Mar 15, 2021 07:15 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Machi 15

Hujambo mpenzi mwanaspoti wa na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa.

Persepolis na Esteqlal zasonga mbele Kombe la Hazfi

Watani wa jadi klabu za Persepolis na Esteqlal za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimesonga mbele kwenye Raundi ya 16 ya Kombe la Mtoano (Hazfi) baada ya kufanya vyema katika mechi zao za hivi karibuni. Siku ya Ijumaa, Wekundu wa Tehran waliinyoa bila maji klabu chovu ya daraja la pili ya Mes Novin kwa kuizaba mabao 3-0 katika Uwanja wa Bahonar mjini Kerman. Katika mchuano huo wa Raundi ya 32, Persepolis haikusakata soka la viwango labda kwa kuwa ilikuwa inavaana na timu dhaifu, na ikaishia kupoteza nafasi nyingi za kuongeza mabao. Mlango wa magoli ya Persepolis ulifunguliwa na Kamal Kamyabinia kunako dakika ya 38, kabla ya Omid Alishah kufunga mawili katika dakika za 58 na 64 kipindi cha pili. Kabla ya hapo, mahasimu wao klabu ya Esteqlal ilikuwa imepata ushindi kwa mbinde wa mabao 2-1 iliposhuka dimbani kuvaana na Peikan katika Uwanja wa Shahre Quds. Cheick Diabate aliwapa wenyeji bao la ufunguzi kunako dakika ya 17, huku Mohammad Daneshgar akifanya mambo kuwa mawili kwa nunge katika dakika ya 38.

Wachezaji wa Persepolis wakishangilia bao

 

Hata hivyo Ebrahim Salehi aliipunguzia masaibu Peykan katika kipindi cha pili, kwa goli la kufutia machozi kunako dakika ya 58. Katika michuano mingine ya Raundi ya 32 iliyopigwa, Malavan Bandar Anzali 2 – 1 Vista Turbine Tehran huku Esteghlal Mollasani 0 – 0 Shahin Bandar Ameri (3-4 penati). Shahrdari Bardaskan iliadhibiwa mabao 3-0 na Khooshe Talaei Saveh, huku Pars Jonoubi Jam ikitoa kichapo sawia na hicho dhidi ya Pas Hamedan. Sepahan iliinyuka Mes Rafsanjan mabao 2-1.
Naft Masjed Soleyman nayo ililazimishwa sare tasa na Kheybar Khoramabad huku mipigo ya penati ikimalizika kwa ushindi wa mabao 4-3. Tractor Sazi waliambuliwa alama tatu za mezani baada ya Shahrdari Mahshahr kujiondoa kwenye mchuano huo. Kombe la Hazfi liliasisiwa mwaka 1975, huku The Esteqlal (Blues ya Tehran) ikiwa klabu iliyotwaa taji hilo mara nyingi zaidi, yaani mara saba, ikifuatiwa na Persepolis mara sita.

Iran yakosoa siasa chafu za AFC

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa vikali uamuzi wa Shirikisho la Soka Asia (AFC) wa kuinyima Jamhuri ya Kiislamu haki ya kuwa mwenyeji wa mechi za kufuzu Kombe la Dunia. Katika mkutano wake na mjini Tehran siku ya Jumapili na Waziri wa Michezo wa Iran, Masoud Soltanifar na Rais wa Shirikisho la Soka la Iran, Shahabeddin Azizi Khadem pamoja na Reza Salehi Amiri, Rais wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki ya Iran, Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema uamuzi huo wa AFC ni wa kisiasa, lakini hilo halitaitoa Tehran katika mkondo wa kuheshimu diplomasia ya spoti.

Nembo ya AFC

 

Amesema maafisa husika wa Iran watatumia njia zote za kisheria kuhakikisha kuwa uamuzi huo unaangaliwa upya. AFC imetangaza kuwa imeiteua Bahrain kuwa mwenyeji wa mechi zilizosalia za kusaka tiketi za kushiriki Kombe la Dunia litakalotifua mavumbi mwaka ujao 2022 nchini Qatar.

