Jumatano tarehe Mosi Aprili 2020
Leo ni Jumatano tarehe 7 Shaaban 1441 Hijria sawa na Aprili Mosi mwaka 2020.
Miaka 442 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa nchini Uingereza William Harvey, tabibu na msomi wa elimu ya tiba. Harvey alianza kufundisha katika chuo kikuu baada ya kuhitimu mafunzo ya tiba na baadaye akaendelea kufanya utafiti katika uga huo. Mwaka 1616 tabibu Harvey aligundua namna damu inavyozunguka mwilini na kuandika makala kuhusu utafiti huo. William Harvey alifariki dunia mwaka 1657.
Siku kama ya leo miaka 205 iliyopita alizaliwa Otto Von Bismarck mmoja kati ya shakhsia waliokuwa na nguvu na ushawishi mkubwa katika karne ya 19 barani Ulaya na Kansela wa Ujerumani aliyepewa lakabu ya 'Kansela Madhubuti'. Alisoma sheria katika Chuo Kikuu cha Gottingen na baada ya hapo kuhudumu kama mwanadiplomasia wa Ujerumani huko New York na Paris hadi mwaka 1862 alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje. Mfalme Kaiser Wilhelm II aliyekuwa mfalme wa wakati huo wa Ujerumani mwaka 1871 alimteua Bismmarck kuwa kansela wa nchi hiyo na alibakia katika nafasi hiyo kwa muda wa miaka 20. Lakini baada ya kushadidi hitilafu kati yake na Mfalme Wilhelm II, Bismarck alilazimika kujiuzulu. Bismarck alifariki dunia Agosti 24 mwaka 1898.
Tarehe Mosi Aprili miaka 75 iliyopita vikosi vya jeshi la Marekani vilifanya mashambulizi makubwa katika kisiwa cha Okinawa huko Japan. Mashambulizi hayo yaliyofanywa na Marekani mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia yanahesabiwa kuwa vita vikubwa zaidi vya baharini na nchi kavu kuwahi kushuhudiwa kati ya Marekani na Japan. Meli 1300 na karibu ndege elfu 10 za kivita za Marekani zilishiriki kwenye vita hivyo vilivyodumu kwa muda wa siku 83. Hata hivyo wajapan walipambana ipasavyo katika vita hivyo kwa ajili ya kulinda nchi yao kwa kadiri kwamba meli 36 za kivita za marekani ziliharibiwa kikamilifu na nyingine 369 kutiwa hasara. Vilevile ndege za kivita 763 za Marekani zilitunguliwa. Wajapan pia walipata hasara kubwa katika vita hivyo kwani wapiganaji laki moja na elfu kumi kati ya wapiganaji wote laki moja na elfu ishirini wa kisiwa cha Okinawa waliuawa au kujeruhiwa.
Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, vibaraka wa utawala wa Baath uliokuwa ukiongozwa na Saddam Hussein walivamia na kuvunjia heshima Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib A.S katika mji mtakatifu wa Najaf na ya Imam Hussein A.S huko katika mji mtukufu wa Karbala, sambamba na kuyakandamiza mapambano ya Waislamu wa kusini mwa Iraq. Wananchi wa Iraq walianzisha mapambano ya kuuondoa madarakani utawala wa kidikteta Saddam Hussein baada ya muungano wa vikosi vya majeshi ya nchi kadhaa kutekeleza oparesheni ya kuwaondoa wanajeshi wa Iraq katika ardhi ya Kuwait. Wakati huo wanajeshi wa Marekani walisitisha oparesheni zao za kijeshi na kuungana na wanajeshi wa Saddam ili kumwaga damu za Wairaqi waliokuwa wakiendesha mapambano huku wakiwa kwenye saumu.