na kuumizwa sana na tukio hilo. Mtoto huyo wa Kiislamu wa kabila la Rohingya mkazi wa mkoa wa Rakhine nchini Myanmar, alikuwa anaitwa Muhammad.

Yeye na watu wa familia yake walikuwa wamekimbia ukatili katika mkoa huo dhidi ya Waislamu. Hata hivyo familia ya Muhammad akiwemo kaka yake wa miaka mitatu, mama na mjomba wake, walifariki dunia kwa kuzama maji katika mpaka wa Myanmar na Bangladesh. Baba wa mtoto huyo mwenye umri wa miezi 16 alinukuliwa akisema: 'Kila wakati ninapoona picha ya mwanangu Muhammad ninatamani laiti na mimi ningekufa. Kwani maisha ya duniani kwangu hayana thamani yoyote ile.' Mwisho wa kunukuu.

Kama tulivyosema, jamii ya Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar ni jamii ya wachache ambayo inaongoza duniani kwa kufanyiwa ukandamizaji na ukatili dhidi yake. Hii ni kwa kuwa serikali ya nchi hiyo inawahesabu Waislamu wa kabila hilo kuwa ni Wabangladesh katika hali ambayo akthari ya duru za historia na kimataifa zinawatambua watu hao kuwa ni wazawa asili wa mkoa wa Rakhine. Baba wa Muhammad anasimulia kwa kusema: “Walituvamia katika kijiji chetu ambapo helikopta za kijeshi zilianza kutushambulia. Askari wa Myanmar walitulenga kwa silaha mbalimbali. Hatukuweza kubakia ndani ya nyumba zetu hivyo tukaamua kukimbia na kutafuta hifadhi msituni.

Babu na bibi yangu walichomwa moto wakiwa hai mjini Rakhine. Bila huruma jeshi la Myanmar liliteketeza moto kijiji chetu chote na hakukusalia kitu ambacho kilisalimika na moto huo.” Kadhalika baba wa mtoto huyo aliyefariki dunia kwa maji anasema kuwa, katika kujaribu kunusuru maisha yao kutokana na ukatili na jinai za askari wa Myanmar, walikimbilia kijiji kingine. Anaendelea kusema: “Nilitembea kwa miguu kwa muda wa siku sita mtawalia. Kwa siku nne mfululizo sikuweza kula. Katika kipindi cha siku sita sikulala usingizi usiku wala mchana. Na hata tulipokimbilia kijiji kingine askari wa serikali ya Myanmar walikuwa wakitufuata na hivyo kulazimika kuendelea kukimbilia sehemu zenye amani.” Mwisho wa kunukuu.
*************************************
Ndugu wasikilizaji katika kipindi chote cha siku sita hizi, baba yake Muhammad alikuwa ametengana na familia yake bila kujua mahala ilipo. Katika hali hiyo ya kukimbia huku na kule hatimaye akafika katika Mto Naf ambao unapita katikati ya mpaka wa Myanmar na Bangladesh. Bila kujali maisha yake alijitupa katika mto huo mkubwa ambapo baadaye aliokolewa na mvuvi mmoja raia wa Bangladesh na hivyo kumvusha kutoka ardhi ya Myanmar.

Zafar Alam, baba wa mtoto Muhammad alifanya juhudi kubwa zenye lengo la kuihamishia familia yake nchini Bangladesh. Anaendelea kusimulia kwa kusema: “Nikiwa Bangladesh nilimpata mmoja wa wamiliki wa boti na nikamtaka anisaidie kuwavusha mke na wanangu wawili kutoka Myanmar. Tarehe 4 Disemba mwaka jana nilifanikiwa kuwasiliana nao ambapo walionyesha kukata tamaa ya maisha kutokana na tabu waliyoipitia na hiyo ikawa mara yangu ya mwisho kuongea na familia yangu. Wakati naongea na mke wangu nilisikia sauti ya Muhammad akiniita.