Iran yazoa medali Taekwondo na Karate

Makarateka wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamezoa medali mbili za dhahabu, moja ya fedha na shaba mbili katika mashindano ya Ligi Kuu ya Karate-1 yaliyofanyika mjini Istanbul, Uturuki. Katika mashindano hayo ya Jumapili, Muirani Sajad Ganzjadeh alimelemea Ryzvan Talibov wa Ukraine kwa alama 7-0 katika fainali ya Karate mtindo wa Kumite kwa upande wa wanaume wenye kilo zaidi ya 84. Dhahabu nyingine ya Iran ilitwaliwa na bingwa wa karate barani Asia, Zabiollah Poorshab baada ya raia wa Kazakhstan, Daniyar Yuldashev kujiondoa kwenye mpambano huo wa fainali kutokana na jeraha. Binti wa Kiirani, Rozita Alipour alitia kibindoni medali ya fedha baada ya kuibuka wa pili katika fainali ya Kumite kwa upande wa wanawake wenye kilo zisizozidi 61. Medali za fedha za Iran katika mashindano hayo ya kimataifa zilitwaliwa na Sara Bahmanyar na Aliasghar Asiabari. Mashindano ya kimataifa ya karate kama haya yalifanyika mara ya mwisho mwishoni mwa Februari hadi Machi Mosi mwaka jana 2020.

Makarateka wa kike wa Iran

 

Katika hatua nyingine, wanamichezo wa Iran wameshinda medali kochokocho katika Duru ya Nane ya Mashindano ya Wazi ya Taekwondo ya Uturuki. Ghazal Soltani alitwaa medali ya fedha wikend baada ya kuzidiwa na raia wa Morocco Oumaima El Bouchti katika fainali ya wanataekwondo wenye kilo chini ya 53. Nahid Kiani na Melika Mirhosseini walitwaa medali ya shaba kila mmoja katika michezo ya kutafuta mshindi wa tatu kwa wachezaji wenye kilo zisizozidi 57 67 kwa utaratibu huo. Katika siku ya ufunguzi wa mashindao hayo, Zahra Pouresmaeil aliipaisha Jamhuri ya Kiislamu kwa kutia kibindoni medali ya dhahabu baada ya kumtandika Mhispania Tania Castineira Etcheverria katika fainali ya wanataekwondo wenye kilo 73 na zaidi. Yalda Valinejhad na Parisa Jaavdi walitwaa medali fedha kila mmoja katika safu ya kilo zisizozidi 62.

  CAF yapata Rais mpya

Mmiliki wa klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Patrice Motsepe ndiye Rais mpya wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF). Bilionea huyo raia wa Afrika Kusini amechukua hatamu za uongozi wa CAF baada ya washindani wake wawili – Jacques Anouma wa Ivory Coast, Augustin Senghor wa Senegal kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho. Kadhalika Motsepe amechaguliwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Ijumaa hii kushika nafasi hiyo baada ya mgombea aliyetarajiwa kuweka upinzani mkubwa, Ahmad Yahya Ahmad kufungiwa kujihusisha na soka kwa miaka miwili, ikiwa ni punguzo la adhabu aliyopewa na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) ya miaka mitano. Punguzo hilo la adhabu lilifanywa na Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS) baada ya Ahmad kukata rufaa kupinga adhabu ya Fifa iliyotokana na kutiwa hatiani kwa makosa kadhaa yakiwemo ya kutumia madaraka vibaya na kujihusisha katika mkataba na kampuni ya vifaa vya michezo.

Nembo ya CAF

 

Dkt Motsepe ameeleza nia yake ya kutaka kubadili soka la Afrika kuwa la kiushindani zaidi na lenye faida katika bara hili. Amebainisha kuwa, "Nmefurahi. Kuna kazi kubwa ya ziada inatakiwa kufanywa ili hili litimie. Tunatakiwa kuhakikisha soka la Afrika sio la ushindani tu bali la mafanikio ya kimataifa. tunatakiwa kujenga bidhaa zetu ambazo zitakuwa bora na zenye kufanikiwa kuliko kuendelea kuwa tegemezi." Wakati huohuo, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallace Karia amejiondoa katika kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya ujumbe wa Baraza la Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA Council). Karia alikuwa akiwania nafasi hiyo, ambayo ingempa uwakilishi wa Nchi za Afrika zinazozungumza lugha ya Kingereza. Kwa mujibu wa taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)Karia amejiondoa baada ya kushauriana na viongozi wenzake wa Baraza la Vyama vya mpira wa miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA)ambapo yeye ni Rais kafanya hivyo ili awekeze nguvu TFF na Baraza hilo. "Kutokana na kumuunga mkono Patrice Motsepe wa Afrika Kusini ambaye ni Mgombea pekee wa Urais wa Shirikisho la Mpira wa miguu Afrika CAF nafasi ya Afrika kwa Nchi zinazozungumza kingereza inabaki moja,"imesema taarifa hiyo. Aidha kwa kuwa Rais mpya wa CAF, Motsepe ambaye anatoka Nchi inayozungumza Kingereza anakuwa moja kwa moja mjumbe wa FIFA Council ambapo Uchaguzi wa CAF uliofanyika Ijumaa jijini Rabat, Morocco.

