Jumamosi, 19 Agosti, 2023
Leo ni Jumamosi tarehe Pili Mfunguo Tano Safar 1445 Hiijria sawa na tarehe 19 Agosti 2023 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1324 iliyopita, aliuawa shahidi Zaid bin Ali bin Hussein mwana wa Imam Sajjad (as) na mjukuu wa Mtume Muhammad (saw). Zaid bin Ali alisimama kupambana na dhulma za Bani Umayyah na kulinda matunda ya mapambano ya babu yake, Imam Hussein bin Ali (as). Baada ya mapambano ya kishujaa, Zaid bin Ali aliuawa shahidi katika mji wa Kufa nchini Iraq. Harakati ya mapambano ya Zaid ni miongoni mwa matunda ya mapambano ya Imam Hussein (as) katika medani ya Karbala mwaka 61 Hijria, kwani baada ya mapambano ya siku ya Ashura kulijitokeza harakati nyingi baina ya Waislamu zilizopigana jihadi kwa lengo la kuuondoa madarakani utawala dhalimu wa Bani Umayyah. ***

Katika siku kama yale leo miaka 1175 iliyopita, sawa na tarehe Pili Safar mwaka 270 Hijiria, harakati ya mapambano za Wazanji ilifeli baada ya kuuawa kiongozi wa harakati hiyo Sahib al-Zanj. Ali Bin Muhammad maarufu kwa jina la Sahib al-Zanj ambaye alikuwa akijitambua kuwa mmoja wa wajukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) na Imam Ali bin Abi Twalib (as) alianzisha harakati ya mapambano mwaka 255 Hijiria akisaidiwa na wafuasi wake pamoja na watumwa weusi ambao walikuwa wakiitwa Wazanji, dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Bani Abbas huko kusini mwa Iraq. Sahib al-Zanj aliwaahidi watumwa hao weusi kuwaachilia huru kutoka katika minyororo ya utumwa na kuwapa haki zao za kijamii kama watu wengine suala ambalo liliwafanya watu wa jamii hiyo kuvutiwa na harakati yake. Mwaka 257 Sahib al-Zanj aliudhibiti mji muhimu wa Basra, Iraq na taratibu akaanza kutwaa maeneo mengine ya karibu na mji huo. Katika kipindi hicho majeshi ya utawala wa Bani Abbasi yalifanya hujuma kadhaa dhidi ya Wazanji lakini hata hivyo hujuma hizo zilifeli kutokana na msimamo imara wa jamii ya watu hao weusi. Hata hivyo kutokana na matatizo ya ndani Wazanji walidhoofika sana na harakati yao iliyoendelea kwa kipindi cha miaka 15 ikasambaratika baada ya kuuawa kiongozi wao Sahib al-Zanj. ***
Miaka 700 iliiyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia nchini Misri, Abu Hayyan Gharnati, malenga na mtaalamu wa fasihi wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 654 Hijiria huko Andalusia 'Uhispania ya leo' na baadaye alifanya safari katika miji mbalimbali kwa ajili ya kutafuta elimu. Mwaka 679 Abu Hayyan Gharnati, alielekea nchini Misri ambako aliishi hadi mwisho wa maisha yake. Akiwa nchini humo alijishughulisha na ufundisha na kuandika vitabu. Gharnati alikuwa mtaalamu wa elimu ya Qur'ani, Hadithi na sharia za Kiislamu, lakini alipata umashuhuri mkubwa katika utaalamu fasihi ya lugha ya Kiarabu. Abu Hayyan Gharnati ambaye mwishoni mwa uhai wake alikuwa kipofu, ameacha turathi nyingi kama kitabu cha 'Al-Idraaku Lilisaanil-Atraak' 'Tadhkiratun-Nuhaat' 'Tafsirul-Bahril-Muhit' na diwani ya mashairi. ***

Siku kama ya leo miaka 361 iliyopita, alifariki dunia Blaise Pascal, mwandishi, mwanahisabati na mvumbuzi wa calculator au kikokotoo wa Kifaransa. Alizaliwa Juni mwaka 1623 na tangu utotoni Pascal alivutiwa mno na somo la hisabati. Vilevile urafiki wa baba yake Pascal na msomi mmoja maarufu wa zama hizo ulisaidia mno katika kuchanua kipawa na kugunduliwa uwezo wa kijana huyo katika taaluma ya hisabati. Mwishoni mwa umri wake Blaise Pascal alijielekeza mno katika masuala ya dini na kuandika vitabu kadhaa katika uwanja huo. ***
