Jumatano, Agosti 23, 2023
Leo Jumatano tarehe 6 Safar mwaka 1445 Hijria, sawa na Agosti 23 mwaka 2023.
Siku kama ya leo, miaka 79 iliyopia mji wa Paris ulikombolewa kutoka kwenye uvamizi wa Ujerumani. Miezi 15 baada ya kushtadi moto wa Vita vya Pili vya Dunia na katika kuendeleza njama zake za kutaka kujitanua, dikteta Adolph Hitler aliyaamuru majeshi ya nchi hiyo kuushambulia mji wa Paris kwa lengo la kutaka kuudhibiti mji huo. Tarehe tano Juni mwaka 1940, Hitler alitoa amri ya kuharibiwa kikamilifu muundo wa majeshi ya Ufaransa na siku tatu baadaye yaani tarehe nane Juni mwaka 1940, vikosi vya Wanazi vilikishinda kikosi cha ulinzi cha Ufaransa katika eneo la kaskazini mashariki mwa taifa hilo, na hivyo kutoa mwanya kwa jeshi la Ujerumani kuingia nchini Ufaransa.

Miaka 25 iliyopita katika siku hii sawa na ya kwanza ya Shahrivar mwaka 1377 Hijria Shamsia:
Mpiganaji wa mapinduzi na mmoja wa wanachama wakuu wa Chama cha Muungano wa Kiislamu "Sayyid Asadollah Lajevardi" aliuawa shahidi na kundi la munafiqin. Sayyid Asadollah Lajevardi alizaliwa mjini Tehran mwaka 1314 Hijria. Akiwa kijana, aliacha shule ya upili na kuanza kufanya kazi na baba yake. Baadaye, alijiunga na chuo cha kidini. Kuanzia mwanzo wa harakati ya Kiislamu ya wananchi wa Iran chini ya uongozi wa Imam Khomeini, Shahidi Lajevardi naye alijiunga na mwenendo huo na akawa na nafasi muhimu katika kuanzishwa kwa jumuiya za muungano wa Kiislamu mwaka 1341. Pamoja na mashahidi Beheshti na Motahari, aliamua kuunda muungano dhidi ya serikali na alifanya jitihada kubwa katika uwanja huu. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Shahidi Sayyid Asadollah Lajevardi aliteuliwa katika Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Mapinduzi ya Kiislamu. Uteuzui huo ulifanywa na Shahidi Dakta Beheshti aliyekuwa mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran wakati huo. Baada ya hapo akawa mkuu wa shirika la magereza nchini humo. Kundi la munafiqina lilijaribu kumuua mara nyingi hadi akauawa shahidi na mnafiki mamluki akiwa na umri wa miaka 63 mahali pake pa kazi katika soko la Tehran mnamo tarehe ya kwanza ya Shahrivar 1377.
Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 23 Agosti 2003, alifariki dunia Michael Kijana Wamalwa, Makamu wa Rais wa Kenya. Wamalwa alizaliwa 25 Novemba 1944 katika kijiji cha Sosio karibu na Kimilili, wilayani Bungoma. Michael Kijana Wamalwa alikuwa mtoto wa mwanasiasa na mbunge machachari William Wamalwa. Mwaka 2002, Wamalwa akiwa pamoja na wanasiasa wengine mashuhuri nchini Kenya, wakiongozwa na Mwai Kibaki wa chama cha National Rainbow Coalition NARC, walifanikiwa kuung'oa madarakani utawala wa chama cha KANU uliotawala nchi hiyo kwa zaidi ya miongo minne. Kijana Wamalwa alizikwa kwenye shamba lake lililoko Kitale.

Na leo tarehe Mosi Shahrivar katika kalenda ya mwaka wa Kiirani inatambuliwa kuwa ni siku ya kumuenzi Hassan bin Abdullah maarufu kwa jina la Abu Ali bin Sina na inatambuliwa kuwa ni Siku ya Daktari hapa nchini. Abu Ali Sina mwanafalsafa na tabibu mashuhuri wa Kiislamu na Kiirani aliyejulikana pia kwa laqabu ya Sheikhul Rais alizaliwa tarehe 3 Safar mwaka 370 Hijria Qamaria katika mji wa Balkh. Ibn Sina alihifadhi Qur'ani yote alipokuwa na umri wa miaka 10. Msomi na tatibu huyo mashuhuri wa Kiislamu alijifunza tiba baada ya kupata elimu za mantiki, hisabati, nujumu, falsafa pamoja na elimu nyinginezo. Alianza kuandika vitabu akiwa na umri wa miaka 21 na miongoni mwa vitabu vyake maarufu ni Qanun, Shifaa na Isharaat.