Ligi ya EPL

Sergio Aguero alifunga bao lake la kwanza tangu Januari 2020 mnamo Jumamosi usiku na kusaidia waajiri wake Manchester City kusajili ushindi wa 3-0 dhidi ya Fulham uwanjani Craven Cottage. Ni ushindi uliowezesha masogora hao wa kocha Jurgen Klopp kufungua pengo la alama 17 kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) japo nambari mbili Manchester United ambao wana pointi 54 wangali na mechi mbili zaidi za kusakata ili kufikia idadi ya michuano ambayo imepigwa na Man-City. Huku ushindi wa Man-City ukiwafanya sasa kunusia taji la EPL, matumaini ya Fulham kusalia kwenye kampeni za kipute hicho msimu ujao yanazidi kudidimia. Baada ya kipindi cha kwanza kukamilika kwa sare tasa, Man-City walianza kampeni za kipindi cha pili kwa matao ya juu na wakafunguliwa ukurasa wa mabao na beki John Stones aliyekamilisha krosi ya Joao Cancelo katika dakika ya 47. Goli la pili la Man-City wanaotiwa makali na kocha Pep Guardiola, lilifumwa wavuni na Gabriel Jesus kunako dakika ya 56, kabla ya Aguero kufunga penalti dakika nne baadaye. Penalti hiyo ilichangiwa na tukio la Tosin Adarabioyo kumchezea vibaya kiungo Ferran Torres. Man-City wangalifunga mabao zaidi katika kipindi cha pili ila mafowadi wao wakashindwa kumzidi ujanja kipa Alphonse Areola aliyesalia imara katikati ya michuma. Kwengineko, baada ya kutoa kichapo cha mbwa mwizi cha mabao 5-0 dhidi ya vibonde Sheffield United, Leicester imefanikiwa kukaa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza na kuishusha Man United.

Arsenal

 

Leicester inakua imefikisha alama 56 baada ya kucheza mechi 29, ikiwa ni alama mbili tofauti na Man United ambayo ipo nafasi ya tatu ikiwa imecheza mechi 28. Leicester ilianza mauaji dakika ya 39 kwa bao la Kelechi Iheanacho aliyepokea pasi ya Jamie Vardy kabla ya Ayoze Perez kushindilia msumari wa pili dakika ya 64. Pasi kutoka kwa Vardy tena ikamkuta Iheanacho dakika ya 69 na akashindilia msumari wa tatu kabla ya kufunga bao la nne dakika ya 78 na kutimiza Hat trick yake kwenye mechi hiyo na bao la tano lilikuwa la kujifunga la Ethan Ampadu dakika ya 80. Kipigo hicho kimeendelea kuiweka kwenye hali mbaya Sheffield ambayo inaburuza mkia kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 14 pekee ilizokusanya katika mechi 29. Huku hayo yakiarifiwa, SAFARI ya kikosi cha Chelsea kutoka Jijini London hadi Leeds nchini England imegubikwa na majonzi makubwa baada ya kuambuliwa suluhu ya 0-0 dhidi ya vijana wa Marcelo Bielsa, kwenye muendelezo wa Ligi Kuu England uliopigwa leo Machi 13, 2021. Baada ya mchezo kocha wa Chelsea Thomas Tuchel amesema tatizo kubwa lililosababisha timu yake ipate matokeo hayo ni hali ya uwanja. Mbali na hayo, bao la dakika ya mwisho wa kipindi cha pili kutoka kwa Jamaal Lascelles lilisaidia Newcastle kuwalazimishia Aston Villa sare ya 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyochezewa uwanjani St James’ Park mnamo Ijumaa usiku. Matokeo hayo yaliwezesha Newcastle kuweka hai matumaini finyu ya kuepuka shoka la kuwateremsha ngazi kwenye kampeni za EPL msimu huu. Katika mchuano mwingine wa kuvutia, klabu ya Arsenal iliibamiza Tottenham mabao 2-1 wakati ambapo Southampton ilikuwa inanyukwa mabao 2-1 na Brighton.

…………………TAMATI…………….