Mfululizo wa vipindi vya 'Ukatili wa Mabudha dhidi ya Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar' na Sauti
Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya pili ya makala yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar.
Katika kipindi cha kwanza tulikunukulieni kisa kichungu cha Zafar Alam kinachohusu kifo cha familia yake akiwemo mtoto mchanga wa miezi 16 kwa jina la Muhammad. Pia tulizungumzia jinai za kutisha zinazofanywa na Mabudha dhidi ya jamii ya Waislamu chini ya kimya cha jamii ya kimataifa. Leo pia tutaendelea kujadili suala hilo hivyo endeleeni kuwa nami hadi mwisho wa kipindi. Ndugu wasikilizaji mwezi Juni mwaka 2012 mamia ya Mabudha walivamia basi lililokuwa limewabeba Waislamu waliokuwa wametoka msikitini eneo la Arakan kwenda mji wa Rangoon (au Yangon), na kuwaua kwa namna ya kutisha Waislamu hao.

Jambo la kushangaza ni kuwa waliotekeleza hujuma hiyo kwa mikono yao wenyewe ni viongozi wa Kibudha. Mmoja wa watu walioshuhudia jinai hiyo ya kutisha anasimulia kwa kusema: "Baada ya kutekeleza mauaji hayo dhidi ya Waislamu waliokuwa ndani ya gari hilo, sambamba na kuwachuna ngozi zao, viongozi wa Kibudha waliichukuwa miili ya wahanga hao na kuilaza barabarani na kuanza kuitemea mate na kuimwagia pombe. Wakati wakifanya hivyo walikuwa wakisema kuwa wanasherehekea ushindi wa mauaji ya Waislamu." Mwisho wa kunukuu. Baada ya tukio hilo, mwezi Agosti mwaka huo huo wa 2012 ikiwa ni miezi miwili tu imepita tokea kujiri tukio hilo chungu, Mabudha hao katili waliwaua kwa umati Waislamu wapatao elfu 20.

Ndugu wasikilizaji ni vyema mkafahamu kwamba, hadi sasa duru huru za kujitegemea hazijaweza kufahamu sababu hasa ya ukatili na mauaji hayo ya kikaumu yanayofanywa na Mabudha dhidi ya Waislamu. Hii ni katika hali ambayo kwa kipindi chote cha historia ya Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar hawajawahi kufanya jinai yoyote dhidi ya Mabudha. Aidha haijawahi kuthibiti kuwa kuna wakati ambapo serikali za kigeni zimewahi kuwatumia Waislamu hao kufanya uasi dhidi ya serikali kuu ya Myanmar kama ambavyo pia hakuna ushahidi wowote unaoelezea uhaini wao.
***********************************
Ubakaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na mabinti wa Kiislamu na kadhalika kuwalazimisha kufanya matendo machafu yanayohesabiwa na Waislamu kuwa ni haramu, ni miongoni mwa jinai dhidi ya binaadamu ambazo zinafanywa kila uchao na Mabudha hao wasio na mioyo ya utu wala huruma. Aisha Solhi, mwanamke wa Kiislamu wa Myanmar alifanyiwa mahojino na gazeti la nchini Misri la al-Watan na kusema: "Mabudha wa Burma wanatuamuru ima kula nyama ya nguruwe, kunywa pombe au kukubali kuuawa. Kwa kawaida Waislamu huwa wanapendekeza kufa kuliko kuishi katika maisha ya namna hiyo." Mwisho wa kunukuu.

Kwa hakika kisa cha Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar ni chenye kusikitisha sana ambapo hata wataalamu wa kuchunguza ukiukaji wa haki za binaadamu duniani na wenye uzoefu mkubwa katika kazi hiyo wanakiri kwamba, hawajawahi kushuhudia ukatili na jinai za kutisha kama zile zinazowakabili Waislamu wa Burma. Kuhusiana na suala hilo, Lenny Aruydsun, kiongozi wa timu ya watu wanne kutoka ofisi ya Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) anasema: "Nasema kwa hakika kwamba mahojiano niliyoyafanya na wahanga wa jinai dhidi ya Waislamu wa Burma, ni kadhia ambayo haiwezi kuvumilika." Mwisho wa kunukuu. Ripoti ya timu hiyo ilisambazwa mwaka jana ambapo ilikuwa ya kushtua sana. Uchunguzi huo uliofanyika kwa kuwahoji wanawake na wanaume 204 na iliyotolewa mwezi Oktoba mwaka jana iliwahusisha Waislamu wa mjini Rakhine na hata wale waliokimbilia nchi jirani ya Bangladesh. Akthari ya watu waliohojiwa walithibitisha kuwajua watu na wanawake waliouawa au kubakwa na Mabudha.

Lenny Aruydsun anasema: "Sijawahi kushuhudia katika kipindi kifupi sana cha kuhojiana na wahanga upate idadi kubwa ya uthibitisho wa jinai kiasi ambacho tulipata nchini Myanmar." Kadhalika afisa huyo wa masuala ya haki za binaadamu anathibitisha kwamba ripoti zinazohusiana na mauaji, ubakaji, ukandamizaji ukiwemo wa adhabu na udhia mbalimbali dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohongya, unaofanywa na polisi wa Mabudha wa Myanmar, ni za kushtua sana. Kwa hakika picha na jinai za mauaji yanayofanywa kuwalenga Waislamu wa Myanmar, zinauchoma moyo wa kila mwanadamu kutokana na ukubwa wa jinai hizo.
Wahanga hao ni Waislamu ambao si tu kwamba wanaondoshwa kutoka katika ardhi zao asili, bali wanakabiliwa pia na aina mbalimbali za mauaji na ukatili dhidi yao. Nyumba zao zinachomwa moto, kubakwa wanawake na mabinti wao, kuteswa kwa aina ya kutisha na kuuawa na kuchomwa moto wakiwa hai. Swali la msingi ni hili kwamba, ikiwa serikali ya Burma inawatambua Wailamu wa kabila la Rohingya kuwa sio raia halali wa nchi hiyo, je hiyo inaweza kuwa sababu ya kutekeleza jinai na mauaji ya kutisha dhidi yao?
Jinai za hivi karibuni dhidi ya Waislamu hao zilizoanza tangu mwezi Juni 2012, ni jinai mbaya na hatari sana zilizofanywa na Mabudha katili dhidi ya watu hao wa kabila la Rohingya nchini Myanmar. Katika awamu hiyo, Mabudha magaidi wa Burma wakisaidiwa na askari wa usalama wa nchi hiyo, walitekeleza jinai zisizoweza kuelezeka dhidi ya jamii ya Waislamu hao madhlumu.

