Ijumaa Tarehe 19 Mei, 2017
Leo ni Ijumaa tarehe 22 Shaaban 1438 Hijiria, sawa na tarehe 19 Mei 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 850 iliyopita alifariki dunia mfasiri, faqihi, mpokezi wa hadithi na alimu mkubwa wa Kiislamu Ibn Shahrashub. Alizaliwa mwaka 489 katika mji wa Mazandaran ulioko kaskazini mwa Iran na kuaanza kutafuta elimu na maarifa katika kipindi cha utotoni. Bin Shahrashub alikuwa amekwishahifadhi Qur'ani nzima akiwa na umri wa miaka 8. Alipata ruhusa ya kunukuu hadithi za Mtume (saw) kutoka maulamaa wakubwa wa zama hizo kama Zamakhshari, Muhammad Ghazali na Khatib Khorazmi na alikuwa hodari katika kutunga mashairi. Moja ya mashairi yake ya kuvutia ni lile alilotunga akitaja sifa na matukufu ya Mtume Muhammad (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu. Shairi hilo linapatikana katika kitabu cha Manaqib Al Abi Twalib. Mwanazuoni huyo mkubwa ameandika vitabu vingi katika elimu za hadithi na sayansi ya Qur'ani Tukufu.

Siku kama ya leo miaka 713 iliyopita, alifariki dunia malenga na mtu mwenye zuhdi, Shihabu Mahmud. Abuth-Thanai Shihabud-Din Mahmud Bin Sulaiman Bin Fahd Halabi Dimashqi maarufu kwa jina la Shihabu Mahmud, alikuwa malenga na mwandishi mashuhuri katika uga wa upangiliaji maneno katika kipindi chake huku akiwa na uelewa wa historia ya wasomi wakubwa. Katika fani hiyo Shihabu Mahmud aliandika vitabu mbalimbali. Msomi huyo mtajika alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 81 na kuzikwa baina ya milima ya Qasioun, ya mji wa Damascus, Syria.

Siiku kama ya leo miaka 665 iliyopita, alizaliwa mjini Cairo Misri, Ibn Hajar Asqalani, faqih, mwanahadithi, mwanahistoria na mshairi wa Waislamu wa nchini Misri. Alimpoteza baba yake mzazi alipokuwa na umri wa miaka mitano tu na katika umri huo akaanza kujifunza Qur'ani Tukufu pamoja na masomo mengine ya kidini. Kufikia miaka 10 alikuwa amehifadhi Qur'ani nzima na alisafiri katika nchi tofauti kwa lego la kupata masomo ya juu. Alionyesha kipawa na ujuzi mkubwa katika taaluma ya hadithi kiasi kwamba alifahamika kwa jina la Muhifadhi Mkubwa wa Hadithi. Ibn Hajar Asqalani anahesabiwa kuwa mmoja wa waandishi mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu. Ameandika vitabu vinavyopata 150. Miongoni mwa vitabu hivyo ni Lisaan al-Mizaan, Fat'h al-Bari fii Sharh Hadith al-Bukhari na al-Ishara fii Tamyiz as-Swahaba. Ibn Hajar al-Asqalani aliaga dunia mwaka 852 Hijiria.

Siku kama ya leo miaka 496 iliyopita, majeshi ya utawala wa kifalme wa Othmania yaliuteka mji muhimu wa Belgrade, uliokuwa mji mkuu wa Yugoslavia ya zamani. Mwishoni mwa karne ya 14 Miladia Utawala wa Othmania ulianza kusonga mbele katika eneo la Balkan na kuweza kulitawala karibu eneo lote hilo. Miaka 20 baadaye yaani mwaka 1541 utawala huo uliweza kuyadhibiti maeneo ya Hungary.

Siku kama ya leo miaka 255 iliyopita, alizaliwa Johann Gottlieb Fichte mwanafalsafa wa Kijerumani katika familia maskini. Johann alikuwa mmoja wa waasisi wakuu wa harakati ya kifalsafa iliyojulikana kama "German Idealism", harakati ambayo ilitokana na maandiko ya kinadharia na kimaadili ya rafiki yake Immanuel Kant. Johann Gottlieb Fitche aliathiriwa sana kinadharia na mwanafalsafa mwenzake huyo na kumkabidhi baadhi ya kazi zake. Johann Fitche ameandika vitabu vingi muhimu ambapo baadhi ni vile alivyovipa majina kama vile" Foundations of Nature Right, Mustakbali wa Binadamu na makala ya The Way Towards the Blessed Life.

Siku kama ya leo miaka 92 iliyopita, alizaliwa Malcolm X, kiongozi wa harakati za kupigania uhuru Wamarekani wenye asili ya Afrika. Malcolm X alizaliwa katika familia masikitini nchini humo na akiwa na umri wa miaka minne, alishuhudia kijiji chao kikiteketezwa moto na watu wa jamii ya Ku Klux Klan kutokana na mashambulizi ya kibaguzi. Baadaye alienda kujiunga na shule ya kutwa hata hivyo akiwa na umri wa miaka 15 hakuweza kukamilisha masomo yake kutokana na umasikini, hivyo akalazimika kufanya kazi katika mgahawa mmoja ambapo alijikuta akijiunga na utumiaji wa madawa ya kulevya na unyang’anyi. Kufuatia hali hiyo akiwa na umri wa miaka 21 alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kutokana na hali hiyo. Akiwa jela alifahamiana na wafungwa wengi wenye asili ya Kiafrika waliotokana na familia za Kiislamu kama ambavyo pia alikuwa na mahusiano na Elijah Muhammad, kiongozi wa harakati ya siri ya Wamarekani weusi. Mahusiano na kiongozi huyo yaliendelea hata baada ya Malcolm X kutoka jela. Baada ya hapo alianza kusoma na kufanya utafiti mwingi kuhusiana na Uislamu ambapo kwa msaada wa Waislamu alifanikiwa kujenga misikiti miwili katika mji wa Detroit, Philadelphia nchini Marekani.

Na siku kama ya leo miaka 82 iliyopita Thomas Edward Lawrence mwanasiasa na afisa wa ujasusi wa Uingereza alipoteza maisha yake katika ajali ya gari. Lawrence alizaliwa mwaka 1888 Miladia. Katika kipindi cha miaka kati ya 1910 hadi 1914, mwanasiasa huyo wa Uingereza aliwakilisha kamati ya masuala ya akiolojia (elimu kale) na pia kuhudumu huko Iraq, Syria na Palestina. Aidha alikuwa mfanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza na mwaka 1916 aliteuliwa kuwa mkuu wa idara ya ujasusi ya jeshi la Uingereza nchini Misri. Thomas Edward Lawrence alichangia pakubwa kuingia madarakani kwa wafalme Fadhil huko Syria, Abdallah nchini Jordan na Mfalme Abdulaziz huko Saudi Arabia.
