Jan 08, 2023 02:46 UTC
  • Tafakuri kuhusu kusitishwa uanachama wa Iran katika Kamati ya Hadhi ya Wanawake ya UN

Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nasi tena katika kipindi cha Makala ya Wiki ambacho leo kitatupia jicho hatua ya kusitishwa uanachama wa Iran katika Kamisheni ya Hadhi ya Wanawake ya UN.

Kwa miaka mingi tumeshuhudia juhudi za nchi za Magharibi za kuingilia kati masuala ya ndani ya nchi huru hususan Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Wakati huo huo, neno "haki za binadamu" limekuwa kisingizio cha muda mrefu kinachotumiwa na nchi hizo kama wenzo wa kuingilia mamlaka na masuala ya ndani ya nchi nyingine. Nchi za Magharibi zimekuwa na vigezo vya kinafiki na kindumakuwili hasa katika uwanja wa haki za binadamu, na zinafumbia macho unyanyasaji uliokithiru wa wanawake katika jamii za Magharibi. Tabia hii ya kinafiki na kindumakuwili ilidhihirika tena dhidi ya Iran Jumatano, Novemba 24, 2022. Mara hii tumeona maonyesho ya Marekani dhidi ya Iran kwa kisingizio cha kuwaunga mkono wanawake wa Iran katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Mkutano huo ulifanyika ili kusitisha uanachama wa Jamhuri ya Kislamu katika Kamisheni ya Hadhi ya Wanawake na hatimaye, kura ikapigwa. Kutokana na njama hiyo ya Marekani, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo imekuwa mwanachama wa Kamati ya Hadhi ya Wanawake ya Umoja wa Mataifa kupitia mchakato wa kidemokrasia na kwa kupata kura nyingi, imeondolewa kwenye kamati hiyo.***

Mkutano wa Marekani dhidi ya Iran wa kuiondoa Iran katika Kamati ya UN kuhusu Hadhi ya Wanawake 

Kwanza kabisa, inatupasa kujibu swali kwamba, Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hadhi ya Wanawake ni nini, na ina uwezo kiasi gani wa kiutendaji?

"Kamisheni ya Hadhi ya Wanawake" ni taasisi iliyo chini ya Baraza la Masuala ya Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa (ECOSOC), ambayo tangu mwaka 1946 imekuwa ikijaribu kutatua changamoto na matatizo ya wanawake. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipewa uanachama katika kamati hiyo kwa njia ya uwazi na kupitia chaguzi za kidemokrasia na kwa kuungwa mkono na kundi la Asia na Pasifiki, na ilipata kura za wanachama wengi wa ECOSOC.

Kwa sasa Baraza la Masuala ya Uchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa, ECOSOC, lina wanachama 54 na ni moja ya mihimili sita ya Umoja wa Mataifa, ambayo ina jukumu la kushughulikia masuala ya kijamii na kiuchumi na masuala kitaalamu ya Umoja wa Mataifa. 

Kamisheni ya Hadhi ya Wanawake ya Umoja wa Mataifa pia ina wajumbe 45, na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipewa uanachama katika kamati hiyo kwa kupata kura nyingi za wajumbe wa ECOSOC, yaani kura 43 kati ya kura 54 za wajumbe wa chombo hicho. Jambo la kuzingatia ni kwamba Kamisheni ya Hadhi ya Wanawake haina jukumu la kufanya maamuzi au dhamana ya utendaji, lakini kwa mujibu wa baadhi ya wanaharakati wa haki za wanawake, kamisheni hii inahesabiwa kuwa msimamizi muhimu katika uwanja wa masuala ya wanawake katika Umoja wa Mataifa. 

Mpango wa kuiondoa Iran katika Kamisheni ya Hadhi ya Wanawake ya Umoja wa Mataifa unadhihirisha hatua ya uhasama na ya matashi ya kisiasa ya Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi kwa kisingizio cha kuwaunga mkono wanawake wa Iran na umeibua maswali mengi ya kujiuliza kwa wajumbe wengi wa ECOSOC. Hii ni kwa sababu Marekani na baadhi ya wanachama wengine, ambao ni wakiukaji wakubwa wa haki za binadamu, wamefanya njama ya kuitenga nchi huru na inayojitawala kutoka kwenye Kamisheni ya Hadhi ya Wanawake, suala ambalo ni kinyume cha sheria ECOSOC. 