Hata kama serikali ya Myanmar daima imekuwa ikikanusha kushiriki katika jinai za Mabudha kuwalenga Waislamu, lakini taasisi moja ya Haki za Binaadamu yenye makao yake mjini London, Uingereza ya The Equal Rights Trust ilitangaza wazi kwamba, jeshi la Burma huwa linawasaidia Mabudha katika kufanya mauaji dhidi ya Waislamu. Hata kama wimbi la jinai dhidi ya Waislamu wa Rohingya zilishika kasi kuanzia mwaka 2012, lakini mauaji hayo yameendelea kwa muda mrefu chini ya kimya cha jamii ya kimataifa na asasi za kutetea haki za binaadamu duniani. Hata hivyo kwa masikitiko makubwa, si Umoja wa Mataifa wala jamii ya kimataifa ya karne ya 21 zimewahi kutoa radiamali kuhusiana na jinai hizo dhidi ya ubinaadamu huko Burma, bali zote kwa pamoja zimejizuia kutoa sauti yoyote ya kulaani mauaji hayo. Licha ya taasisi kubwa za haki za binaadamu kushuhudia filamu na picha za kutisha za mauaji ya umati dhidi ya Waislamu yanayofanywa na Mabudha, lakini zimesalia kimya kuhusiana na suala hilo. Muamala usiojali majukumu na usio na taathira yoyote ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na kadhia ya Waislamu wa Rohingya, unakumbusha kimya cha umoja huo katika mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa Bosnia na Herzegovina, ambapo kimya hicho kilibariki Malaki ya Waislamu kuuawa kinyama.
**************************************
Julai mwaka 2012 Dalai Lama, kiongozi wa Mabudha duniani alifanya safari katika jimbo la Kashmir, wakati ambao Mabudha wa Myanmar walikuwa wakifanya mauaji makali dhidi ya Waislamu.

Katika safari hiyo Dalai Lama sambamba na kudai kuwa alikuwa akifuatilia hali ya wafuasi wake kwa ajili ya usalama na kutatua migogoro kwa njia ya amani, alipuuza kabisa habari za jinai zilizokuwa zikifanywa na wafuasi wake (yaani Mabudha wa Myanmar) katika kuwaua watoto na kuwabaka wanawake na mabinti wa Kiislamu wasio na ulinzi nchini Burma. Katika hali ya kushangaza, kiongozi huyo wa Mabudha duniani hakuashiria kwa aina yoyote ile kile kilichokuwa kinafanywa na Mabudha hao wakatili nchini Myanmar. Dalai Lama aliamua kukaa kimya kuhusiana na kadhia hiyo, baada ya vyombo vya habari kufichua kuwa serikali ya Naypyidaw sambamba na kushiriki katika mauaji dhidi ya Waislamu, ilikuwa pia ikibariki jinai hizo. Suala hilo lilimfedhehesha kiongozi huyo wa Mabudha duniani na ndipo mwaka mmoja baadaye yaani 2013 akaamua kutoa tamko kuhusu suala hilo. Katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na Shirika la Habari la ABC News la nchini Marekani kuhusiana na ukubwa wa mauaji na jinai dhidi ya binaadamu zinazofanywa na wafuasi wake huko Burma alisema: “Ni suala la kuumiza sana.” Mwisho wa kunukuu.
Huku Dalai Lama akisema hayo, radiamali na mapendekezo ya rais wa Myanmar juu ya utatuzi wa kadhia hiyo ilikuwa ya kushangaza sana.

Rais wa wakati huo wa Myanmar, Thein Sein ambaye Wamagharibi wanamsifu kwa jina la ‘Mrekebishaji’ kutokana na jinai zake kubwa za kuwaua kwa halaiki Waislamu wa Rohingya, alitoa pendekezo kama njia ya utatuzi wa mogoro huo kwa kusema: “Watu wote wa Rohingya lazima waondolewe nchini au wahifadhiwe katika kambi za wakimbizi za Umoja wa Mataifa.” Mwisho wa kunukuu.

Naye kwa upande wake Aung San Suu Kyi, mshindi wa zawadi ya Nobel wa nchini Myanmar alijaribu kuzitaja jinai hizo kama mgogoro wa kikaumu na wa ndani tu huku akiwambia waandishi wa habari: “Mgogoro wa kikaumu ambao umeiumiza nchi ni lazima uchunguzwe na kutatuliwa kimantiki.” Mwisho wa kunukuu. Hata hivyo mwanzoni mwa mwezi huu, mwanamke huyo aliwashangaza wengi, alipoitangazia dunia kwamba, hakuna mauaji ya umati yaliyowahi kutokea katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa Burma.
Ndugu wasikilizaji sehemu ya pili ya makala haya yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar inakomea hapa. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./