Wasiwasi kuhusu kubadilishwa uongozi barani Afrika kwa nguvu za kijeshi
Siku chache baada ya mapinduzi ya kijeshi nchini Gabon, baraza la kijeshi la nchi hiyo limefungua mipaka yote ya nchi kavu, bahari na anga na kutangaza kwamba lina azma ya kudumisha utawala wa sheria, uhusiano mzuri na majirani zake na nchi zote za dunia sambamba na kutimiza wajibu wa kimataifa wa nchi hiyo.
Jenerali Brice Oligui Nguema, kamanda wa waliopanga mapinduzi na ambaye sasa amechukua mamlaka nchini Gabon, pia amesisitiza haja ya kuejiepusha kufanya uchaguzi wa haraka, akisema: "Baraza la kijeshi litachukua hatua za haraka lakini kwa uthabiti, uvunjaji wa taasisi za serikali ni wa muda tu na baraza limejitolea kupanga upya mfumo wa utawala kwa kutegemea misingi ya kidemokrasia."
Mapinduzi ya kijeshi nchini Gabon yalitokea baada ya kutangazwa ushindi wa Ali Bongo, rais wa wakati huo wa nchi hiyo. Bongo alikuwa anapanga kuendelea kutawala kwa muhula wa tatu lakini jeshi likamuondoa madarakani na kumuweka katika kizuizi cha nyumbani.
Wakuu wa Jeshi la Gabon wanasema kulikuwa na uchakachuaji wa matokeo ya uchaguzi. Wamesema nchi kwa muda mrefu imeharibiwa na ufisadi, utawala usiowajibika na usiotabirika.
Gabon ni nchi ya tatu barani Afrika ambapo, katika miezi michache iliyopita, jeshi limetwaa mamlaka kwa kumuondoa madarakani rais anayetawala.
Kabla ya hapo, wanajeshi waliingia madarakani kupitia mapinduzi nchini Niger na Burkina Faso. Jambo la kuzingatiwa hapa ni kuwa mabadiliko hayo ya utawala kwa nguvu za kijeshi yameungwa mkono na raia. Watu wa nchi hizo ambao wamenasa katika duara la watawala wanaofungamana na nchi za Magharibi hususan Ufaransa sasa wanataka kujikomboa na kupata uhuru kamili kutoka kwa wakoloni wa zamani.
Katika miongo ya hivi karibuni, Ufaransa, ikiwa na ushawishi wake wa kisiasa na kiuchumi katika nchi nyingi za Kiafrika, sio tu imepora rasilimali na utajiri wa nchi hizo, bali pia imeingilia maamuzi ya ndani kwa kujipenyeza katika maamuzi ya serikali, jambo ambalo kwa muda mrefu limewakasirisha wananchi wazalendo katika nchi husika.

Mtaalamu wa masuala ya kisiasa Amaury Coutansais anasema: Afrika inazidi kupata utandawazi na siku hizi marais wa Afrika wameiweka dunia nzima katika hali ya tahadhari kwani chochote kinaweza kutokea.
Naye Antoine Glase, mwandishi wa Kifaransa, pia anasema katika muktadha huu kwamba: Afrika imeingia katika mchakato ambao haiwezekani kurudi nyuma ambapo Ufaransa itafukuzwa kutoka katika nchi za bara hili, kwa sababu ilipaswa kuacha makoloni yake ya zamani huko Afrika Magharibi na Kati miaka iliyopita lakini iliamua kuendeleza jukumu la polisi katika nchi za Afrika na kudumisha vituo vya kijeshi katika bara hili; suala ambalo limesababisha hasira ya umma barani Afrika.
Sasa, kufuatia mapinduzi ya Gabon, suala linalojadiliwa ni iwapo nchi zingine za bara la Afrika zitapitia mabadiliko kama hayo au la.
Inaonekana kwamba raia wengi wa nchi za Kiafrika, ambao hawajaridhishwa na hali ya mambo, wanajaribu kujikomboa kutokana na kuingiliwa na madola yaliyokoloni bara hilo.
Hivi sasa watu wa Afrika wameweza kuamka na kutambua kuwa wana utajiri mkubwa ambao umekuwa ukiporwa na madola ya kikoloni kwa kushirikiana na watawala vibaraka na sasa wamesema imetosha kwani wanataka kuingia katika kipindi kipya cha historia.
Katika uchanganuzi wake wa hali ya Afrika, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron hivi karibuni alisema: "Muungano usioeleweka umeanzishwa kati ya watu wanaojiita Pan-Africanists yaani wanaharakati wa umajumui wa Afrika na mabeberu mamboleo ambao kwa mtazamo potovu wa Macron ni China na Russia. Anasema muungano huo ndio chanzo cha kuenea mapinduzi ya kijeshi katika nchi zinazozungumza Kifaransa zikiwemo Gabon, Niger, na Burkina Faso, Guinea na Mali.
Bila shaka, sio tu nchi za Magharibi ambazo zina wasiwasi kuhusu harakati mpya za wanajeshi kuchukua madaraka kwa nguvu katika nchi za Afrika. Taasisi za kikanda kama vile Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) pia zimeonya kuhusu kutokea mapinduzi katika eneo hilo na hata zinatafakari kuanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya nchi hizo ili kuwarejesha madarakani viongozi waliopinduliwa. Hii ni katika hali ambayo hatua kama hizo za kijeshi zinaweza kuibua vita vikubwa barani Afrika. Aidha, nchi za Kiafrika kimsingi zinapinga ukoloni na zinataka uhuru baada ya miongo kadhaa ya uporaji wa utajiri wao. Kimsingi kile ambacho nchi za Afrika zinataka ni mahusiano yanayozingatia maslahi ya kitaifa, kuheshimiana na uwepo amilifu katika nyanja za kimataifa.