SPOTI, MACHI 09
Ulimwengu wa Michezo, Machi 09
Hujambo mpenzi msikilizaji na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri kitaifa na kimataifa ndani ya siku saba zilizopita….nakusihi tuandame sote hadi tamati ya kipindi…….karibu……
Corona yazidi kuvuruga ratiba za spoti
Zimwi la Corona limeendelea kuzusha wasi wasi katika sekta na kona mbalimbali duniani, na ulimwengu wa michezo haujasazwa na virusi hivyo hatarishi. Ratiba za ligi, michezo na mechi mbali mbali duniani zimefutwa kabisa au kuakhirishwa kutokana na virusi hivyo. Katika baadhi ya nchi, ligi kuu za soka zinaendelea kuchezwa bila ya uwepo wa mashabiki viwanjani. Hapa nchini Iran, ligi na michezo yote imesimamishwa ili kuzuia maambukizi zaidi ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi hivyo. Aidha Shirikisho la Soka Duniani FIFA limeafikiana na Muungano wa Mashirikisho ya Soka Asia AFC juu ya kusimamishwa kwa mechi za kikanda katika eneo la Asia Magharibi kutokana na virusi vya Corona ambavyo vimeua watu zaidi ya elfu 3 katika pembe mbalimbali za dunia hususan nchini China ambako ilianzia. Michuano hiyo sasa itachezwa mwezi Septemba mwaka huu, huku mechi za nusu fainali zikitazamiwa kuchezwa Oktoba. Fainali ya AFC itapigwa Novemba kama ilivyokuwa imepangwa awali. Huku hayo yakiarifiwa, wasimamizi wa Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza wamezuia wachezaji na waamuzi kusalimiana kwa kupeana mikono kuanzia mechi za wikiendi hii hadi watakapopewa taarifa nyingine.

Hii inakuja kutokana na hofu ya virusi vya Corona. Hatua hiyo inakuja baada ya serikali kuitaka EPL kuimarisha mipango yake ya kujikinga na Corona. Timu zitajipanga kama kawaida lakini timu mwenyeji ndio itapita mbele ya timu iliyoikaribisha bila kupeana mikono. Kabla ya hapo, Shirikisho la Soka Tanzania TFF lilitangaza zuio kama hilo kwa wachezaji na waamuzi kutosalimiana kwa kupeana mikono.
Soka Wanawake: Kenya yalimwa na Chile
Timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Kenya Harambee Starlets ilikubali kichapo cha mbwa katika mechi yake ya pili ya soka ya kimataifa ya Turkish Women's Cup baada ya kuaibishwa mabao 5-0 na Chile katika mechi ya Kundi B iliyogaragazwa Jumamosi uwanjani Gold City mjini Alanya nchini Uturuki. Chile iliingia mchuano huu ikipigiwa upatu kunga'ara, hasa kwa sababu inaorodheshwa katika nafasi ya 36 kwenye viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa). Kenya ambayo itamenyana na Black Queens ya Ghana katika mechi yake ya mwisho ya makundi Machi 10, ipo katika nafasi ya 133 duniani. Kabla ya hapo, Starlets ambao ni mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) Kenya walitangaza kuwasili kwao katika mashindano ya kimataifa ya Turkish Women’s Cup kwa kishindo baada ya kulipua Northern Ireland Under-19 kwa mabao 2-0 mjini Alanya, Uturuki, Jumatano usiku. Kocha wa Starlets David Ouma amesema timu hiyo inatumia mashindano haya ya timu nane kujipiga msasa kabla ya kuvaana na Tanzania katika mechi yake ya raundi ya kwanza ya kutafuta tiketi ya kushiriki Kombe la Bara Afrika (AWCON) baadaye mwaka huu 2020. Akina dada hao wa kocha David Ouma, ambao wamealikwa kushiriki makala hayo ya tatu kwa mara yao ya kwanza kabisa, wanashikilia nafasi ya pili katika Kundi B kwa tofauti ya ubora wa magoli na Chile waliopepeta Black Queens kutoka Ghana 3-0. Kenya na Tanzania zitapepetana mwezi Aprili, huku mshindi akikutana na mshindi wa mechi nyingine ya raundi ya kwanza kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sao Tome & Principe katika raundi ya pili ili kuingia AWCON 2020.
Soka: Watani wa jadi wavaana mbele ya rais
Watani wa jadi wa soka nchini Tanzania, klabu ya Simba na Yanga siku ya Jumapili walishuka dimbani kuvaana kwa mara nyingine, tena, mara hii wakiupiga mbele ya Rais John Magufuli. Bernard Morrison, kiungo mshambuliaji wa klabu ya Yanga Jumapili alifanya kazi yake iliyompelekea Bongo kwa kuifunga Simba bao 1-0 kwenye mchezo wa mzunguko wa pili uliochezwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam. Bao pekee la ushindi lilifungwa dakika ya 44 kwa mpira wa adhabu alioupiga kiungo huyo raia wa Ghana na kuuzamisha mzima langoni baada ya Aishi Manula kuzidiwa nguvu na mpira huo.