Miongoni mwa maoni yaliyopewa mazingatio katika Umoja wa Mataifa wakati wa kikao cha kabla ya kupigwa kura kuhusu kadhia hiyo ni yale yaliyotolewa na mwakilishi wa Russia katika taasisi hiyo ya kimataifa. Akipinga hoja ya kuondolewa Iran katika Kamisheni ya Wanawake ya UN, mwakilishi wa Russia aliuliza: "Je, mmesoma ufafanuzi wa hati ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na suala hili? Wenzetu wa Magharibi wamezoea kuharibu miundo na sheria za kimataifa." Ameongeza kuwa: "Sikuwahi kuona Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa likiitisha kikao cha kujadili kukandamizwa kwa mandamano ya amani nchini Ufaransa na Uingereza; au kufanya mkutano kama huo baada ya mauaji ya George Floyd huko Marekani." Mwakilishi huyo wa Russia amesema kinyume chake uchunguzi wa kina na kamili umefanywa nchini Iran kuhusiana na kifo cha Mahsa Amini na kubainika kuwa aliaga dunia kutokana na matatizo yake ya kiafya ya hapo awali. ***

Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya wanasheria wa kimataifa, upigaji kura wa kuiondoa nchi yoyote kwenye kamisheni ya kimataifa kimsingi ni jambo ambalo halijawahi kutokea, na kuondolewa kwa nchi kutoka kwenye Kamisheni ya Wanawake ya Umoja wa Mataifa ni uzushi utakaokuwa na matokeo mabaya ya kisheria kwa wanachama wengine. Kuhusiana na hilo mwakilishi wa Pakistan katika Umoja wa Mataifa amekumbusha kuwa, hakuna sheria ya kuwafukuza wanachama kwenye kamati hiyo. Amesisitzia kuwa: Uanachama wa Iran ulipigiwa kura na wajumbe wa baraza hilo mwaka 2021 kwa ajili ya kipindi cha miaka minne, na uanachama huo haupaswi kusitishwa kwa sasa kabla ya muda wake kumalizika. 

Hapa kunajitokeza swali kwamba, nchi zilizopelekea kuondolewa Iran katika Kamisheni ya Hadhi ya Wanawake, zinawaunga mkono wanawake kwa kiasi gani na je, kweli zinaheshimu haki za wanawake au la?***

Je kuhusu madai ya Marekani kuhusiana na ukiukwaji wa haki za wanawake katika jamii za Kiislamu, tovuti ya habari ya "Sandvision" imeandika kuwa: "Kila mwaka, zaidi ya wanawake na wasichana laki tano wenye umri wa zaidi ya miaka 12 wanabakwa nchini Inasikitisha kwamba, licha ya kuwepo kwa mashirika na taasisi za kimaanyesho tu za kimataifa, ripoti zilizochapishwa katika uwanja huu zinaonyesha kuwa Marekani ina hali mbaya katika suala la kuheshimu haki za wanawake. Kwa mfano tu katika ripoti yake iliyokeMarekani, na idadi hiyo ya vitendo vingine vya ukatili dhidi ya kundi hili la jamii ni zaidi ya kesi milioni 3.8. Vilevile asilimia 20 hadi 30 ya wanawake wanaoenda kwenye idara ya dharura ya hospitali huwa na alama za kupigwa kwenye miili yao."

Hivi karibuni pia "Tara Reade" alifichua ufisadi wa kimaadili wa Rais wa Marekani  Joe Biden katika studio ya Fox News wakati alipokuwa mjumbe wa Seneti ya Marekani.   ***

Gazeti la Washington Post pia linaripoti kwamba tangu 2015, karibu wanawake 250 wamepigwa risasi na polisi wa Marekani mitaani na kuuawa bila kesi. Leona Hale, mama mjamzito aliyekuwa na umri wa miaka 26, ni miongoni mwa waliouawa kwa kupigwa risasi na polisi wa Marekani. ***

Katika uwanja huu, kuna ushahidi mwingi wa ukiukwajii wa haki za binadamu huko Ulaya. Kulingana na ripoti ya 2019 ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa, mwaka 2020, wanawake 102 na mwaka 2019 wanawake 146 waliuawa katika ukatili ulioshuhudiwa kati ya wanandoa huko Ufaransa. Kati ya 2020 na 2021, unyanyasaji wa majumbani nchini Ufaransa uliongezeka kwa asilimia 21. Ripoti iliyochapishwa na Taasisi ya Taifa ya Takwimu ya Ufaransa mwaka 2016 ilionesha kuwa, ukatili wa kingono huathiri wanawake 600,000 nchini Ufaransa kila mwaka. Hapana shaka yoyote kwamba hivi sasa takwimu hizi zimeongezeka sana ikilinganishwa na mwaka huo wa 2016.

