Feb 09, 2023 10:54 UTC
  • Picha halisi ya sura ya familia ya kifalme ya Uingereza katika kitabu

Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nasi tena katika kipindi hiki cha Makala ya Wiki ambacho leo kitatupia jicho sura ya familia ya kifalme ya Uingereza katika kitabu cha Spare.

Kitabu cha kumbukumbu cha Prince Harry - Mwana wa Mfalme wa Uingereza - kilichopewa jina la "Spare" ambacho kilichachapishwa hivi karibuni kina simulizi za siri kuhusu maisha yake na watu wa familia ya kifalme ya Uingereza. Kitabu hiki kinafichua mengi na picha ya sura halisi ya ubaguzi, ria, ukatili na uhasama unaojiri ndani ya familia hiyo. 

Katika kampeni ndefu ya kujionyesha kama muathiriwa wa wakosoaji, vyombo vya habari vya Uingereza na familia ya kifalme, Prince Harry na mkewe Meghan, wamefichua siri zao katika vipindi vingi vya televisheni na mahojiano katika  miaka miwili iliyopita. Sasa ni zamu ya kumbukumbu za wanachama hawa wa familia ya kifalme, ambao katika wiki chache zilizopita wametoa maelezo mengi kwenye vyombo vya habari kuhusu yaliyomo.

Kitabu cha kumbukumbu "Spare", ni tawasifu ya "Henry Charles Albert David" anayejulikana kama Prince Harry, mtoto wa mwisho wa Mfalme wa sasa wa Uingereza, ambacho kilichapishwa katika siku za mwanzo za mwaka huu. Riwaya hiyo inayoibua changamoto nyingi, ambayo imepewa jina la "Kipuri" au "kitu cha ziada", ilikuwa mada na gumzo katika vyombo vya habari wiki chache kabla ya kutolewa rasmi. Ni wazi kwamba kitabu hili kimejaa ufunuo na kashfa nyingi za kushtua, na inaonekana kuwa Prince Hary hakufanya ubakhili katika kueleza tajiriba na uzoefu wake yeye na mke wake kama wanachama wa familia ya kifalme. Katika kitabu hiki pia, amemshambulia vikali kaka yake -Mwanamfalme William ambaye ni mrithi wa sasa wa taji ya ufalme wa Uingereza - na kumtaja kuwa ni "adui mkuu". Pia amewashutumu wanafamilia ya kifalme na watumishi wa kasri kuwa wabaguzi wa rangi.  *****

Prince Harry 

Kauli za Prince Harry katika kitabu cha "Spare" kuhusu kaka, baba yake na mke wa baba yake ni za kijasiri sana na zinafichua wazi sura zao za nyuma ya pazia na njama zinazofanyika katika kasri la Mfalme kwa ajili ya kudumisha mamlaka na kuvihadaa vyombo vya habari na wananchi kwa kughushi au kupindua ukweli. Harry amemshutumu Camilla, malikia na mke wa Mfalme Charles - "Queen Consort" - kuwa amevujisha habari za ndani ya kasri kwa waandishi wa habari, akidai kwamba alianzisha kampeni ya kuolewa na Charles ili kushinda taji la kimalkia. Mwanamfalme Harry anadai kuwa, Kate na William (kaka na shemeji yake) walimhimiza kuvaa taji hilo la malkia.