Mpaka dakika 90 zinakamilka Simba ya Meddie Kagere ilishindwa kufurukuta mbele ya Yanga waliokuwa wakifanya mashambulizi ya hatari huku nyota wa mchezo kwa Yanga akiwa ni Metacha Mnata ambaye aliokoa michomo mingi ya hatari kwa Simba iliyokuwa ikipigwa na Meddie Kagere. Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 50 ikiwa imecheza mechi 25 huku Simba ikiwa na pointi 68 imecheza mechi 27 za Ligi Kuu Bara. Kichapo hicho mbele ya rais kimewaghadhabisha sana mashabiki wa Simba.

Wakati Simba ikivaana na Yanga nchini Tanzania, nchini Kenya pia watani wengine wa jadi siku ya Jumapili walikuwa wanatoana udhia, klabu a Gor Mahia na AFC Leopards.
Katika mchuano huo unaofahamika kama debi la mashemeji ugani Kasarani jijini Nairobi, Gor au ukipenda Sirkali walifanikiwa kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya vijana hao wa Ingwe. Ni mechi ambayo Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa upinzani Raila Odinga walikuwa wakiishuhudia moja kwa moja uwanjani hapo. Bao la dakika ya 27 la Boniface Omondi lilitosha kuwapaisha vijana hao wanaonolewa na Steven Polack na kujiongezea alama tatu kwenye kapu lao.

Kwa Kogalo kuizaba Leopard na kuibuka mshindi kwa mara ya 30 kwenye debi hilo la mashemeji la 89, wanazidi kutuama na kutamalaki kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Soka nchini Kenya, wakiwa na alama 54. Leopards wako katika nafasi ya sita, kwa mwanya wa pointi 11 nyuma ya Gor, lakini hawajakata tamaa katika kampeni yao ya kutwaa ubingwa wa msimu huu. Leopards iliishinda Gor mara ya mwisho mnamo 2016, ugani Kasarani katika mechi ambayo ilimalizika kwa 1-0.

Mara ya kwanza timu hizo zilipokutana mnamo 1968, Gor Mahia walichapwa mabao 2-1.
Debi la City; Man U yaitolea uvivu City
Ilikuwa wikendi ya madebi. Mbali na debi la watani wa jadi Tanzania, na debi la mashemeji Kenya, Uwanja wa Old Trafford ulishuhudia debi la Machester la Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza. Manchester United ilishuka dimbani kutoana udhia na Manchester City katika mechi hiyo iliyokuwa na msisimko wa aina yake. Bao la Anthony Martial katika awamu ya kwanza na la Scott McTominay dakika za lala salama yalitosha kulizamisha jihadi la Man City. Martial akiandikisha historia katika uwanja wa Old Trafford huku akiibuka mchezaji wa pili wa United kufunga mabao mfululizo katika gozi la Ligi Kuu dhidi ya Manchester baada ya Eric Cantona. Dakika tano za nyongeza zilikuwa baraka kwa United ambao walipachika bao lao la pili kupitia kwa McTominay ambaye alitumia vyema masihara ya goli kipa Ederson ambaye alikuwa ameondoka langoni.

Vijana wa Ole Gunnar Solskjaer kwa sasa wamekamilisha ligi kwa kuikabithi City kichapo cha pili kwa mara ya kwanza tangu uongozi wa kocha mstaafu Sir Alex Ferguson. Katika mchezo mwingine wa wikendi, Chelsea iliigaragaza Everton mabao 4-0 nyumbani Stamford Bridge na kufikisha alama 48 wakiwa katika nafasi ya nne. Liverpool inasalia kileleni mwa jedwali la EPL wakiwa na alama 82 wakifuatiwa na City wenye pointi 57 huku orodha ya tatu bora ikifungwa na Leicester City wenye alama 50. Man U kwa sasa wameridhika na nafasi ya tano wakiwa na pointi 45.
………………….TAMATI……………..