 

Nchini Ujerumani, takwimu zinazotolewa na polisi wa kukabiliana na uhalifu zinaonesha kuwa, unyanyasaji wa nyumbani husababisha kifo cha mwanamke mmoja kila baada ya siku tatu. Mnamo mwaka wa 2018 pekee, wanawake 122 walipoteza maisha yao nchini humo kutokana na unyanyasaji wa nyumbani.

Huko Uingereza, ripoti zinaonyesha kuwa wanawake 139 waliuawa na jamaa zao wa kiume katika nchi hiyo mnamo 2017, na mbili ya tano kati yao walifariki dunia kutokana na ukatili uliokithiri na kupita kiasi.

Kukithiri kwa ukatili huo kuliilazimisha serikali ya Uingereza kutenga pauni milioni 100 kati ya 2016 na 2020 kwa ajili ya huduma zinazohusiana na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.   ***

Ili kuelewa vyema tabia na mienendo ya kinafiki ya nchi za Magharibi hususan Marekani kuhusiana na suala la haki za wanawake, tunaweza kuashiria nchi nyingine kakdhaa, ikiwemo Saudi Arabia, ambazo zina mtazamo hasi kabisa na wa kibaguzi dhidi ya wanawake. Hata hivyo, Marekani haichukua hatua yoyote ya kusitisha uanachama wa Riyadh katika Kamisheni ya Hadhi ya Wanawake ya UN. Mbali na kukandamiza wanawake nchini Saudi Arabia, Aal Saud wanaendelea kufanya mauaji ya kinyama dhidi ya wanawake na watoto wa Yemen kwa miaka kadhaa sasa tena kwa himaya na uungaji mkono na silaha za nchi za Magharibi hususan Marekani na Uingereza. Waziri wa Afya wa Yemen, Taha Al-Mutawakkil anasema: "Muungano vamizi wa Saudi-Marekani umeua watoto na wanawake elfu 8 wa Yemeni katika kipindi cha miaka minane iliyopita."

Katika upande mwingine, taasisi mbalimbali eti za kutetea haki za binaadamu kama Umoja wa Mataifa hadi sasa hazijachukua misimamo mikali ya kuzuia jinai na uhalifu mwingi unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wanawake na watoto katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina. Utawala huo umeua shahidi maelfu ya wanawake wa Kipalestina na watoto zaidi ya 2,500 katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.  ***

Bila shaka unyanyasaji dhidi ya wanawake mahala popote pale ni jambo baya na la kulaaniwa, na kila mtu ana wajibu wa kuzuia na kukabiliana nao; hata hivyo nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, kutokana mienendo yao ya kinafiki, zimeendelea kunyoosha kidole cha lawama kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na zinatumia suala hilo kama kisingizio cha kuingilia mambo ya ndani ya nchi hii. Hii ni licha ya kwamba, miongoni mwa mafanikio muhimu zaidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuwapa utambulisho wanawake ambao wameweza kung'ara katika nyuga mbalimbali za kisiasa, kijamii, kiutamaduni na kimichezo kwa kutegemea nafasi na uwezo wao. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ikiwa ni nchi ya Kiislamu, inaheshimu nafasi ya mwanamke na kinyume na nchi za Magharibi zinazomfanya aonekane kama kielelezo cha hisia za kingono, inalenga kutumia talanta na uwezo mkubwa wa kifikra wa wanawake kwa ajili ya kuenyanyua juu zaidi nafasi yake na jamii kadri inavyowezekana.

Mtazamo wa haraka wa machapisho na vitabu vingi vinavyochapishwa hapa nchini kwa majina ya wanawake, vikiwemo vya taaluma za kisayansi, utafiti, historia, fasihi, siasa na kadhalika, unaonyesha nafasi ya juu ya kielimu na kisayansi ya wanawake wa Iran. Uwezo na shughuli za wanawake wa Kiirani katika nyuga za tiba, sayansi na teknolojia pia ni jambo la kupewa mazingatio makubwa, na wanawake wamekuwa na taathira kubwa za maendeleo hapa nchini katika nyuga zinazohusiana na sayansi za kisasa.

Ni kwa kutilia maanani haya yote ndiyo maana Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei anasema: “Sisi ndio tunaopaswa kutoa madai ya kutetea haki za wanawake na nchi za Magharibi. Wao ndio wanaowadhulumu na kuwakandamizia wanawake, wanawadhalilisha wanawake na kuwashushia hadhi yao. Wanawashinikiza kiakili, kisaikolojia, kihisia na kudhalilisha utu na heshima yao kwa kutumia jina la uhuru, kwa jina la ajira, kwa madai ya kuwapa majukumu. Hivyo Wamagharibi wanapaswa kuwajibishwa."