Katika kitabu hicho, Prince Harry anaangazia mapigano makali baina yake na kaka yake mkubwa, William, na kuzungumzia masuala mengine kama vile jinsi mama yake, Princess Diana alivyouawa, kashfa za ujanani mwake, uraibu wa mihadarati na mambo mengine mengi, ambayo kila moja linaweza kuharibu sifa ya familia ya kifalme ya Uingereza. Catherine Mayer, mwandishi wa wasifu wa Mfalme Charles ameonya kuhusu hatua hiyo ya Mwanamfalme Harry na kusema: Hasira dhidi ya ubaguzi wa rangi, vita dhidi ya wanawake na masuala yanayohusiana na utajiri katika familia ya kifalme vinaweza kuharibu imani ya umma kwa familia hiyo. *****

Mwendazake, Princess Diana 

Kabla ya kutolewa kwa kitabu hicho, katika sehemu za kumbukumbu zake zilizoshirikiwa na ITV, Harry alidokeza kuhusu jinsi hitilafu katika familia yake zilivyochochewa na Buckingham Palace (makazi ya Mfalme wa Uingereza mjini London) na vyombo vya habari vinavyodhibitiwa na ofisi ya mfalme. Kuhusu suala hili anasema: "Hatuzungumzii tu uhusiano wa kifamilia, tunazungumza juu ya mshindani, ambaye ni vyombo vya habari vya Uingereza, haswa magazeti ambayo yanataka kuibua migogoro mingi kadiri inavyowezekana. Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba, baadhi ya wanafamilia yangu na watu wanaowafanyia kazi wanahusika katika mzozo huu. Uvujishaji wa habari kwenye vyombo vya habari hauhusiani na mtu asiyejulikana; Ni Kasri ambayo huwatonya waandishi wa kisha kuficha nyayo zake.."

Pia amezungumzia jinsi mama yake alivyokuwa akisumbuliwa na mapaparazi na wapiga picha ambao kazi yao ni kuchukua picha zenye utata za watu maarufu, na vilevile akakumbusha usiku ambao baba yake alimwambia kwamba Princess Diana amefariki dunia kutokana na majeraha aliyopata katika ajali ya gari.

Anwani ya kitabu yaani "Spare" inaonyesha nafasi ya Harry na zamu yake kwenye silisila ya uongozi wa kiti cha ufalme cha Uingereza. Katika mlolongo huu, kaka yake mkubwa, William yuko mbele yake, na Harry mwenyewe ni chaguo linalofuata au mchezaji wa benchi na kipuri. 

Mistari ya kwanza ya kitabu "Spare" inaanza kwa kusimUlia mivutano ya ndani ya familia ya kifalme ya Uingereza, na mada yake kuu ni malalamiko ya Prince Harry kuhusu hitilafu za kina za kifamilia; mateso aliyopata kutokana na mienendo ya kindumakuwili aliyokabiliana nayo ikilinganishwa na kaka yake mkubwa, vikwazo alivyowekewa vilivyosababishwa na mtindo wa maisha ya familia ya kifalme na usumbufu wa mara kwa mara wa vyombo vya habari, ambavyo vinafuatilia nyendo zake zote.  *****

Kitabu "Spare" kimegawanywa katika sehemu tatu na sehemu yake ya pili inagusia jinsi alivyoshiriki katika kikosi cha jeshi la Uingereza kwenye vita nchini Afghanistan.

Mnamo 2007, Harry na makamanda wa jeshi la Uingereza waliamua kumtuma Iraqi kwa kazi za kijeshi. Baada ya suala hilo kufichuliwa hadharani kwenye vyombo vya habari, serikali na familia ya kifalme waling'amua kuwa ushiriki wa Harry katika vita kama hivyo haungekuwa na matokeo mazuri kwa sifa yake na hata maisha yake, na kwa sababu hiyo, walighairi kumpeleka Iraqi. Baada ya muda, ilipendekezwa aende Afghanistan, na mwishoni mwa 2007, Harry aliondoka nchini Uingereza na kwenda Afghanistan. Wakati huo, idadi ya askari wa Uingereza nchini Afghanistan ilikuwa karibu watu 7,000, na inaonekana hakuwa na jukumu la moja kwa moja katika vita na alitumia redio na ufuatiliaji kwenye ukurasa wa kumputa kuruhusu ndege kutua na kupaa. Baada ya muda, alichoshwa na kazi hiyo aliyokuwa amepewa na anafikiria kuwa na jukumu kubwa zaidi katika vita. Hivyo aliomba kupelekwa katikati ya vita, eneo la Garmsir.

