Jan 03, 2023 09:17 UTC
  • Njia ya fikra ya Shahidi Qassem Soleimani: Mhimili wa Muqawama na Mapambano

Assalamu Alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo, na karibuni kuwa nasi tena katika mfululizo mwingine wa kipindi hiki maalumu tulichokuandalieni kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mwaka wa tatu wa kuuawa shahidi Luteni Jenerali Shahidi Qassem Soleimani, ambapo katika mfululizo huu wa tatu tutatalii moja ya vipindi maalumu vya maisha ya kamanda huyo.

Ni kipindi kilichoshuhudia mitikisiko na misukosuko mingi; kipindi ambacho kililivukisha jina la Luteni Jenerali Qassem Suleimani nje ya mipaka ya Iran. Kipindi hicho kilipelekea picha ya Kamanda Qassem Suleimani, kupamba kurasa za mbele za majarida ya Time na Newsweek, akitajwa kuwa shakhsia na mtu mwenye taathira kubwa katika matukio ya ukanda wa Asia Magharibi; na muhimu zaidi ya hilo, ni ushawishi wa kamanda huyo wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ndani ya nyoyo za makumi ya mamilioni ya watu waliokuwa wakimpenda, na si ndani ya Iran pekee, bali katika eneo zima. Endeleeni kuwa nami basi kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu.

Picha ya Shahidi Kamanda Qassem Soleimani katika ukurasa wa mbele wa Jarida la Newsweek

Kikosi cha Quds, ni tawi la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambacho kiliasisiwa mwaka 1988 kwa amri ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei na kujumuishwa kwenye vikosi vya jeshi hilo. Kwa miaka yote tokea kuasisiwa kwake baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, IRGC inayofahamika pia hapa nchini Iran kwa jina la mkato la Sepah, imekuwa na nafasi muhimu ya kuzuia hujuma za kijeshi na kiusalama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kikosi cha Quds kiliundwa kwa ilhamu ya fikra ya Imam Khomeini (MA), mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye alisema: "Leo Mashariki na Magharibi zinaelewa vyema kwamba, Uislamu ndio nguvu pekee inayoweza kuwapiku. Inawapasa viongozi watambue kuwa, mapinduzi yetu hayaishii kwenye mipaka ya Iran. Mapinduzi ya watu wa Iran ni nukta yanapoanzia mapinduzi makubwa ya Uimwengu wa Uislamu, ambayo bendera yake itabebwa na Mtukufu Imam Mahdi, roho zetu ni mhanga kwa ajili yake, ambaye ni fadhila ya Mwenyezi Mungu kwa Waislamu wote na walimwengu; na ajaalie kudhihiri kwake kuthibiti katika zama hizi". Kwa mujibu wa Imam Khomeini, kuthibiti kwa jambo hili kunahitaji uhamasishaji mkubwa wa jeshi la Uislamu duniani.

"Walinzi wa Haram" ni moja ya majimui zinazobainisha na kuakisi fikra na mtazamo huu. Kutokana na mtazamo wake wa kiulimwengu na kimataifa, Shahidi Kamanda Haj Qassem Soleimani, aliasisi vuguvugu la walinzi wa Haram kwa ajili ya kukabiliana na hatua za kinyama na kijinai za genge la kigaidi la DAESH (ISIS). Mbinu na taktiki alizotumia Kamanda Shahidi Soleimani katika kukabiliana na Daesh zilitokana na tajiriba na uzoefu wake na wanamapambano wenzake katika medani za mapambano ya miaka minane ya Vita vya Kujihami Kutakatifu vya uvamizi wa utawala wa Saddam dhidi ya ardhi ya Iran. Kwa mtazamo wake, tajiriba hiyo ya miaka minane kilikuwa kigezo mwafaka cha kutumiwa katika kuyatetea mataifa manyonge dhidi ya madhalimu. Kamanda Qassem Soleimani alikuwa akisema: "endapo taifa lolote litatendewa dhulma na kuandamwa na hujuma zisizo na mlingano, kama litataka kutetea heshima na sharafu yake na kujihami kutakolipa ushindi, mbinu ya ushindi ambayo imejaribiwa na kuthibiti ni hii ya Kujihami Kutakatifu". Katika kuthibitisha hoja yake hiyo, Jemedari huyo wa medani za Jihadi na mapambano alikuwa akigusia kujihami kwa watu wa mataifa ya ukanda huu kwa jina la Uislamu, ambao kutokana na kuyafanya mapambano ya taifa la Iran katika Vita vya Kujihami Kutakatifu kuwa ndio dira na kigezo chao, taathira chanya za kufanya hivyo wanazishuhudia hii leo katika jamii zao.