Saa chache baada ya mawasiliano hayo ya simu mtu huyo alianza kuitorosha familia yangu. Hata hivyo baada ya polisi wa Myanmar kufahamu kwamba akthari ya Waislamu walikuwa wanakusudia kuvuka Mto Naf na kuelekea nchini Bangladesh walianza kuwafukuza na kuwamiminia risasi. Katika kujaribu kukwepa kuuawa, yule mmiliki wa boti aliwapakia Waislamu wengi katika boti yake. Hata hivyo kutokana na kwamba boti ilikuwa imejaza watu kupita kiasi ikiwemo familia yangu, ilizidiwa uzito na hivyo kuzama.” Mwisho wa kunukuu. Zafar Alam alipata habari ya tukio hilo kupitia mawasiliano ya simu ikiwa imepita siku moja tangu kujiri tukio hilo. Anasema: “Mtu mmoja alinipigia simu na kuniambia kuwa, mwili wa mtoto wangu Muhammad umeonekana kando ya mto. Mtu huyo aliyenipigia simu alinitumia picha ya mwili wa mwanangu ambapo niliamini kwamba ni yeye na hapo ndipo nilipopatwa na uchungu zaidi.” Mwisho wa kunukuu.
***************************************
Kisa cha familia ya Zafar Alam kinabainisha mateso na machungu ya familia nyingi za Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar. Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa karibu watu elfu 34 wa kabila la Rohingya wamevuka mpaka wa Myanmar kuingia Bangladesh katika kipindi cha wiki na miezi ya hivi karibuni. Zafar Alam anasema kuwa Mto Naf ndio unaofahamu idadi kamili ya Waislamu wa Rohingya ambao wamepoteza maisha yao katika maji ya mto huo. Ndugu wasikilizaji ni vyema mfahamu kwamba Myanmar au kwa jina lingine 'Burma' zamani ilikuwa ni moja ya nchi masikini zaidi za Asia Kusini Mashariki ambayo ilipata uhuru mwaka 1948 kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Katika harakati za kupigania uhuru, Waislamu wa nchi hiyo walitumia nguvu zao zote katika kupambana na mkoloni huyo.

Ni kutokana na mapambano makali ya Waislamu hao, ndipo Waingereza wakapandikiza sumu ya mifarakano kwa lengo la kusambaratisha nguvu ya Waislamu hao na sambamba na kuondoka nchini humo, ikawachochea Mabudha kuanzisha hujuma dhidi ya Waislamu. Mwaka 1942 Mabudha walitumia silaha za Waingereza kuanzisha mauaji makali dhidi ya Waislamu, ambapo karibu watu laki moja miongoni mwao waliuawa kwa umati katika jimbo la Rakhine ambalo awali lilikuwa likiitwa kwa jina la Arakan. Jamii ya Waislamu wa Burma inarudi nyuma hadi karne nyingi zilizopita huku ikiwa na utawala wa Kiislamu wa kujitegemea wa kipindi kirefu. Kwa mujibu wa takwimu za serikali, Waislamu hao ambao wanatambuliwa kwa jina la Rohingya, ni laki nane pekee ambao wanaunda asilimia nne ya jamii yote ya Myanmar.

Kwa kuzingatia siasa za ubaguzi na zilizo dhidi ya ubinaadamu zinazotekelezwa na serikali ya nchi hiyo, serikali hiyo imekuwa ikipunguza kwa makusudi idadi hiyo ya Waislamu. Hii ni katika hali ambayo duru za kujitegemea zinatoa idadi halisi ya Waislamu hao ambapo baadhi zinakadiria idadi hiyo kufikia watu milioni 15.
Katika miongo iliyopita Waislamu hao wamekuwa wakikumbwa na ukatili na jinai mbalimbali dhidi yao kutoka serikali na Mabudha wa Myanmar ambapo kutokana na jinai hizo maelfu yoa wamekuwa wakipoteza maisha kwa halaiki au kulazimika kuwa wakimbizi. Kwa mfano tu Waislamu waliolazimika kuyahama makazi yao kutoka Myanmar kwenda Bangladesh mwaka 1978 walikuwa laki tatu, mwaka 1988 laki moja na elfu 50, mwaka 1991 laki tano na mwaka 1992 walikadiriwa kuwa malaki. Inafaa kuashiria kuwa, hadi muongo wa 1970 Miladia jamii ya Waislamu wa Rohingya ilitambuliwa kuwa jamii ya wachache nchini Myanmar. Hata hivyo mwaka 1982 baada ya kujiri marekebisho ya katiba yaliyoenda sambamba na kuingia madarakani makamanda wa jeshi, Waislamu hao hawakutambuliwa tena kama raia halali wa Myanmar.

Ni baada ya hapo ndipo taratibu serikali hiyo ya kijeshi ikaanzisha miamala mibaya dhidi ya watu wa Rohingya sambamba na kukanyaga wazi wazi haki zao za kimsingi kuanzia uhuru wao wa mtu binafsi, kidini na kibinaadamu. Kutokana na mashinikizo mengi yaliyo dhidi ya ubinaadamu, maelfu ya Waislamu hao walilazimika kukimbilia nchi jirani. Aidha ukatili wa serikali ya Burma dhidi ya jamii hiyo ya Waislamu uliongezeka maradufu baada ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11 mwaka 2001 huko nchini Marekani. Hali hiyo ilitokana na serikali ya Naypyidaw kuathiriwa sana na misimamo hasi ya madola ya Magharibi kuuhusu Uislamu. Katika wimbi jipya la jinai dhidi ya Waislamu wa Myanmar, Mabudha wenye kuchupa mipaka, walitekeleza jinai za kutisha dhidi ya maelfu ya Waislamu wasio na hatia wala ulinzi wowote wa nchi hiyo.
Ndugu wasikilizaji sehemu ya kwanza ya makala haya yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar inakomea hapa. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./