Katika kitabu hiki tunasoma kwamba, katika utekelezaji wa operesheni za vita, Harry alitofautiana na Wamarekani. Alitaka litumike bomu la pauni 2,000, wakati Wamarekani walisema kwamba mabomu mawili ya pauni 500 yanatosha. Mwishowe, mabomu hayo yalitumiwa na Waafghani wengi wakauawa. Huwenda utapenda kujua kwamba baada ya tukio hili, Harry alifurahia kutazama nyota angavu katika anga ya Musa Qala katika mkoa wa Helmand na kunywa chokoleti ya moto!

Alipopelekwa kwa mara ya pili nchini Afghanistan kwa jukumu la kijeshi, na kuwasili katika kambi ya kijeshi huko Helmand alikokuwa miaka minne iliyopita, Harry anasema alijihisi "kurejea nyumbani". Harry anakiri kwamba aliua watu 25 wakati wa majukumu yake huko Afghanistan, na anaendelea kueleza kuwa: Wakati wa vita hivyo, sikufikiria juu ya watu hao 25. Kwa sababu ukiwatambua kuwa ni binadamu, huwezi kuwaua… Walikuwa vipande vya chesi vilivyoondolewa kwenye sataranji. Ubaya lazima uondolewe kabla ya kuua wema….

Tunakukumbusha kwamba katika kitabu chote cha Spare, ni mara chache sana ambapo Prince Harry amezungumzia au kuandika chochote kuhusu watu wa Afghanistan, hasa madhara yaliyowapata wananchi wa nchi hiyo kutokana na vita na hujuma za nchi za Magharibi.  *****

Uchapishaji wa kitabu "Spare" umezusha gumzo na zogo kubwa - katika  vyombo vya habari - ambayo, bila shaka, itakuwa na taathira mbaya sana nchini Uingereza. Baada ya jina la kitabu cha Harry kufichuliwa, mwandishi wa habari wa Kiingereza, mtayarishaji na mtangazaji wa runinga, Piers Morgan alimtaja Harry kuwa mtu abusi, mbinafsi na mwenye pupa" na kusema kwamba Mfalme Charles anapaswa kumpokonya "mtoto huyu muovu na mnafiki" vyeo na nyadhifa zote za kifalme.

Andrew Walker, mtangazaji na mmsanii wa vichekesho, aliamua kurarua kitabu hicho cha Prince Harry katika mkanda wa video uliorushwa hewani katika mitandao ya kijamii.

Hata hivyo huko Marekani, watu wamekaribisha vizuri kitabu hicho. Mtangazaji wa runinga Stephanie Soteriou alisema: Uwezo ya Prince Harry katika kuchagua jina yaani "Ziada au Kipuri" kwa ajili ya kumbukumbu yake ni jambo la kusifiwa na kupongezwa.

Kitabu hicho cha kumbukumbu za Mwanamfalme Harry kimetayarishwa na mwandishi wa Marekani aliyeshinda Tuzo ya Pulitzer J. R. Moehringer. Inaripotiwa kuwa Spare ni miongoni mwa vitabu vinavyonunuliwa sana kwa sasa.

Inatupasa kuongeza kuwa kitabu hiki ni mkusanyiko wa maoni makali zaidi ambayo hayaonyeshi ishara ya kutaka kuwepo suluhu kati ya mwanachama huyu wa familia ya kifalme ya Uingereza na wanachama wengine. Kwa hakika, tunaweza kukitambua kuwa ni picha inayokaribia zaidi kwenye ukweli ya familia ambayo inajiona kuwa na damu bora zaidi na ya kiungwana (aristocratic), inayoshikilia madaraka ya nchi na inaendelea kupora utajiri wa mataifa mengine na kuibua vita duniani.