Matunda ya busara na uongozi wa Shahidi Haj Qassem Soleimani, yalikuwa ni kuasisi Mhimili wa Muqawama. Mhimili na kambi hiyo ilijumuisha makundi tofauti ya mapambano kama Hizbullah, Hashdu-Sha'abi, Fat'imiyyun, Zainabiyyun, Haidariyyun, Ansarullah n.k. Wapiganaji mbalimbali kutoka nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Iran, Iraq, Syria, Lebanon, Afghanistan na Pakistan, ambao wote walishajiika kwa lengo la kuilinda Haram ya Bibi Zainab (AS) na kwa ajili ya Uislamu, walifanikiwa kuusamabaratisha ugaidi wa Kidaesh, ulioasisiwa kwa msukumo na uungaji mkono wa baadhi ya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani kwa lengo la kuchafua jina na sura ya Uislamu na kumwaga damu za Waislamu; kiasi kwamba leo hii yamesalia mabaki machache ya genge hilo la kigaidi yanayoshuhudiwa katika nchi za Syria na Iraq ambazo zilidhamiriwa kuwa makao makuu ya utawala wake.

Katika chuo cha fikra na harakati cha Qassem Soleimani nguvu na uwezo unatokana na Mwenyezi Mungu pekee. Kamanda huyo alikuwa akiamini kwa dhati kwamba ahadi za Mwenyezi Mungu zitathibiti tu. Alivichukulia vitisho kuwa ni fursa, na akiitakidi kwamba fursa zinazopatikana ndani ya tumbo la vitisho hazipatikani katika hali na mazingira ya kawaida. Na ndio maana katika kadhia ya Syria, wakati duru za kisiasa na za vyombo vya habari duniani kikiwemo cha Aljazeera vilipokuwa vikizungumzia kukaribia kutekwa mji mkuu wa nchi hiyo Damascus, Shahidi Qassem Soleimani aliamini kwamba, kinyume na kilichoonekana mbele ya macho, inawezekana kuuvunjilia mbali mnyororo wa fitna na njama kubwa iliyokuwa imeratibiwa kwa pamoja na Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na tawala za Kiarabu za ukanda huu. Kamanda Qassem Soleimani alijitosa kwenye medani kwa lengo hilo na kubadilisha kurasa za historia, kiasi kwamba miaka minne baadaye, duru zilezile za kisiasa na za vyombo vya habari zilizungumzia kurejea uthabiti Syria na kukiri kwamba wapinzani wa kambi ya Muqawama wameshindwa.

Ushujaa wa kamanda huyo wa mhimili wa mapambano ulisimuliwa na marafiki na hata maadui zake. Bila shaka watu mashujaa duniani si wachache, lakini kitu kilichompambanua Shahidi Qassem Soleimani na kumfanya aendelee kukumbukwa, ni kuutumia ushujaa huo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na imani zake za dini. Kamanda huyo aliufikia ukingo wa mauti mara kadhaa, lakini kwa ushujaa na ujemadari wake wa hekima aliweza kila mara kuthibitisha ni kwa kiwango gani adui alikuwa duni na dhaifu.

Haukupita muda mrefu mara baada ya kuanza mgogoro wa ndani nchini Syria, mbegu ovu ya magenge ya kigaidi ya ukufurishaji yaliyoasisiwa katika nchi hiyo na kufika hadi ya kukalia asilimia 70 ya ardhi yake ilisambaa mpaka Iraq na kuukaribia mji mkuu wa nchi hiyo Baghdad ikiwa imeshabadilika na kuwa mti khabithi uliokamilika katika shina, mizizi na matawi yake. Hapo Kamanda Soleimani akapanua wigo wa utoaji msaada kwa vikosi vya wanamapambano kwa ajili ya kujihami. Ikapasa sasa kuchukua hatua haraka za kwenda kuwasaidia raia wa Iraq waliokuwa kwenye ukandamizi na dhulma za genge la Daesh. Alipokuwa akizungumzia sababu ya kuwepo kwake Iraq, Shahidi Qassem Soleimani alisema: "Tulipoingia kwa ajili ya kwenda kutoa ulinzi kwa wananchi wa Iraq, hatukuwahi hata mara moja kutafautisha kati ya maslahi ya Iran na Iraq. Tuliyachukulia maslahi ya watu wa Iraq kuwa ni maslahi yetu; tukasema, hawa washinde, wajikomboe na wajitawale; kwa hivyo msingi wa maslahi yetu sisi ni mambo hayo. Na huo ndio ukweli hasa wa sisi kuzisaidia Iraq na Syria na wala hatukuwa tukijitafutia fungu na manufaa ya namna yoyote ile".