Katika siku kama hii ya leo miaka 204 iliyopita aliaga dunia mvumbuzi na mhandisi wa Kiingereza James Watt. Msomi huyo alipendelea na kuvutiwa mno na utafiti kuhusu masuala ya kisayansi. Katika utafiti wake Watt alifanikiwa kuvumbua nishati ya mvuke na kuzusha mapinduzi makubwa katika sekta ya viwanda hususan usafirishaji wa nchi kavu na baharini. ***
Miaka 45 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 28 Mordad 1357, Hijria Shamsia, vibaraka wa utawala wa Shah walifanya maafa ya kutisha ya kuchoma moto jumba la sinema la Rex katika mji wa Abadan kusini mwa Iran. Katika tukio hilo la kinyama watu wasio na hatia 377 wakiwemo watoto na wanawake walipoteza maisha yao. Jinai hiyo ilifanywa na maajenti wa Shirika la Kiintelijensia na Usalama wa Taifa la Iran (SAVAK) na vibaraka wa utawala wa Shah. Watu karibu 700 waliokuwa wakitazama sinema katika jumba hilo walifungiwa ndani baada ya moto kuzuka na mamia miongoni mwao wakateketea. Tukio hilo lilizusha hasira kubwa baina ya wananchi. Utawala wa Shah ulifanya maafa hayo na kisha kuwatuhumu wanamapinduzi kuwa ndio waliotekeleza shambulizi hilo la kutisha kwa shabaha ya kuchafua sura la harakati za Mapinduzi ya Kiislamu mbele ya wananchi. Hata hivyo njama hizo za Shah zilifeli. ***
Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita alifariki dunia Dakta Azar Andami mwanafizikia, mhakiki na mtaalamu mahiri wa bakteria wa Kiirani. Alizaliwa katika eneo la Rasht katika mkoa wa Gilan huko kaskazini mwa Iran. Alikuwa na kipaji kikubwa cha masomo. Azar Andami alihitimu masomo ya PhD katika Chuo Kikuu cha Tehran. ***
Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, makamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Urusi ya zamani wakiongozwa na Gennady Ivanovich Yanayev walifanya mapinduzi dhidi ya rais wa mwisho wa Muungano wa Sovieti, Mikhail Gorbachev. Wanajeshi hao walitaka kukomeshwa marekebisho ya Gorbachev na kuzuia mpango wa kugawanywa Urusi ya zamani. Wakati wa mapinduzi hayo Mikhail Gorbachev alikuwa katika Peninsula ya Crimea huko kaskazni mwa Bahari Nyeusi. Hata hivyo Boris Yeltsin ambaye wakati huo alikuwa kiongozi wa Federesheni ya Urusi na ambaye alikuwa akiungwa mkono na Magharibi, alizima mapinduzi hayo kwa msaada wa wananchi na baadhi ya watu wenye ushawishi serikalini. Kushindwa kwa mapinduzi hayo kulizidisha uwezo na satua ya Boris Yeltsin na kuharakisha mwenendo wa kusambaratika Urusi ya zamani hapo mwaka 1991. ***
Katika siku kama ya leo miaka 3 iiliyopita, aliaga dunia Ayatullah Muhammad Ali Taskhiri, Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu. Ayatullah Taskhiri alizaliwa Najaf Iraq mwaka 1323 Hijria Shamsia. Kwa miaka mingi alikuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu iliyoundwa na Ayatullah Khamenei, Kiiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya kueneza umoja katika ulimwengu wa Kiislamu. Ayatullah Taskhiri kutokana na kubobea katika elimu na kuzifahamu vyema lugha za Kiarabu na Kiingereza aliweza kuwa na nafasi muhimu katika uga wa kueneza umoja miongoni mwa Waislamu. Ayatullaha Taskhiri hakuwa nyuma pia katika uwanja wa uandishi wa vitabu na baadhi ya vitabu vyake ni "al-Mukhtasar al-Mufid fi Tafsir al-Qur'an al-Majid", Aqaliyat'hay Mosalman; Rahkarha va Moshkelat na Eidahaye Goftegu Ba Digaran. Ayatullah Taskhir aliaga dunia katika siku kama ya leo kwa mshtuko wa moyo akiwa na umri wa miaka 75. ***