Kamanda wa RSF akiri wamefukuzwa Khartoum Sudan, aapa kujipanga upya
Kamanda wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) Mohamed Hamdan Dagalo amekiri kwamba kundi lake limetimuliwa mjini Khartoum, sehemu ya mji mkuu wa Sudan na kuitaja hatua aliyoiita ni ya kujiondoa kwa hiari, kuwa ni mbinu ya kujipanga upya na kurejea Omdurman, mji mwingine muhimu sana.
Katika ujumbe wa sauti uliosambazwa kupitia Telegram, Dagalo ameviambia vikosi vyake kuwa kuondoka kwao huko ulikuwa ni "uamuzi ulioidhinishwa na komandi ya operesheni za RSF ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kundi hilo. Amesema: "Ninakuhakikishieni tumeondoka Khartoum wenyewe, lakini tutarejea kwa nguvu zaidi." Aidha amesema kuwa vita vya karibu miaka miwili dhidi ya jeshi la Sudan SAF bado viko katika hatua zake za awali.
Matamshi hayo ya Dagalo ni majibu ya kwanza ya moja kwa moja ya RSF kwa madai ya hivi karibuni ya Jeshi la Sudan (SAF) ya kurejesha maeneo muhimu mjini Khartoum, ikiwa ni pamoja na ikulu ya rais na majengo ya serikali kuu.
Tarehe 26 Machi yaani wiki iliyopita, jeshi la SUDAN lilitangaza kuwa limefanikiwa kuudhibiti tena Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum, kitovu cha kimkakati kilichokuwa kinashikiliwa na RSF tangu mwezi Aprili 2023. Baada ya hapo maafisa wa kijeshi wa Sudan wakatangaza kuwa jeshi la SAF hivi sasa linaidhibiti Khartoum yote ambayo ni moja ya miji mitatu katika eneo kuu la utawala linalojumuisha pia miji ya Omdurman na Bahri.
Mgogoro kati ya SAF na RSF uliozuka tarehe 15 Aprili 2023 kutokana na uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi, umeshaua makumi ya maelfu ya watu, kuwafanya wakimbizi zaidi ya watu milioni 15 na kuitumbukiza Sudan kwenye majanga mengi yasiyofidika.