Ethiopia yataka juhudi za pamoja za kudumisha amani katika Pembe ya Afrika
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia ametoa mwito wa kuwepo juhudi za pamoja kati ya nchi za Pembe ya Afrika katika kupambana na al-Shabaab nchini Somalia.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, Taye Atske Selassie amesema kuwa, genge la al-Shabaab lina zana na vifaa vya kutosha vya kuliwezesha kufanya mashambulizi mabaya ya kigaidi katika eneo la Pembe ya Afrika akibainisha kuwa, nchi za ukanda huo lazima ziungane zaidi kuliko huko nyuma ili kujilinda mbele ya vitendo vya kigaidi vya al-Shabaab.
Waziri huyo wa mambo ya nje amesema kuwa, Ethiopia imejitolea kwa pamoja kupambana na genge hilo la kigaidi kwa kutoa msaada wa kijeshi usio na kikomo na misaada mingine hadi Jeshi la Taifa la Somalia litakapoweza kukabiliana na changamoto za usalama peke yake. Pia amesema kuwa, nchi za eneo hilo lazima ziongeze juhudi zao ili kukomesha vitendo vya kigaidi vya genge la al Shabab ambalo linafanya njama za kila namna za kuvuruga mafanikio yaliyopatikana katika vita dhidi ya ugaidi katika eneo hilo.
Ameahidi kuwa Ethiopia itaendelea kujenga, kurekebisha na kuimarisha uhusiano na nchi jirani, akibainisha kuwa kuna uhusiano usioweza kuvunjika wa udugu kati ya watu wa eneo hilo.
Matamshi hayo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia yametolewa siku chache baada ya nchi hiyo kukasirishwa na taarifa za kuingia jeshi la Misri nchini Somalia, baada ya Somalia kughadhibishwa na mkataba wa bandari baina ya Ethiopia na eneo Somaliland linalotaka kujitenga na Somalia.