Rais wa Rwanda awafuta kazi wanajeshi zaidi ya 200 wakiwemo maafisa wa ngazi za juu
Rais Paul Kagame wa Rwanda amewafuta kazi wanajeshi zaidi ya 200 wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF), wakiwemo maafisa 21 waandamizi na wa vyeo vya chini.
Taarifa ya kijeshi iliyotolewa jana Ijumaa imeongeza kuwa, miongoni mwa walioachishwa kazi ni Martin Nzaramba na Etienne Uwimana pamoja na maafisa wengine 19 waandamizi na wengine wa vyeo vya chini.
Wakati huo huo Rais Kagame ameidhinisha kusitishwa kandarasi za maafisa wengine 195 ndani ya jeshi la RDF.
Hadi wakati tunapokea habari hii hakukuwa kumetangazwa sababu rasmi za kufukuzwa kazi wanajeshi hao, lakini kwa mujibu wa sheria za Rwanda, wanajeshi wanaweza kufukuzwa kutoka na kutenda "makosa makubwa."
Mbali na mabadiliko hayo, Kagame ameteua waziri mpya na mkuu wa jeshi. Miongoni mwa maafisa wa ngazi za juu waliofutwa kazi katika jeshi la Rwanda ni Meja Jenerali wa RDF Aloys Muganga, Brigedia Jenerali Francis Mutiganda pamoja na maafisa 14 wenye vyeo jeshini.
Mabadiliko hayo ya Kagame yamekuja siku moja baada ya kumteua Juvenal Marizamunda mwenye umri wa miaka 58 kuwa waziri wa 11 wa ulinzi wa nchi hiyo tangu Rwanda ilipopata uhuru mwaka 1962. Mkuu wa Jeshi sasa ni Luteni Jenerali Mubarak Muganga (hana uhusiano wowote na Meja Jenerali Aloys Muganga).
Jeshi la Rwanda RDF linaundwa na vikosi vitatu, huku kikosi cha akiba kikiundwa na wanajeshi wa muda ambao wanaweza kuitwa jeshini wakati wowote inapobidi kufanya hivyo.