Kwa hakika ilikuwa ni kama kwamba Qassem Soleimani alizaliwa ili kuja kutekeleza majukumu hatari na yenye mifadhaiko na misukosuko mingi na mikubwa. Nchini Iraq pia, Kamanda Qassem Soleimani alishiriki kikamilifu kwenye medani za operesheni muhimu zikiwemo za Amerli, Jurf Sakhar, Samarra, maeneo ya Fallujah na maeneo kadhaa ya al Anbar. Kwa mujibu wa Hadi al Ameri, kamanda wa Jeshi la Badr, DAESH ilikuwa ikiingiwa na woga kutokana na jina la Kamanda Soleimani. Alipohojiwa kuzungumzia maisha ya Shahidi Qassem Soleimani, Ameri alisema: "kama utatembelea mitandao ya habari ya Madaesh utaweza kufahamu ni kiwango gani wakufurishaji hao wanamuogopa mujahidina huyu shujaa".

Woga na kiwewe kilichowapata Daesh kutokana na kamanda huyo havikuwa na mfano. Masoud Barzani, kiongozi wa zamani wa eneo la Kurdistan ya Iraq amesimulia katika kitabu cha kumbukumbu zake kuhusu kipindi ambapo Daesh walikuwa pua na mdomo na Erbil, mji mkuu wa eneo hilo, ambapo kwa kuhofia kutekwa mji huo, yeye mwenyewe aliwasiliana na balozi za Marekani, Uturuki, Uingereza, Ufaransa na hata Saudi Arabia kwa ajili ya kuomba msaada, lakini si yeyote aliyekuwa tayari kutoa msaada. Barzani anasema, "mtu pekee aliyekuja kutusaidia alikuwa ni Haj Qassem Soleimani, akiwa ameandamana na wapiganaji wake maalumu 50. Alielekea haraka eneo la mapigano. Akavipanga vikosi na wapiganaji Peshmarga na kurudi baada ya masaa machache. Baadaye tulikuja kumkamata mateka kamanda mmoja wa Daesh, tukamuuliza, mlikuwa mnakaribia kuiteka Erbil, ilikuwaje mkarudi nyuma? Akasema: wanasaji wetu wa habari walitupa taarifa kwamba Qassem Soleimani yuko Erbil. Ari na motisha ya watu wetu ilivurugika, tukaamua kurudi nyuma".

Shahidi Qassem Soleimani akiwa Erbil, Kurdistan ya Iraq

Wapenzi wasikilizaji, Haj Qassem Soleimani hakuwahi kuwasahau katu wananchi madhulumu wa Palestina. Kwa msaada na uungaji mkono wake kwa wanamapambano wa Palestina, aliuingiza muqawama wa wananchi hao, wa kukabiliana na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kwenye awamu mpya ya mapambano. Aliuimarisha na kuutia nguvu zaidi muqawama wa eneo la Ukanda wa Gaza kwa kuuongezea nyenzo na suhula. Shahidi Qassem Soleimani hakutafautisha kati ya makundi ya muqawama ya Gaza, bali alitoa msaada kwa makundi yote ili yaweze kukabiliana na adui wao wa pamoja wa Kizayuni. Jina la Quds lilikuwa na nafasi kuu katika maisha ya kamanda huyo. Tariqul-Quds, ni jina la operesheni ya kwanza aliyoongoza Kamanda Shahidi Qassem Soleimani kupitia bataliani mbili wakati wa vita vya miaka minane vya Kujihami Kutakatifu. Baada ya vita, alikabidhiwa ukamanda wa kambi ya Quds iliyokuwa na jukumu la kupambana na maharamia katika mipaka ya mashariki mwa nchi. Mwaka 1998 aliteuliwa kuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Pengine ni kwa sababu hiyo, ndio maana kuna wengi wanaoamini kwamba, kikomboleo cha damu ya Haj Qassem Soleimani ni ukombozi wa Quds tukufu. Alaysa-ssubhu bi Qariib? Je mapambazuko ya kuthibiti ndoto hiyo si yanakaribia?  Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags